Hizi Ndiyo Hatua Nane (8) Za Kutoka Chini Kabisa Mpaka Kufikia Mafanikio Makubwa. Zijue Hapa Ili Uweze Kufanikiwa.

Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi sana wanapenda kufanikiwa kwenye maisha yao, ila wanaopata mafanikio hasa wanabaki kuwa wachache.

Licha ya kuwepo na kupatikana kwa urahisi kwa maarifa yoyote ambayo watu wanahitaji ili kufanikiwa, bado wengi wanashindwa kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.

Katika kupitia maisha ya wale waliofanikiwa sana, nimeweza kukutana na hatua nane ambazo wengi wamepitia, zilizowawezesha kutoka chini kabisa mpaka kwenye viwango vya juu vya mafanikio.

Nilichojifunza kwenye hatua hizi, na kilichonifanya nisukumwe kukushirikisha wewe rafiki yangu ni kwamba hatua za chini ni ngumu na wengi hukata tamaa kabla hawajafika hatua za juu, ambazo ni rahisi zaidi.

Hivyo ninachokuomba rafiki yangu, ni uzisome hatua hizi nane zote, angalia ni hatua ipi ambayo upo kwa wakati huu kwenye maisha yako, na ujue hatua nyingine zinazokusubiri.

Lakini kabla hatujaingia kwenye hatua hizo nane, naomba pia nikukumbushe kitu kimoja, hatua hizi hazitakusaidia kama bado hujajua na kuchagua kitu gani unataka hasa kwenye maisha yako. Kama hujafanya maamuzi nini unataka, nini upo tayari kupigania, nini upo tayari kufia, hatua hizi hazitakuwa na manufaa kwako.

Hivyo rafiki, kama bado hujajua unataka nini na maisha yako, nakushauri usiendelee kwanza, mpaka pale utakapojua kwa hakika nini unataka kwenye haya maisha mafupi uliyonayo hapa duniani.

Na kama umeshindwa kujua wewe mwenyewe, ninaweza kukusaidia, tukafanya kazi kwa pamoja na ukaweza kujua unataka nini na ukasimamia hicho kwa kipindi cha maisha yako yaliyobakia hapa duniani. Kumbuka hakuna kuchelewa, hivyo usihofu pale unapoona labda umri umesogea. Kama ungependa tufanye kazi kwa pamoja ili uweze kujua nini hasa unataka, niandikie ujumbe kwa wasap namba 0717396253 andika unahitaji PERSONAL COACHING na nitakupa maelekezo zaidi.

cropped-mimi-ni-mshindi

Baada ya utangulizi huo muhimu, niende moja kwa moja kwenye hatua nane za kutoka chini mpaka kufikia mafanikio makubwa.

HATUA YA KWANZA; SABABU.

Hatua ya kwanza kabisa, na ambayo wengi wamekuwa wanaishia hapo ni SABABU. Watu wengi huwa wanakuwa na kila aina ya sababu kwa nini hawawezi kufanya au kupata kile wanachotaka.

Mtu anataka kufanya biashara lakini anasema hana mtaji, au hana wazo, au hana watu wa kumsaidia.

Mtu anataka kuandika anasema hana muda, hana utulivu, hana kifaa anachotaka.

Iko hivi rafiki, kila unapochagua kupiga hatua halafu sababu inakuja, usihofu, jua ni namna ya wewe kutaka kutoroka, hivyo ikubali sababu hiyo, halafu jiambie utafanyaje licha ya kuwepo kwa sababu hiyo.

Mfano kama unataka kuanza biashara na sababu ni huna mtaji, basi jiambie ni biashara gani unaweza kuanza bila ya mtaji, na zipo nyingi mno.

HATUA YA PILI; HOFU.

Ukishavuka hatua ya sababu, siyo kwamba mambo yatakwenda mteremko kama unavyotaka. Bali unaingia hatua ya pili ambayo ni hofu. Umeweza kuivuka sababu, hofu inaanza kukuingia.

Umeshavuka sababu kwamba huna mtaji, unapata wazo la biashara ambayo inahitaji mtaji kidogo au haihitaji mtaji kabisa, lakini hofu inakuingia. Je vipi kama utashindwa, au watu watakuchukuliaje ukianza biashara ndogo, vipi kama utatapeliwa? Mawazo ya aina hii na mengine yanakuwa kikwazo kwa wengi kuendelea zaidi.

