Mpendwa rafiki,

Usipochukua hatua ya kujifunza basi utabaki kama ulivyo. Mtu ambaye hasomi vitabu basi anajinyima vitu vingi sana kwa sababu kuna vitu vingi vimefichwa katika vitabu ambavyo huvijui. Ama kweli, waswahili wanasema jambo usilolijua ni kama usiku wa giza.

Mara nyingi huwa tunakuwa na hofu ya kuchukua hatua juu ya kitu fulani, huenda ni mazoea yalitokana na tabia ulizotengeneza na kisha tabia zikakutengeneza. Hofu inaua ndoto za watu wengi kuliko hata kifo tunachokijua. Kila siku hofu inaua watu wengi kuliko kifo tunachokijua , watu wanaogopa kuchukua hatua mbalimbali katika maeneo tofauti tofauti katika maisha yao.

Wiki hii nilikuwa nasoma kitabu cha a gift to my children kilichoandikwa na mwandishi Jim Rogers. Mwandishi kupitia kitabu hiki anamwandikia mwanae barua mbalimbali akimuasa mambo mbalimbali katika maisha. Jim Rogers alikuwa ni mwekezaji aliyefanikiwa hivyo anamwandikia na mwanaye barua kumpa mbinu mbalimbali za kuweza kufanikiwa katika maisha.

Kusoma

Kwahiyo, mwandishi anamweleza mwanaye kuwa  umri siyo kigezo cha wewe kutofanikiwa kama  kweli una mapenzi na kile kinachohusu  malengo yako. Mara nyingi huwa tunajidanganya katika jamii zetu kuwa ukiwa na umri mdogo huwezi kufanikiwa na ili mtu afanikiwe anatakiwa awe mkubwa.  Hii imekuwa ni kama laana katika jamii yetu watu wenye umri mdogo kuogopa kuchukua hatua hata muda mwingine kuongelea juu ya mambo ya mafanikio.

SOMA; Njia Kumi (10) Za Kuyafanya Maisha Yako Kuwa Rahisi Bila Ya Kuyarahisisha.

Rafiki, ni watu wa chache katika jamii yetu walioweza kuchukua hatua wakiwa wadogo na kupiga hatua kubwa. Huenda siyo kosa letu kwa sababu hatukuandaliwa kimazingira kwani tumezaliwa katika mfumo ambao hatufundishwi namna bora ya kuanza kuzalisha na kuanza kuwa na mafanikio tokea ukiwa mdogo.

Kitu ambacho kimenishangaza ni mwandishi yeye alianza biashara akiwa ana miaka sita. Hivyo anamsihi mwanaye kuwa hakuna kizuizi cha umri katika mafanikio. Na leo siyo mara yangu kuandika hili nilishaandika hata kitabu moja ya vitabu vyangu kuwa hakuna kizuizi cha umri katika mafanikio. Hivyo wewe kama mzazi unaweza kuanza kumfundisha mtoto wako mambo mazuri yanayohusiana na mafanikio tokea akiwa mdogo.

Usimwache mtoto akue bila kupata msingi wa mafanikio kama wewe ulivyokosa kutoka kwa wazazi wako. Mfundishe mtoto mambo ya fedha, anza kumfundisha jinsi ya kuweka hata akiba na umfundishe njia halali za kupata mafanikio na siyo njia zisizo halali za kupata mafanikio.

Tukiweza kuwaandaa watoto kimafanikio tokea wakiwa wadogo ni rahisi sana kuchukua hatua katika maisha yao huko mbeleni. Ewe mzazi au mlezi mfundishe mtoto wako mafanikio ni wajibu wako wa kuchunga kondoo uliopewa usiwaache wakapotea kwani mchungaji mwema hawezi kuwaacha kondoo wake wakipotea.

SOMA; Jinsi Ya Kumfundisha Mtoto Kuwa Mfikiriaji Bora Na Mwenye Uwezo Mkubwa Akili

Hatua ya kuchukua leo, hakuna kizuizi cha umri katika mafanikio, kama bado hujaanza safari ya mafanikio ukihofia umri ujue unajinyima haki yako ya msingi kabisa. Kwani ni haki yako wewe kufanikiwa kila eneo la maisha yako je unasubiri nini? Unasubiri kupewa ruhusa? Usisubiri kupewa ruhusa wakati sahihi ni sasa.

Mpendwa msomaji, ni haki yako kufurahia mambo mazuri hapa duniani, hujaumbwa kuja kuvumilia bali kuja kufurahia. Maisha ni mafupi sana kuishi katika mtazamo hasi hivyo jiondoe huko kwenye mitazamo hasi na anza kutembea barabara ya chanya ya mafanikio. Kumbuka wewe ni mshindi umezaliwa kushinda.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu  kwa kutembelea tovuti  hii hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana !