Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Sisi binadamu huwa ni rahisi sana kuanguka kwenye mitego ambayo inatukwamisha kupata mafanikio makubwa. Unapopanga kufanikiwa, unajua kabisa ni nini unapaswa kufanya ili upate matokeo unayotaka.
Lakini inapofika wakati wa kufanya hayo tuliyopanga, huwa hatuyafanyi. Badala yake tunajikuta tukifanya mambo mengine ambayo hayana mchango kabisa kwenye mafanikio tunayoyataka.
Unapanga wewe mwenyewe kwamba utaamka asubuhi na mapema, unaweka mpaka alamu ya kukuamsha. Lakini alamu inapoita unaizima na kuendelea kulala. Unaweka orodha ya majukumu ya kukamilisha kwenye siku yako, siku inaanza, lakini unatingwa na mambo mengi kiasi cha kushindwa kabisa kufanyia kazi orodha hiyo.
Hali hiyo ya kujua cha kufanya, kupanga kufanya lakini kutokufanya imekuwa ndiyo kikwazo kikubwa kwa watu kupata mafanikio makubwa wanayoyataka. Na wengi wamekuwa hawaelewi ni kwa nini inatokea, jambo linalowafanya wawe na hisia kwamba kuna namna wanakwamishwa kufanikiwa.
Lakini ukweli uko wazi, kwa asili, sisi binadamu huwa tunachagua njia rahisi zaidi. Yaani, kunapokuwa na njia mbili mbele yako, moja rahisi na nyingine ngumu, mara zote unajikuta ukitumia njia rahisi. Hata kama njia ngumu ndiyo yenye matokeo bora zaidi.
Kama tunataka kujenga nidhamu kali ya kufanya yale yote tunayopanga, tunapaswa kugeuza hali hiyo ya ugumu. Tunapaswa kufanya kile kinachopaswa kufanyika kiwe ndiyo rahisi kufanya kuliko mbadala uliopo. Yaani tufanye yote ambayo siyo muhimu kwetu kufanya yawe ndiyo magumu zaidi.
Unaweza kuwa unafikiria hilo linawezekanaje, yaani kuamka mapema kuwe rahisi kuliko kuendelea kulala? Jibu ni ndiyo, ipo namna ya kufanya hilo litokee, ambayo ukiweza kuitumia utakuwa na nidhamu kali sana kwenye utekelezaji.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza mbinu ya kugeuza ugumu ili iwe rahisi kwako kutekeleza mambo yote unayopanga bila kubadilisha au kuahirisha.

1. Mazoezi Makali Ya Jeshi La Sparta Yaliyofanya Vita Kuwa Mapumziko.
Kwa mujibu wa mwanahistoria Plutarch, aliyeandika kwa kina historia ya jamii za kale, jeshi la Sparta lilikuwa moja ya majeshi bora sana kuwahi kutokea. Jeshi hilo liliweza kushinda vita nyingi kwa sababu ya ubora ambao jeshi hilo lilikuwa nao.
Ubora wa jeshi hilo la Sparta ulitokana na nidhamu kali sana ya wakati wa mazoezi, ambayo ilifanya vita kuwa sehemu ya mapumziko. Yaani, wakati wa kufanya mazoezi na maandalizi, mambo yalikuwa magumu sana kuliko ilivyokuwa wakati wa vita yenyewe.
Kwa wanajeshi wa Sparta, kipindi cha vita kilikuwa ni kipindi rahisi kwao kuliko kipindi ambacho hakikuwa na vita. Mazoezi ya wakati ambao hawakuwa na vita yalikuwa makali na ya mateso sana. Hilo liliwafanya wanajeshi hao kutokuogopa kabisa vita, badala yake wakawa wanaipenda. Kwa sababu wakati wa vita ulikuwa sehemu ya mapumziko hayo.
Kuna somo kubwa sana la kujifunza kuhusu mafanikio kutoka kwenye jeshi hilo la Sparta. Kuna mambo ambayo tunapaswa kuyafanya ili tupate mafanikio, lakini yamekuwa ndiyo mambo magumu zaidi kwetu kufanya.
Tunachopaswa kufanya ni mambo mengine yote yawe magumu kiasi kwamba kile tunachopaswa kufanya kiwe ndiyo mapumziko. Yaani tunapopanga kufanya kitu, vitu vingine vyote ambavyo siyo hicho kitu viwe vigumu zaidi kufanya na hicho tulichopanga kiwe ndiyo kitu rahisi kwetu kufanya.
Kwa kuweza kufanya hivyo tutaweza kujenga nidhamu kali ya kupanga na kufanya kwa msimamo bila kuacha. Na kwenye vipengele vinavyofuata tutaangalia jinsi ya kutumia mbinu hii kwenye maeneo yote ya mafanikio tunayojenga.
2. Fanya Kutokutekeleza Uliyopanga Kuwe Kugumu Sana Ili Utekeleze Kwa Uhakika.
Umekuwa unapanga mambo makubwa na mazuri ya kufanya, lakini unapofika wakati wa kufanya hutekelezi, kwa sababu ni rahisi zaidi kutokutekeleza kuliko kutekeleza. Ili kuvunja hiyo hali ya kupanga na kutokufanya, unapaswa kufanya kutokutekeleza kuwe kugumu kuliko kutekeleza.
Unapopanga kufanya kitu, panga muda na mahali utakapofanyia kitu hicho. Ukishapitisha kwamba hicho ulichopanga kufanya ndiyo muhimu kwa mafanikio unayoyataka, unapaswa kujidhibiti ili usibadilishe na ufanye kama ulivyopanga.
Na hili utalifanya kwa hatua mbili. Hatua ya kwanza ni kufanya iwe vigumu kubadilisha hicho ulichopanga. Maana hapo huwa ndiyo tunaanguka kirahisi, unapanga cha kufanya na kabla hujakifanya unabadilisha kwa kuona ulichokuwa umepanga hakikuwa sawa. Hapa weka mchakato mrefu na mgumu sana wa kufanya kubadilisha iwe vigumu.
Hatua ya pili ni kufanya iwe vigumu kuahirisha kufanya hicho ulichopanga kwa namna ulivyopanga kufanya. Wakati wa kutekeleza mipango unapofika, huwa yanajitokeza mambo mengine yanayoonekana ni muhimu na rahisi zaidi kuliko uliyopanga. Hilo unapaswa kulivunja kwa kufanya mambo hayo mengine yawe magumu zaidi kufanya kuliko kile ulichopanga kufanya.
Njia ya kuweka ugumu kwenye kutokufanya uliyopanga ni kuwa na maelezo mengi pale unapotaka kwenda tofauti na ulivyopanga. Jiwekee utaratibu ambao kama unabadili kile ulichopanga, ulazimike kuandika maelezo yanayojitosheleza, kueleza kwa kina kile ulichokuwa umepanga na manufaa yake, kisha uelezee cha tofauti unachotaka kufanya na manufaa yake. Kisha utume maelezo hayo kwa mtu ambaye anakuwajibisha, ayapitie kwa kina na aweze kukujibu kwa maandishi pia ndiyo uweze kubadilisha.
Kwa kuangalia huo mchakato wa wewe kuandika maelezo ya kina ya kutetea mabadiliko unayotaka kufanya, yasomwe na mwingine na yeye pia aandike kwa kina, ni zoezi ambalo ni gumu kuliko kutekeleza uliyopanga. Kama huna sababu za msingi za kutokufanya, inakuwa rahisi zaidi kwako kufanya kuliko kuacha. Na hilo litakusukuma kutekeleza yote uliyopanga na kuweza kupata mafanikio makubwa.
Soma #BaruaYaKocha hapa; #BZK150; Tumia Hii Mbinu Ya Kugeuza Ugumu Ili Ujenge Nidhamu Kali Itakayokupa Mafanikio Makubwa