Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kama una soma hapa, kuna jambo moja nina uhakika nalo. Kwamba wewe unataka kupata mafanikio makubwa. Na umefungua hapa kwa sababu bado hujafika kwenye yale mafanikio makubwa unayoyataka.
Huenda pia umeshajaribu mambo mengi kwenye safari yako ya mafanikio. Umekimbizana na siri nyingi ulizoambiwa ni za mafanikio. Ukaziona fursa ambazo zimewapa watu matokeo makubwa, lakini ulipozifanyia kazi hukupata matokeo hayo.
Unafika mahali na kushawishika kuamini kwamba mafanikio makubwa siyo kwa ajili yako. Unatafakari maneno mengi ya kukatishwa tamaa ambayo umewahi kuambiwa, na kuanza kuona labda ilikuwa sahihi.
Mimi kama rafiki yako, nataka nikuhakikishie jambo moja, mafanikio makubwa yanawezekana kwako pia. Chochote unachofikiria kukipata kwenye maisha, kinawezekana kabisa. Na haijalishi uko chini au juu kiasi gani, bado una nafasi ya kwenda zaidi ya hapo.
Kitu kikubwa kinachokukwamisha ni kukosa majibu ya maeneo matatu muhimu sana kwenye safari yako ya mafanikio.

Kwenye jambo lolote tunalofanya kwenye maisha, huwa kuna ngazi tatu.
Ngazi ya kwanza, ambayo ni ya nje kabisa ni NINI. Hii ni ngazi ya kujua nini hasa tunachofanya. Hii unaweza kuona ni rahisi, lakini watu wengi sana kwenye maisha hawajui hata ni NINI wanachotaka.
Ngazi ya pili, ambayo ni ya kati ni VIPI. Hii ni ngazi ya kujua jinsi ya kufanya na/au kupata kile unachotaka. Hapa unajua namna ya kupata matokeo unayotaka na ni wachache sana ambao wanafika ngazi hii.
Ngazi ya tatu, ambayo ndiyo ya ndani ni KWA NINI. Hii ni ngazi ya kujua sababu au kusudi la kile unachofanya au kutaka. Hii ndiyo inayokusukuma uendelee na safari hata pale mambo yanapoonekana kuwa magumu.
Ili kupata mafanikio makubwa, unapaswa kuwa na majibu ya maeneo hayo matatu, majibu yanayotoka ndani yako mwenyewe na siyo ya kuiga wengine.
Swali la kwanza; NINI hasa unachotaka kwenye maisha?
Hili ni swali muhimu, ambalo litakuondoa kwenye kukimbizana na kila aina ya usumbufu unaojitokeza. Ndiyo swali litakalokufanya uchague njia moja na kuachana na nyingine nyingi.
Umekuwa unashindwa kupata mafanikio kwa sababu huchagui kimoja unachotaka. Na matokeo yake ni kukimbizana na vitu vingi. Na kama unavyojua, mshika mawili, yote humponyoka.
Ni lazima ujue kile hasa unachotaka kufanya au kupata na kuachana na vingine vyote.
Swali la pili; VIPI unafanya na kupata unachotaka.
Hili ni swali la JINSI YA …. Kujua tu unachotaka, hakumaanishi itatokea kimiujiza. Ni lazima ujue njia na namna sahihi ya kupata hicho unachotaka. Ni lazima upate maarifa na ujuzi utakaokupa matokeo unayotaka.
Wapo watu wanaojua nini wanataka, lakini hawawekezi kiasi cha kutosha kujua JINSI ya kupata kile wanachotaka. Wewe usiwe mmoja wa hao, jua jinsi ya kupata unachotaka na hakikisha unapata kama unavyotaka.
Swali la tatu; KWA NINI unataka unachotaka.
Safari ya mafanikio siyo nyepesi, ina changamoto na vikwazo vya kila sina. Wengi sana wanaoianza safari ya mafanikio huwa wanaishia njiani. Na siyo kwa sababu hawaiwezi safari, bali kwa sababu wanakosa msukumo wa kuvuka wanayokutana nayo.
Unahitaji kuwa na KWA NINI kubwa ndani yako, inayokusukuma kuyapambania mafanikio unayotaka licha ya magumu utakayokutana nayo. Kwa nini ni kujua kusudi la maisha yako na alama unayotaka kuacha hapa duniani.
Bila ya KWA NINI kubwa, unaishia kuiga wengine na kukwamishwa na maoni yao.
Hakikisha una sababu kubwa za kutoka ndani yako zinazokusukuma kupata mafanikio unayoyataka. Hizo ndizo zitakazokuwezesha kupata mafanikio unayoyataka.
Hatua ya kuchukua ili kuijua KWA NINI yako halisi.
Rafiki, kwenye #BaruaZaKocha nimeshirikisha mchakato wa KWA NINI SABA ambao unakuwezesha kujua sababu yako ya ndani ya kufanikiwa.
Mtu yeyote anayefanya mchakato huo wa KWA NINI SABA, hawezi kubaki pale alipo. Na wala hawezi kukwamishwa na kitu chochote.
Karibu usome barua hiyo ya Kocha na uyabadili kabisa maisha yako.
Fungua; #BZK002; Kwa Nini Saba Zitakazokuwezesha Kulijua Kusudi La Maisha Yako.
Nikutakie kila la kheri kwenye kujipa majibu ya maswali matatu uliyojifunza hapa.
Rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.