Dawa ya hofu ni moja, kufanya kile unachohofia kufanya. Ukiisikiliza hofu, hutaweza kufanya chochote, maana hofu huwa haitibiwi na hofu, bali hutibiwa na kuchukua hatua.

SOMA; Usiogope Kuanza Mafanikio Kwa Sababu Ya Kizuizi Hiki

HATUA YA TATU; KUSHINDWA.

Unapokutana na hofu na ukaweza kuishinda, haimaanishi kwamba vikwazo vyote vitaisha. Hapo unakuwa umejiandaa kuingia kwenye hatua ya tatu ya kuelekea mafanikio ambayo ni kushindwa.

Nisikudanganye, utashindwa, utaanguka, ulivyopanga ni tofauti na matokeo utakayokuja kupata. Yale uliyokuwa unahofia yatatokea.

Na hapa ndipo penye kipimo kizuri sana cha mafanikio, maana asilimia 90 ya watu huishia hapa na kwenda kuanza kitu kingine. Lakini wale wanaofanikiwa sana, huwa wanavuka na kwenda hatua ya nne.

HATUA YA NNE; UNG’ANG’ANIZI.

Baada ya kushindwa, unachopaswa kufanya ni kurudia tena kufanya, hata kama umeanguka chini kabisa, unapaswa kujifunza nini kimekuangusha kisha kurudia tena kufanya kile ulichochagua kufanya. Unakumbuka mwanzo nimekuambia unapaswa kuchagua nini hasa unataka kwenye maisha yako, nini upo tayari kupigania, nini upo tayari kufia? Kwa sababu usipokuwa tayari kujitoa hasa, hutaweza kupata unachotaka.

Ung’ang’anizi ni muhimu mno, na ndiyo unaowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa sana kwenye maisha yao.

HATUA YA TANO; MTANDAO.

Baada ya kung’ang’ana kwa muda, kuna wataanza kukuona na wewe utaanza kuwaona pia. Hapa sasa ndipo unapotengeneza mtandao mzuri wa wale wanaofanya unachofanya, na mtandao huu unakuwa nafasi ya wewe kujifunza na kuziona fursa zaidi.

Mtandao huu huwezi kuuona au kuutengeneza awali kwa sababu unakuwa bado hujalipa gharama ya mafanikio. Kabla hujashindwa na ukaweza kuendelea, ni vigumu kuwaona wengine ambao nao wameshindwa lakini wakasimama.

Hivyo kwenye ung’ang’anizi wako, kuna watu utakutana nao, na hao watakuwa fursa nzuri kwako kujifunza na kupata nafasi za kufanikiwa zaidi.

HATUA YA SITA; UNAKUWA BORA ZAIDI.

Kadiri unavyoendelea kufanya, kwanza kuna kitu kinatokea ndani yako, unajiona wa tofauti, unaanza kujiamini, unaanza kuwa na msimamo na kuweza kufanya maamuzi ambayo ni magumu lakini yanaleta matokeo mazuri.

Hii ni hatua ambayo umeshakuwa bora, umeshapitia magumu na kuyavuka na hivyo unakuwa umetengeneza ngozi ngumu, inayokuwezesha kuendelea zaidi.

Katika hatua hii, hakuna anayeweza kukudanganya kwamba kuna njia ya mkato, au kuna fursa rahisi mahali pengine. Hapa unakuwa umeshalipa gharama kubwa kiasi kwamba huwezi kurudi tena nyuma.

SOMA; Piga Hatua Moja Kwa Wakati; Ushauri Muhimu Kwa Mafanikio Kwa Wanaoanzia Chini Kabisa.

HATUA YA SABA; MAFANIKIO MAKUBWA.

Hapa sasa ndiyo kile unachoona kwenye mitandao na kusikia kwenye vyombo vya habari. Unasikia mtu alianzia chini na sasa amefanikiwa sana. Hapa ndipo watu wanaamini kwamba umelala masikini na kuamka tajiri. Hapa ndipo wengi watasema una bahati sana.

Hatua hii ya mafanikio makubwa, ni ile hatua ambayo huweki nguvu kubwa, lakini matokeo unayopata ni makubwa sana. Yaani watu wanaweza kufikiri kuna namna unatumia nguvu zisizoeleweka kupata mafanikio unayopata.

Wasichojua ni kwamba, umeshavuka hatua ngumu sita huko nyuma.

HATUA YA NANE; KURUDIA.

Kama umewahi kuona, wapo watu ambao wanaanzia chini, wanafanikiwa sana, lakini baadaye wanashindwa na kudondoka chini. Kinachotokea ni kwamba wanapofika hatua ya saba wanajisahau. Wanaanza kuona kwamba wameshaijua siri ya mafanikio, wanaanza kuona wao siyo wa kawaida, hakuna kinachoweza kuwaangusha maana wameshafika juu sana. Na hapo ndipo wanapoanguka vibaya sana.

Ukishafika hatua ya juu kabisa ya mafanikio, unahitaji kurudia tena mchakato mzima, unahitaji kuanza miradi mingine, na unapoanza, unaanzia kwenye sababu, hofu, kushindwa, ung’ang’anizi, mtandao na matokeo mazuri. Kitakachokusaidia kwenye marudio ni kwamba utakuwa na uzoefu hivyo haitakuchukua muda mrefu kama wakati unaanza.

Unachopaswa kujua ni kwamba, lazima uwe tayari kurudia hatua hizi saba kwa kipindi chote ambacho utakuwa hai. Jua kwamba mafanikio siyo matokeo, bali ni mchakato. Hivyo usikae kwenye kilele cha mafanikio uliyopata, bali kuwa tayari kuanza tena na tena na tena.

Rafiki yangu, hizo ndiyo hatua nane muhimu kabisa za kutoka chini kabisa mpaka kufikia mafanikio makubwa.

Ningependa kujua wewe rafiki yangu upo kwenye hatua ipi, au hatua ipi imekukwamisha.

Nijibu email hii kwa kuniambia nini hasa unachotaka na maisha yako, kisha niambie umekwama kwenye hatua ipi, na nitaona namna gani bora ya kukushauri ili utoke pale ulipokwama.

Karibu sana rafiki, nasubiri jibu lako ili niweze kukusaidia zaidi.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu

Usomaji

3 thoughts on “Hizi Ndiyo Hatua Nane (8) Za Kutoka Chini Kabisa Mpaka Kufikia Mafanikio Makubwa. Zijue Hapa Ili Uweze Kufanikiwa.

Add yours

 1. Nashukuru sana Kocha kwa kuendelea kuhakikisha ninafanikiwa kutimiza ndoto zangu kubwa.

  Mimi ALIKO MUSA nipo hatua ya kwanza kabisa ya sababu. Mambo niliyochagua kufanya maisha yangu yote hapa Duniani ni kama ifuatavyo:

  1. UANDISHI -Makala, Vitabu Na Mafundisho. 2. UFUGAJI WA SAMAKI, 3. KILIMO CHA MBOGA MBOGA (Organic farming), 4. UFUGAJI WA NYUKI Na 5. REAL ESTATE INVESTMENT.

  Haya matano tu ndiyo nimechagua kuhakikisha kuwa nitapamabana mpaka nifanikiwe katika maeneo haya matano.

  Mambo ambayo bado sijaanza ni REAL ESTATE INVESTMENT, UFUGAJI WA NYUKI, UFUGAJI WA SAMAKI Na KILIMO NA MBOGA MBOGA AU KILIMO BILA KEMIKALI (Organic farming)

  Sababu kubwa ya kutoanza maeneo haya manne ni mtaji kidogo nilionao.

  Kwa sasa nafanya kila kitu ambacho ni Halali kwangu. Nimefungua akaunti ya AIRTEL MONEY kwa ajili ya kutunza mtaji fedha. Laini hii nimeiacha mbali huko Tabora vijijini pamoja na vitambulisho nilivyotumia kufungulia.

  Pia nina akaunti za Benki za wanachuo ambazo hazina makato ya kila mwezi kwa ajili ya kutunzia mtaji fedha.

  Nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kukushirikisha hatua niliyofikia.

  Asante sana.

  Mimi ALIKO MUSA

  Like

  1. Hongera sana Aliko kwa kujua nini hasa unataka kufanya na maisha yako.
   Na vizuri kwa kujua wapi ambapo umekwama.
   Pia vizuri kwa kujua hatua zitakazokutoa hapo na ambazo umeshaanza kufanyia kazi.
   Endelea kuweka juhudi na hakikisha hukwami kwenye hatua yoyote.
   Kila la kheri.
   Kocha Makirita.

   Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: