Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Mwandishi Leo Tolstoy, alianza kitabu chake cha Anna Karenina na sentensi ambayo imekuwa nukuu maarufu sana. Sentensi hiyo inasema; “Familia zote zenye furaha zinafanana; kila familia isiyo na furaha inakosa furaha kwa njia zake yenyewe.”

Inapokuja kwenye mafanikio, hilo linakuwa kinyume. Kupitia historia na uzoefu, tunaweza kusema; ‘Watu wote walioshindwa wanafanana; kila aliyefanikiwa amefanikiwa kwa njia zake mwenyewe.’

Hilo lina ukweli mkubwa na unapoliangalia kwa uhalisia, ndivyo lilivyo. Japokuwa watu wengi hawawezi kulikubali, kwa sababu wanadhani watu waliofanikiwa wanafanana, na ndiyo maana wanakazana kuiga mafanikio na hawayapati.

Kama umekuwa msomaji mzuri wa barua hizi, utakuwa umeshaelewa na kukubali kwamba mafanikio hayafanani na hayawezi kuigwa. Ndiyo, kila mtu anaweza kufanikiwa, lakini atafanikiwa kwa namna na njia zake mwenyewe na siyo kwa kuiga yale yaliyowapa wengine mafanikio.

Lakini inapokuja kwenye kushindwa, sababu zinazopelekea watu kushindwa ni zile zile. Ni sababu ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu na ambazo zinakubalika na wote walioshindwa. Japo wengi hapa huwa wanakataa kukubali, wakiona kushindwa kwao ni kwa kipekee sana na hakuwezi kuelezewa wala kutatuliwa.

Kila mtu anayeshindwa kupata kile anachotaka, kitu cha kwanza huwa anatafuta nani aliyemkwamisha kupata. Na kwa sababu wa kulaumiwa anatafutwa, lazima atapatikana tu. Kama atakosekana kwa watu, basi atapatikana kwa mazingira, hali ya hewa, hali ya uchumi na chochote ambacho kitawafanya watu wajisikie vizuri.

Huwa nasema, kuna watu ambao huwa wana visa ya kudumu ya kupokea lawama pale watu wanaposhindwa. Wazazi ndiyo wanaweza kuwa wanashika nafasi ya kwanza, kwa sababu kila mtu anaweza kupata sababu ya wazazi wake kuwa sababu ya wao kushindwa, hata kama ni kwa mambo yaliyofanyika au kushindwa kufanyika miaka mingi iliyopita. Serikali inashikilia nafasi ya pili, na wakati mwingine inaweza kwenda namba moja, kulingana na wakati. Halafu kuna watu wengine wa karibu, kulingana na ukaribu wao, ndivyo mchango wao unavyoonekana mkubwa.

Kwa upande wa biashara, nako mambo ni hayo hayo. Kila biashara inayoshindwa, sababu huwa zinatafutwa za nje. Washindani hulaumiwa, kwa kushusha bei, kutumia mbinu za ulaghai kuiba wateja na mengine mengi. Kadhalika hali za uchumi na mienendo ya soko vimekuwa vinalaumiwa sana.

Lakini hayo yote siyo sahihi, ndiyo maana pamoja na kuwa na watu na hali za kulaumu, bado wa kushindwa wanashindwa na wa kushinda wanashinda, kwenye mazingira hayo hayo.

Yaani, kwenye hali hizo hizo ambazo zinafanya baadhi washindwe, kuna wengine wanafanikiwa. Siyo kwamba hao wanaofanikiwa wanakuwa na wepesi kwenye mambo ya nje, kote inakuwa sawa.

Kama kuna wanaopata matokeo kwenye mazingira yanayolalamikiwa, bado unaamini mazingira yatakuwa ndiyo tatizo?

Tatizo Ni Kujihujumu Mwenyewe.

Kwenye sayansi, kitu huwa kinaitwa kanuni pale kinapofanya kazi mara zote, maeneo yote na kwa hali zote. Kama kitu kinafanya kazi eneo moja na kwingine hakifanyi kazi, hiyo siyo kanuni au sheria, ni maoni tu.

Kwenye mafanikio, kama kitu kinacholalamikiwa kufanya watu washindwe, kuna wenye nacho lakini wamefanikiwa, haiwezi kuwa kweli kwamba hicho kitu ni kikwazo. Yanabaki kuwa tu maoni ya kujifurahisha, hasa kwa anayekuwa ameshindwa.

Tunapoacha kupokea visingizio ambavyo watu wanatumia kama chanzo cha kushindwa na tukazama ndani zaidi kuona nini ambacho kipo, kuna kitu kimoja kinachoonekana kwa wote wanaoshindwa.

Kwa sababu kitu hicho kinakuwa kwa wote, bado ni ushahidi tosha kwamba hicho ndiyo sababu kuu ya kushindwa. Kitu hicho ni kujihujumu. Watu hawawezi kukubali kwamba wameshindwa kwa sababu wamejihujumu wao wenyewe, lakini huo ndiyo ukweli.

Sababu zinazotolewa na watu, ambazo zinaonekana kushawishi, zinakuwa zimekuja kumalizia tu kile ambacho kimeshaanzishwa. Yaani mtu anakuwa amejihujumu yeye mwenyewe kiasi kwamba ushindani ukija, unamwondoa kwa haraka zaidi. Kama angekuwa hajajihujumu, angekuwa imara kukabiliana na ushindani na kushinda.

Kujihujumu kwenye mafanikio ni kama ukimwi kwenye afya. Mtu akiwa na ukimwi, kinga ya mwili inakuwa dhaifu, hivyo ugonjwa wa kawaida tu unaweza kumuua. Ataonekana amekufa kwa huo ugonjwa, lakini ukimwi ndiyo umechangia kwa kiasi kikubwa.

Hivyo, sababu zote unazoweza kujipa za kushindwa, zinaweza kuwa na ushahidi wa kuhusika kweli. Lakini waliofanikiwa nao wana sababu hizo, ila wamepata ushindi. Kinachowatofautisha hapo ni hali ya kujihujumu. Ukishajihujumu, chochote kitakuangusha, kwa sababu unakosa nguvu ya kupambana.

Huenda bado unaandamana, unagoma kukubali kwamba umekuwa unajihujumu wewe mwenyewe. Wacha nikuonyeshe maeneo ya msingi ambayo umekuwa unajihujumu wewe mwenyewe na uchukue hatua sahihi ili uache kujikwamisha.

1. Unajihujumu Kwa Kupanga Lakini Hutekelezi.

Tuanze na hili jepesi kabisa rafiki. Hebu jipe dakika chache za kutafakari mipango yote mizuri sana ambayo umewahi kuwa nayo kwenye kila eneo la maisha yako. Mimi nakujua wewe rafiki yangu, umewahi kuwa na mipango kabambe sana, ambayo uliona ndiyo mlango wako wa mafanikio ya uhakika.

Unakumbuka malengo mbalimbali umekuwa unajiwekea kila mwanzo wa mwaka? Unakumbuka mipango ya kifedha ambayo umekuwa unajiwekea, kwenye kuongeza kipato, kuweka akiba na kufanya uwekezaji? Unakumbuka mikakati ya kibiashara ambayo umekuwa unaiweka kila unapojifunza?

Umeshapanga sana, lakini kwa nini bado hujapiga hatua kubwa kama ulivyotarajia? Jibu ninalo, hata kabla hujanipa, na unadhani ni jibu sahihi kabisa. Kwamba unasubiri, bado hujawa tayari, kuna vitu vya kujifunza, hujapata mtaji na mengine mengi. Kwa kifupi ni mipango unayo, lakini huitekelezi, kwa sababu kuna vitu unataka viwe kwa namna unavyotaka wewe ndiyo uanze.

Nikuulize kitu kwa mfano, halafu utajipa majibu kama imewahi kukutokea. Unapita mahali mara kwa mara na unaona fursa ya kuanzisha biashara fulani. Unaweka mipango yako vizuri na kujiandaa kuja kuanza biashara hiyo. Siku moja unapita na kukuta mtu mwingine ameshaanzisha biashara kama uliyokuwa unafikiria wewe.

Sasa hapo niambie wewe mwenyewe, nani wa kulaumiwa? Hivi unaweza kumfuata mtu huyo na kumwambia kwa nini umeniibia wazo langu la kuanzisha biashara hapa? Watu watakushangaa. Lakini hivyo ndivyo umekuwa unajihujumu kwenye mambo mengi sana.

Umekuwa unaweka mipango mizuri, unakuja na mikakati ambayo una uhakika wa kupata matokeo. Lakini sasa, inapokuja kwenye utekelezaji, huchukui hatua. Unafurahia sana kupanga, lakini hufanyi utekelezaji wa yale uliyopanga.

Kutokutekeleza uliyopanga ndiyo hujuma namba moja kwenye mafanikio. Na hii haina mwingine wa kumlaumu isipokuwa wewe mwenyewe.

Japo unaweza kujifariji kwamba hujawa tayari na unahitaji rasilimali zaidi, lakini bado haiondoi ukweli kwamba umejihujumu mwenyewe.

Kuacha kujihujumu ni kuanza mara moja utekelezaji wa chochote unachopanga. Hata kama unaona bado hujawa tayari, hata kama unaona kuna rasilimali umekosa, wewe anza kwanza. Mengine utajifunza na kuboresha kadiri unavyokwenda.

Mipango mingi tunayoweka huja kuwa tofauti kwenye utekelezaji. Huenda vingi unavyoona vinakukwamisha visiwe kikwazo kabisa wakati wa kutekeleza. Huwezi kujua hilo mpaka utakapoanza utekelezaji.

Kuanzia sasa acha kabisa kujihujumu kwa kupanga na kutokutekeleza. Heshimu hata muda wako uliotumia kupanga. Tekeleza, hata kama utakosea, utajifunza zaidi kwa kukosea kuliko kutokufanya kabisa.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekuonyesha maeneo mengine manne ambayo umekuwa unajikwamisha kufanikiwa. Unapaswa kuyajua maeneo hayo ili uache kujikwamisha na ujenge mafanikio unayoyataka.

Isome barua hiyo hapa; #BZK053; Ukiweza Kumshinda Adui Huyu Mmoja, Hakuna Kinachoweza Kukuzuia Kufanikiwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.