Habari mpenzi msomaji wa Amka Mtanzania? Heri ya mwaka mpya na karibu tena katika makala yetu ya leo ambapo leo tutajifunza namna gani tunaweza kukabiliana na msongo wa mawazo au njia za kukabiliana na msongo wa mawazo. Msongo wa mawazo ni mambo ambayo binadamu huwa yanamkuta katika maisha yake ya kila siku. Nini maana ya msongo wa mawazo?
Msongo wa mawazo ni mfadhaiko utokanao na shida/taabu, dhiki, matatizo, na mambo mbalimbali.

 
Msongo wa mawazo ni kitu kibaya kwako. Akili yako inapokua na msongo wa mawazo na mwili pia inakua vivyo hivyo. ‘’ Wakati miili yetu na akili inapokea hatari, shinikizo la damu huwa linakwenda juu na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula unashuka chini’’ hayo ni maneno ya mwanasaikolojia Wetter ‘’ when our bodies and minds perceive danger, blood pressure goes up and the digestive system shuts down’’ kwa hiyo miili yetu inapokuwa vema na akili yetu inakuwa vema pia hatuna budi kujifunza namna za kukabiliana na msongo wa mawazo. Zifuatazo ni njia sita za kukabiliana na msongo wa mawazo;
1. Usingizi
Usingizi ni dawa kwa binadamu unatibu mambo mbalimbali katika mwili wako. Unapokuwa umepatwa na msongo wa mawazo unashauriwa kulala usingizi unapolala unaipa akili na mwili wako kupumzika. Ili ufanye akili yako ifanye kazi vema inahitaji usingizi mzuri unaoshauriwa na wataalamu wa afya kuanzia masaa 7-9 kulala zaidi ya hapo ni matatizo. Usingizi una kupa nguvu mpya na akili ya kufanya kazi. Kama ukiwa umechoka muda wote hutoweza kufanya kazi zako kwa ufanisi na hutoweza kuzalisha katika kiwango cha juu. hivyo basi, usingizi ni moja ya dawa katika kukabiliana tatizo la msongo wa mawazo.
SOMA; MSONGO WA MAWAZO; SABABU NAMBA MOJA YA MATATIZO YAKO.
2. Mazoezi
Kama ukiwa na msongo wa mawazo fanya mazoezi. Mazoezi yanasaidia kuongeza nguvu ya akili na kusambaza hewa ya oxygen kwa wingi katika mishipa yako ya damu. Kama unataka kuongeza uzalishaji na kupunguza mawazo fanya mazoezi, kama huwezi kukimbia tembea kwa hiyo mazoezi ni muhimu kwa afya zetu siyo kuondoa msongo wa mawazo bali pia kuimarisha na kuipa akili nguvu.
3. Kula vizuri
Mwili wako unategemea chakula ili uweze kujiendesha kama vile gari lina tegemea nishati ya mafuta ili liweze kufanya kazi. Kama unakula vibaya usitegemee kuwa na afya nzuri, jinsi ulivyo na mwonekano inatokana na vyakula unavyokula. Kula matunda, mboga za majani na vyakula vinavyojenga mwili na siyo vyakula vya kuharibu afya yako, kumbuka kuwa usipo lipia gharama ya afya yako leo utakuja kulipia baadaye kwa kupata magonjwa ambayo yatakutesa katika maisha yako yote ni bora ulipie gharama sasa. Hivyo basi, kula vizuri ni njia nzuri ya kukabiliana na msongo wa mawazo.
4. Soma kitabu
Unapokuwa unahisi kuwa na msongo wa mawazo basi kifanye kitabu kuwa rafiki yako wa karibu. Utasahau yale ambayo yalikuwa yanakusibu. Pia utapata faida nyingi zisizoelezeka pale unapokuwa unasoma kitabu, utapata maarifa mengi ambayo ulikuwa huyajui. Unaposoma soma na akili yako yote iweke katika kitabu na achana na shughuli nyingine utapata matokeo mazuri. Kitabu ni njia ya kuondoa msongo wa mawazo ni njia nzuri ambayo inakupa chakula cha kulisha ubongo wako.
SOMA; Hizi Ndizo Sababu 7 Zinazosababisha Msongo Wa Mawazo.
5. Burudani
Burudani ni njia mojawapo ya kukabiliana na msongo wa mawazo katika maisha yako. Unaweza ukasikiliza muziki mzuri unaoupenda hatimaye ukakuondolea msongo wa mawazo au unaweza kuwa na mtu wako karibu ( mpenzi wako), ukacheza na watoto au mtoto wako ,kuangalia picha katika albamu za kumbukumbu zako za nyuma, kuangalia mpira, kucheza nakadhalika.
Kwa hiyo burudani ina mchango mkubwa katika kukabiliana na msongo wa mawazo.
6. Kubadilisha mazingira
Unaweza kutembelea sehemu mbalimbali kama vile fukwe za bahari, kuogelea katika sehemu zilizoandaliwa yaani swimming pool, kubadilisha mazingira inasaidia pia katika kubaliana na msongo wa mawazo, tembelea mbuga za wanyama, au sehemu zingine zenye vivutio vya utalii. Sehemu zenye mazingira tulivu ya kijani na upepo mzuri zinasaidia kufanya akili yako kuwa mpya na yenye nguvu.
Mwisho, maisha yetu yanahitaji furaha, upendo, amani na afya nzuri itakayotufikisha katika safari yetu ya mafanikio.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com