Rafiki yangu mpendwa,
Sipendi kuwa mtu wa kuleta habari mbaya kwako, lakini ukweli huwa haujali.
Ukweli huwa unabaki kuwa ukweli iwe unapendwa au haupendwi.

Hivyo badala ya kutumia mbinu ya mbuni, kuficha kichwa kwenye mchanga ili kutokuiona hatari, ni vyema tukaiona hatari na kuchukua hatua sahihi.

Kuna watu huwa wanasema mafanikio hayana fomula. Watu hao huwa hawajui. Kuna vitu ambavyo waliofanikiwa wote wanavyo na kuna vitu ambavyo walioshindwa wanavyo.
Hilo haliwezi kuwa bahati, kuna kanuni inahusika.

Mafanikio ni kama sayansi, yana kanuni ambayo ikifuatwa basi mtu anapata matokeo mazuri bila kujali yuko wapi au tuko kwenye hali gani.
Sheria ya mvutano ya dunia inafanya kazi Tanzania kama inavyofanya marekani. Na hivyo pia ndivyo mafanikio yalivyo, kuna vitu ukivifanya utafanikiwa, iwe upo Tanzania au Marekani. Na kuna vitu ukivifanya utashindwa.

Tumeshajifunza sana vile ambavyo ukifanya utafanikiwa. Leo ni siku ya kujifunza vile ambavyo ukifanya utashindwa ili uweze kuviepuka kama unataka mafanikio kwenye maisha yako.

Kuna tabia kumi ambazo ni sumu sana na zipo kwa wengi walioshindwa. Ukizijua hizi na kuzikana kwenye maisha yako, utaweza kufika kwenye mafanikio makubwa.
Karibu ujifunze tabia hizo kumi.

1. Kutokujitambua.

Kama hujijui wewe ni nani na kwa nini uko hapa duniani, utatumia muda wako mwingi kuhangaika na kila kinachokuja mbele yako.
Kama hujui kusudi la maisha yako na huna ndoto kubwa unazopambana kufikia, utaridhika na chochote kinachokupa chakula na malazi.
Tofauti kubwa ya waliofanikiwa na walioshindwa ni kujitambua.
Tatizo la kujitambua ni kwamba hakuna anayeweza kukufanyia, ni kitu unapaswa kufanya mwenyewe.
Hivyo kama mpaka sasa hujajua wewe ni nani (siyo jina lako wala cheo chako) na uko hapa duniani kwa sababu gani, basi hilo linapaswa kuwa jukumu lako la kwanza.
Wanasema kusudi la maisha ni kuishi maisha yenye kusudi.
Huwezi kufika kwenye mafanikio makubwa kama hujajitambua mwenyewe. Hata ukikutana na bahati nzuri, kama hujajitambua utaishia kuipoteza.
Jitambue na yaishi maisha yako, hiyo  ndiyo njia ya kufikia mafanikio makubwa.

2. Kutokujisomea.

Kujisomea vitabu na kujifunza vitu vipya ndiyo nguvu ya kuleta miujiza mikubwa kwenye maisha yako.
Chochote unachotaka kujua kipo kwenye vitabu.
Changamoto na magumu unayopitia kuna wengine walishayapitia na uzuri ni waliyaandika kwenye vitabu, wajibu wako ni kusoma uzoefu wao na kuchukua hatua kwa hali yako.
Waliofanikiwa ni wasomaji wazuri, wanajua kuna mengi hawajui.
Walioshindwa siyo wasomaji wa vitabu, wanajiambia tayari wanajua kila kitu au hawana muda wa kusoma.
Ni sawa na kukutana na mtu ambaye amekula chakula mara moja na kusema ameshiba milele, hakuna kitu cha aina hiyo, utaendelea kula mpaka siku ya kufa.
Kadhalika unapaswa kuendelea kujifunza kila siku mpaka siku unakufa.
Kama hupendi kujisomea, hakuna namna utafanikiwa.

3. Kutokuweka akiba.

Kama unatumia kipato chote unachoingiza, hakuna namna unaweza kufanikiwa. Haijalishi kipato ni kidogo au kikubwa kiasi gani.
Hebu fikiria mkulima ambaye anakula mavuno yake yote bila kuacha mbegu, hawezi kufanikiwa kwenye kilimo.
Mafanikio yako hasa kwa upande wa fedha hayatokani na kiasi unacholipwa, bali jinsi unavyotumia kiasi hicho.
Kuweka akiba ni tabia unayopaswa kuijenga, hakutegemei kiasi cha kipato unachoingiza.
Usiseme huweki akiba kwa sababu kipato ni kidogo, kama huwezi kuweka akiba kwenye kipato kidogo, hutaweza kuweka akiba kipato kikiwa kikubwa.
Jijengee tabia ya kuweka akiba kwenye kila kipato chako na kisha kuwekeza ili izalishe zaidi. Hiyo ndiyo mbegu ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

4. Kutokujiamini.

Kama hujiamini wewe mwenyewe, hakuna mwingine anayeweza kukuamini. Na kama hakuna anayeweza kukuamini, huwezi kufanikiwa.
Maana chochote unachotaka ni wengine wanacho na watakupa pale wanapokuamini.
Waliofanikiwa wanajiamini mno, wanajiamini kupitiliza. Wakati mwingine wanaigiza kujiamini mpaka wanajiamini kweli.
Angalia timu mbili zinazokwenda kwenye mashindano yoyote, japo kuna moja itashindwa, lakini zote zinaingia uwanjani ziliwa zinajiamini kwa asilimia 100 na bila ya shaka yoyote kwamba zinakwenda kushinda.
Na hata tafiti zinaonesha ushindi huwa unapatikana kabla hata timu haijaingia uwanjani, kutokana na kiwango cha kujiamini.
Kama hujiamini, umeshashindwa kabla hata hujaingia kwenye mapambano.
Jiamini sana, jiamini mpaka wengine waone kama umechanganyikiwa na watakapoona imani yako kwako na kwa mafanikio yako haitikisiki, watakuamini na kuwa tayari kushirikiana na wewe.
Ukijitambua na kujiamini bila ya kuwa na shaka, hakuna kinachoweza kuwa kikwazo kwako.

5. Kulaumu na kulalamika.

Kuwalaumu na kuwalalamikia watu wengine ni kukubali kuyaweka maisha yako kwenye mikono yao na waamue kuyafanya watakavyo.
Huwezi kufanikiwa kama hujashika hatamu ya maisha yako, kama hunayafanya maisha yako kuwa wajibu namba moja kwako.
Kwa lolote linalotokea kwenye maisha yako, wewe ndiye unayewajibika kwa asilimia 100. Usilaumu wala kumlalamikia yeyote.
Siyo serikali, siyo wazazi, siyo ndugu, siyo mazingira na wala siyo hali ya uchumi. Ni wewe ndiye unayewajibika na maisha yako, shika hatamu, chukua hatua sahihi ili ufanikiwe.

6. Kuahirisha mambo.

Unapanga vizuri kitu unachopaswa kufanya, lakini unapofika wakati wa kufanya unaahirisha na kujiambia hujawa tayari, utafanya kesho au wakati mwingine.
Kama unataka kufanikiwa futa kabisa msamiati wa kesho kwenye maisha yako.
Kila unapopanga kitu cha kufanya na wakati wa kufanya ukafika ukajisikia kuahirisha, jiambie nitafanya sasa na kisha anza kufanya.
Huhitaji kufanya kwa kiasi kikubwa sana, wewe anza kufanya na utajikuta unaendelea kufanya.
Nidhamu binafsi ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio yako. Kupanga tu haitoshi, lazima utekeleze kama ulivyopanga.
Usiwe mtu wa kuahirisha, kuwa mtu wa kuchukua hatua.

7. Kutokutoa kafara.

Unataka ufanikiwe halafu hutaki kubadili namna unavyoishi maisha yako. Hiyo ni sawa na kuwa na pipi, unataka kuila lakini pia ubaki nayo.
Hiyo sayansi haipo, kupata bora ambacho huna sasa, lazima upoteze kizuri ulichonacho sasa.
Yote tunayojifunza hapa kuhusu mafanikio, yatafanya kazi kama utakuwa tayari kutoa kafara.
Ili uweze kuweka akiba lazima utoe kafara kifedha, uachane na baadhi ya matumizi mazuri na unayoyapenda ili uweke akiba.
Ili upate muda wa kujisomea, lazima utoe kafara ya muda, uachane na mazuri unayofanya sasa ili upate muda wa kujisomea na kuwa bora zaidi.
Ili uzungukwe na watu sahihi, lazima uwe tayari kuwapoteza wale ulionao sasa.
Kuwa tayari kutoa kafara, kuwa tayari kutengana na unachokipenda sana ili uweze kupata makubwa zaidi.

8. Kutokuwa king’ang’anizi.
Safari ya mafanikio siyo ya njia iliyonyooka. Kuna milima na mabonde na pia kuba kona kali.
Utakutana na vikwazo na changamoto za kila aina. Kama mawazo yako ni mambo kuwa rahisi, hutafika mbali.
Utashindwa, utaanguka, lakini haimaanishi huo ndiyo mwisho wa safari.
Unapaswa kung’ang’ana na kuendelea na safari yako bila kujali nini umekutana nacho.
Ili ufanikiwe, lazima ujipe agano kwamba utapata unachotaka au utakufa ukiwa unakipambania.
Kama una mbadala wa hilo, kama utakutana na ugumu na kukimbilia kufanya kitu kingine, hutaweza kufanikiwa.
Utahangaika na mengi lakini yote utakutana na magumu na kukimbia.
Ng’ang’ana hasa mpaka upate kile unachotaka.

9. Kuamini njia za mkato.

Kama unaamini siku moja utalala masikini na kuamka tajiri basi jua utakufa masikini.
Kama unasubiri ‘zali la mentali’, kwamba ukutane na bahati ambayo itakutoa ulipo na kukufikisha juu unajidanganya.
Kama unaamini kuna siri ulizofichwa ambazo wachache tu ndiyo wanazijua utabaki kwenye mahangaiko.
Kama unadhani waliofanikiwa ni freemason au wana njia zisizo za kawaida ambazo wametumia utahangaika sana na kuendelea kubaki pale ulipo.
Hakuna njia ya mkato ya kufanikiwa, njia ni ndefu na ngumu.
Hakuna siri zozote ulizofichwa, kanuni iko wazi.
Hakuna nguvu zozote za kishirikina, ni kujitambua na kujiamini kupitiliza.
Acha kuhangaika na njia za mkato, tengeneza njia yako na komaa hapo mpaka ufanikiwe.

10. Kuzungukwa na watu wasio sahihi.

Wale wanaokuzunguka na unaotumia nao muda wako mwingi wanaathiri sana maisha yako.
Ukitaka kuthibitisha hili, angalia maisha yako na ya wale ambak unatumia nao muda wako mwingi.
Utagundua hamtofautiani sana, viwango vyenu vya mafanikio vinalingana.
Ili ufanikiwe zaidi, unapaswa kuzungukwa na watu ambao tayari wameshafanikiwa zaidi yako au wako kwenye safari ya kufika kwenye mafanikio makubwa kama wewe.
Najua hili ni gumu kwenye jamii zetu, kuwapata watu sahihi siyo kazi rahisi.
Lakini ipo jamii ya kipekee sana ambayo unaweza kujiunga nayo na ikakusaidia kufanikiwa.
Jamii hiyo inaitwa KISIMA CHA MAARIFA, kama bado hujawa kwenye jamii hiyo, hilo ndiyo linapaswa kuwa jukumu la kwanza kwako.
Tuma ujumbe kwa wasap kwenda namba 0717 396 253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA ili upate nafasi ya kuwa kwenye jamii hii ya kipekee kwako.

Rasilimali muhimu kwa mabadiliko.

Baada ya kujua tabia hizi kumi ambazo ni kikwazo kwa mafanikio yako, kuna rasilimali unapaswa kuwa nazo ili kufanikiwa.
1. Kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA ambacho kitakusaidia kujitambua.
2. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA kitakachokusaidia kuweka akiba na kuwekeza.
3. Kitabu cha TABIA ZA KITAJIRI kitakachobadili mtazamo wako kwa ujumla.
4. Kitabu cha MIMI NI MSHINDI kitakachokufundisha kuishi kwa ushindi.
5. Jamii ya KISIMA CHA MAARIFA itakayokusukuma kufika kwenye mafanikio makubwa.
Kupata rasilimali hizi wasiliana na 0752 977 170.

Nikutakie kila la kheri kwenye safari hii ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako na mshirika wa karibu kwenye safari ya mafanikio,
Kocha Dr Makirita Amani.