Maisha ni magumu, lakini ni magumu zaidi ukiwa mpumbavu, ni kauli ambayo mwigizaji John Wayne aliwahi kunukuliwa akisema. Kauli hii ina ukweli mkubwa sana.

Maisha yana changamoto zake, yana magumu yake na hakuna ambaye maisha yake ni rahisi. Lakini pia wapo ambao wanayafanya maisha yao kuwa magumu zaidi ya yanavyopaswa kuwa.

Kwa kukosa maarifa na taarifa sahihi, kwa kukosa misingi imara ya kuishi maisha, wengi wamekuwa wakijikuta kwenye maisha magumu ambayo hawaelewi wanayaendeshaje.

Kwenye kitabu cha Follow Your Heart, mwandishi Andrew Mathews ametushirikisha misingi kumi ya kuishi ambayo itayafanya maisha yetu kuwa rahisi. Misingi hii haitarahisisha maisha, badala yake itatuzuia tuache kuyafanya maisha yetu kuwa magumu zaidi.

Follow-Your-Heart

Katika makala hii nakwenda kukushirikisha misingi hii kumi ambayo kama ukiweza kuiishi, utagundua kusudi la maisha yako na kuwa na maisha yenye furaha na mafanikio makubwa.

Karibu tujifunze misingi hii kumi, njia hizi kumi za kuishi ili kuacha kuongeza ugumu wa maisha yetu wenyewe.

  1. Tupo hapa kujifunza na dunia ndiyo mwalimu wetu.

Maisha ni mwendelezo wa masomo, kila changamoto unayokutana nayo kwenye maisha ni somo unalopaswa kujifunza kwenye maisha yako. Ukitatua changamoto hiyo unakuwa umefaulu somo hilo na hivyo kwenda ngazi ya juu zaidi, kupata changamoto kubwa zaidi. Ukishindwa kutatua utaendelea kupata changamoto hiyo hiyo, hivyo utarudia somo hilo mpaka ufaulu.

Jua kwamba upo hapa duniani kujifunza na usijaribu kukimbia au kukwepa chochote unachokutana nacho, maana hakitaondoka. Pia usifikiri kwa kutatua changamoto moja utakuwa umemaliza kila kitu, bali unakuwa umekaribisha changamoto kubwa zaidi. Masomo ya maisha hayaishi mpaka siku ambayo unakufa.

  1. Dunia haina upendeleo.

Mafanikio na furaha yako kwenye maisha inategemea misingi ya asili ya dunia. Ukiijua na kuiishi misingi hii utakuwa na maisha yenye furaha na mafanikio makubwa. Usipoijua na kuiishi, maisha yako yatakuwa magumu bila ya kujali umetokea wapi na uko wapi.

Dunia haimpendelei yeyote, kama unaona wewe unaweka juhudi sana lakini maisha yako ni magumu, lakini kuna mwingine haweki juhudi kama wewe ila maisha yake ni rahisi, jua kabisa kuna misingi hujaijua na kuiishi.

Jua misingi na iishi, na maisha yako yatakuwa bora sana. Msingi mkuu unaopaswa kuujua kwenye maisha ni sheria ya kupanda na kuvuna, au sheria ya usababishi. Kwamba kila kinachotokea kwenye maisha yako, umekisababisha wewe mwenyewe. Yaani unachoona sasa, ni mavuno ya ulichopanda huko nyuma. Kama unataka matokeo tofauti, basi panda juhudi tofauti.

  1. Maisha yako ni matokeo ya imani zako.

Kile unachoamini kuhusu maisha na dunia kwa ujumla, ndiyo unachopata kwenye maisha yako. Kama unaamini huwezi kufanikiwa basi kamwe hutafanikiwa. Kama unaamini utajiri ni mbaya na matajiri ni watu wabaya basi hutakuwa tajiri. Kama unaamini wewe ni mtu wa kisirani na bahati mbaya, kila kitakachotokea kwenye maisha yako kitakuwa kisirani na bahati mbaya.

Kile tunachoamini ndiyo kinachotengeneza maisha yetu. Mazingira uliyopo ni zao la imani ulizonazo. Anza kubadili kile unachoamini na taratibu utashangaa mazingira yako yanabadilika pia.

SOMA; Mitazamo Hii Mitano (05) Kuhusu Kipato Ndiyo Inakufanya Uingie Kwenye Matatizo Ya Kifedha, Ijue Na Hatua Za Kuchukua Ili Kuondoka Kwenye Umasikini.

  1. Ukianza kujishika na vitu, watu au fedha ndiyo unavuruga kila kitu.

Dhumuni la maisha ni kuthamini kila kitu na kutokujishika na chochote. Ukishaanza kusema hichi ni changu na nastahili kuwa nacho wakati wote, iwe ni fedha, vitu au watu, ndipo mambo yanapokuwa magumu.

Ukianza kusema ili niwe na furaha lazima niwe na kitu fulani, au kiasi fulani cha fedha au niwe na watu fulani, jua kabisa kwamba hutaweza kuwa na furaha.

Thamini kila kitu unachokutana nacho kwenye maisha, kitumie kwa wakati unacho na jua wakati wowote kinaweza kuondoka. Usijishike au kung’ang’ana na vitu. Pia jifunze kutoa kwa wengine, hii itakusaidia kutokujishika na vitu na pia itafungua milango ya kupata zaidi.

  1. Kile unachofikiria ndiyo kinakua.

Kile ambacho unatumia muda mwingi kukifikiria kwenye maisha yako, ndiyo ambacho kinakua zaidi na kuwa maisha yako. Ukifikiri mawazo hasi unapata  matokeo hasi, na ukifikiri mawazo chanya unapata matokeo chanya.

Hivyo unachohitaji kufanya ni muda wote kufikiria vile vitu ambavyo unataka na siyo kufikiria vile vitu ambavyo hutaki. Unapata kile unachofikiri, hivyo hakikisha mawazo yako yametawaliwa na yale unayotaka kwenye maisha yako.

vitabu softcopy

  1. Fuata moyo wako.

Dhumuni lako kwenye maisha siyo kutokuwa na changamoto, bali dhumuni lako ni kuyafurahia maisha, kuhamasika na maisha. Hivyo unapaswa kufanya kile ambacho unapenda kufanya, kile kinachotoka ndani ya moyo wako.

Moyo wako unajua sana kuhusu wewe na maisha yako kuliko mtu yeyote anavyoweza kukushauri. Wewe ndiye unayejijua vizuri, ukijua unataka nini na una uwezo gani.

Fanya kile unachopenda kufanya na weka juhudi zako zote ili kuweza kupata matokeo bora kabisa, na maisha yako yatakuwa ya mafanikio na furaha. Ukifanya kitu kwa sababu tu ya fedha, utazipata fedha lakini maisha yatakuwa magumu sana.

  1. Mungu hatakuambia sasa nimekupa ruhusa ya kufanikiwa.

Kuna watu wamekuwa wanafikiri Mungu amewaadhibu wasifanikiwe, au wanaomba mpaka wasikie sauti ya Mungu ikiwaambia sasa wana ruhusa ya kufanikiwa. Mungu alishakuumba na kukuweka hapa duniani, akiwa amekuandalia kila kitu unachohitaji ili kufanikiwa. Ni jukumu lako kuchukua hatua ili kufanikiwa.

Unachohitaji ni kujipa ruhusa ya kufanikiwa wewe mwenyewe na kutumia kila kinachokuzunguka ili kufanikiwa. Hakuna mwingine anayeweza kukupa ruhusa hiyo ila wewe mwenyewe.

SOMA; Misemo Hii Mitano (5) Inaua Kabisa Ndoto Zako Za Mafanikio, Iepuke.

  1. Ukishindana na maisha, mara zote maisha yanashinda.

Maisha siyo vita, lakini ukitaka kuyafanya vita basi mara zote maisha yanashinda. Ukianza kuangalia kila kinachotokea kwenye maisha yako kama kizuri au kibaya, utapata kila aina ya vitu vibaya.

Kila kitu kinachotokea kwenye maisha kinatokea kama kinavyopaswa kutokea. Jukumu lako ni kuona unakitumiaje ili kupata kile unachotaka wewe, na siyo kupingana nacho au kukataa, kwa sababu kadiri unavyopingana nacho, ndivyo unazidi kukikuza, na mwisho wa siku maisha yatashinda.

Usijaribu kukimbizana na kila kitu kwenye maisha, huwezi kufanya kila kitu, chagua kufanya yale muhimu na pata muda wa kufurahia maisha yako. Ukifa leo dunia haitasimama, kila kitu kitakwenda vizuri kabisa bila ya wewe. Hivyo ishi vizuri, furahia maisha na chukulia kila kinachotokea kwenye maisha yako kama sehemu ya maisha na siyo kizuri wala kibaya.

  1. Njia ya kuwapenda watu ni kuwakubali kama walivyo.

Ukishaanza kusema unawapenda watu kwa sababu wako kwa aina fulani, na ukishaanza kutaka watu wabadilike na kuwa kama unavyotaka wewe ndiyo uwapende, jua hapo hujawapenda watu. Haitatokea kila mtu kwenye maisha yako kuwa kama unavyotaka wewe. Na watu hawatabadilika kwa namna unayotaka wewe.

Kila mtu ana utofauti wake, ana changamoto zake na pia ana mchango fulani kwenye maisha yako. Njia bora ya kuwapenda watu na kujenga mahusiano bora ni kuwakubali kama walivyo, bila ya kutaka wabadilike au wawe kama unavyotaka wewe.

  1. Dhumuni lako kwenye maisha siyo kuibadili dunia, bali kujibadili mwenyewe.

Ni rahisi sana kusema unataka kuibadili dunia, lakini hilo ni jambo ambalo huwezi kulifanya. Dunia haihitaji msaada wako kwenye kuibadili, dunia iko sawa kwa namna ulivyo. Wewe ndiye unayehitaji msaada wa kubadilika, hivyo jukumu lako kubwa ni kujibadili wewe mwenyewe.

Jua ni kitu gani unachohitaji kwenye maisha yako na fanyia kazi kukipata, hicho ndiyo kitakuhitaji wewe kubadilika, kitakuhitaji wewe uwe bora na kuweza kufanikiwa zaidi. Usikazane kubadili dunia, kazana kujibadili wewe mwenyewe na dunia itakuwa bora sana kwako.

Katika mambo haya 10 tuliyojifunza, hakuna hata moja linalokutaka wewe uwe na elimu kubwa, uwe na fedha nyingi au uwe na rangi fulani kwenye ngozi yako. Yote ni mambo ambayo mtu unaweza kuchagua kuyaishi wakati wowote wa maisha yako na maisha yako yakawa rahisi, ukaacha kuyafanya kuwa magumu zaidi.

Ishi misingi hii kumi, fanya mambo haya kumi na itakuwa vizuri kama ukayaorodhesha ili mara kwa mara uwe unajikumbusha, maana ni rahisi sana kusahau na kuanza kurudi kwenye mazoea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog