Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Inapokuja kwenye mafanikio, kila ambaye hajafanikiwa, ana sababu zinazoweza kuonekana ni sahihi kabisa kwake kutokufanikiwa. Na sehemu kubwa ya sababu hizo ni hali ya mtu kuwa ameanzia chini kabisa.

Mtu anaweza kuridhika na sababu anazojipa za kutokufanikiwa, lakini huwa kunakuwa na watu wengi ambao wana sababu kama hizo na wamefanikiwa. Hivyo kuanzia chini haiwezi kuwa kikwazo kwa mtu anayetaka kweli mafanikio kuyapata.

Mimi nimejipa wajibu wa kuhakikisha wewe rafiki yangu umefanikiwa. Ndiyo maana nimekuwa nahakikisha chochote kinachokukwamisha nakupa njia ya kukiondoa ili upate mafanikio unayoyataka.

Inapokuja kwenye kuanzia chini kabisa, ambapo ndiyo panaweza kuwa kikwazo kikubwa kwako, kuna mbadala wa uhakika kwako kufanyia kazi. Mbadala huo kamwe hauwezi kushindwa, kwa sababu unaondoa kila kinachokuwa kinakukwamisha.

Kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukushirikisha mbadala huo ili upate mafanikio unayoyataka bila ya kukwamishwa na kitu chochote.

1. Kama Umepewa Karata Mbaya

Mchezo wa karata una funzo kubwa sana kwetu kuhusu maisha na mafanikio kwa ujumla. Kwenye mchezo wa karata, kila mchezaji huwa anapewa karata sawa, kisha kunakuwa na karata ya kuanzisha mchezo. Na hapo kila mchezaji anatakiwa kucheza karata inayoendana na ile iliyoanzisha. Kama karata ulizopewa haziendani na ile iliyochezwa, hauwi mwisho wa mchezo, bali unalamba karata nyingine mpaka upate ile inayofaa kucheza. Kitu cha muhimu ni mchezo unaendelea kwa karata zilizopo au kulamba mpaka kupata karata sahihi za kucheza.

Inapokuja kwenye maisha, watu wanashindwa kutumia kanuni hiyo rahisi ya mchezo wa karata. Wanapojikuta hawana karata za kucheza mchezo ulio mbele yao, wanaona kama wameshashindwa mchezo mzima. Kumbe wanapaswa kuendelea na mchezo, kwa kucheza karata walizonazo au kuendelea kutafuta karata sahihi za kucheza.

Unapojikuta mahali ambapo kinachohitajika ili upate matokeo unayotaka huna, hupaswi kuchukulia kama ndiyo mwisho wa safari yako ya mafanikio. Badala yake unapaswa kufanya kile kilicho ndani ya uwezo wako kufanya kwa hapo ulipo, ili uendelee kukaa kwenye safari hiyo.

Na hapo ndipo tunapoingia kwenye mbadala pekee unaokuwa nao pale unapokuwa unaanzia chini kabisa na unaona huna kabisa yale yanayohitajika kwenye safari ya mafanikio uliyochagua.

2. Mbadala Pekee Ni Kufanya Kazi Kwa Juhudi Zaidi

Fikiria umezaliwa kwenye familia masikini au yenye uwezo wa chini sana. Hukupata nafasi ya kupata elimu ambayo ni bora kiasi cha kujenga uwezo mkubwa. Unatafuta kazi hupati na ukipata kazi malipo yanakuwa ni madogo. Unapoingia kwenye biashara unajikuta unakosa vitu vingi vinavyohitajika, kwa kuanza na mtaji, watu na rasilimali nyingine muhimu.

Unajaribu kupambana utoke kwenye hali hizo, lakini unaona mambo yakizidi kuwa magumu. Watu unaowategemea wawe msaada kwako wanageuka kuwa wanaokukwamisha. Na kila unapojaribu, badala ya kusogea mbele unajikuta ukirudi nyuma.

Kwenye hali kama hizo unaweza kujiona ni mwenye bahati mbaya na ambaye mafanikio siyo fungu lako. Unaweza kushawishika kuridhika na pale ulipo na kuona hiyo ndiyo hatima ya maisha yako.

Habari njema nilizonazo kwako ni kwamba upo mbadala wa kukupa mafanikio hata unapoona kila kitu kimeshindwa. Mbadala huo siyo kitu kipya, na wala siyo utakachokifurahia, lakini ni kitu kinachofanya kazi.

Mbadala pekee ulionao wa kukuwezesha kufanikiwa licha ya kuanzia chini kabisa ni kufanya kazi kwa juhudi kubwa sana. Pale unapojipima na kuona huna kila kinachohitajika ili ufanikiwe, tambua una mbadala mmoja tu, kuweka kazi kwa juhudi kubwa sana.

Huenda siyo kitu ambacho ulitegemea kusikia, hasa pale unapokuwa unadhani kuna siri za mafanikio ambazo bado hujazijua. Lakini huo ndiyo ukweli, ni uamue kama utaufanyia kazi upate matokeo au utaukataa na ubaki kwenye kukata tamaa.

Kitu ambacho kinakuchanganya sana ni kwamba tayari unaona unafanya kazi kwa juhudi sana, ila mambo hayaendi. Hivyo ninapokuambia mbadala pekee ni kufanya kazi kwa juhudi kubwa unakuwa huelewi. Na ukweli ni kwamba, kama unaona unaweka kazi kwa juhudi kubwa na matokeo hayaji, ni kwa sababu kuna namna wengine wanakuzidi kwenye kuweka kazi. Na hapo ndipo unapopaswa kuanzia.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK149; Mbadala Pekee Wa Kufanikiwa Kwa Wanaoanzia Chini Kabisa