Mashujaa wamekuwa wachache sana kwenye zama tunazoishi sasa.
Watu wengi wamekuwa wanaishi maisha ya kawaida kiasi kwamba hakuna chochote kikubwa wanachofanya ambacho wengine wanaweza kunufaika nacho na kujifunza kutoka kwao.
Hivyo tumeishia kujifunza kuhusu mashujaa wa zama zilizopita au mashujaa ambao siyo wa kweli, mfano kuangalia tamthilia na maigizo mbalimbali, huwa tunachagua mashujaa wa kuangalia safari yao kupitia tamthilia hizo.
Habari njema ni kwamba, wewe unaweza kuchagua shujaa kwenye maisha yako na ukawa shujaa wa wengine pia. Hatua za safari ya kufika kwenye ushujaa ziko wazi, unaweza kujifunza na ukazitumia kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.
Ray Dalio, kwenye kitabu chake kinachoitwa PRINCIPLES; Life And Work anatushirikisha kuhusu safari ya shujaa. Dhana hii alijifunza kupitia kitabu kinachoitwa The Hero with a Thousand Faces kilichoandikwa na Joseph Campbell.
Kwenye kitabu cha Campbell, alishirikisha hatua 12 za safari ya shujaa kwa kutumia mifano ya watu halisi na hata hadithi mbalimbali. Kanuni hii ya safari ya shujaa ndiyo imekuwa inatumika kwenye maigizo na tamthilia mbalimbali ambazo zimekuwa maarufu sana.
Kwenye kitabu cha Dalio, ameshirikisha hatua 7 muhimu za safari hiyo ya shujaa, ambazo kila mmoja wetu anaweza kuzitumia kufanya makubwa kwenye maisha yake.
Kwenye makala hii tutakwenda kujifunza hatua hizo saba za safari ya shujaa na jinsi ya kuzitumia ili kupiga hatua kwenye maisha yako. kupata uchambuzi kamili wa kitabu cha Principles, jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua; https://www.t.me/somavitabutanzania
SHUJAA NI NANI?
Kabla hatujaingia kwenye hatua za safari ya shujaa, ni vizuri tukamjua shujaa ni nani ili ujue jinsi gani na wewe unaweza kuwa shujaa.
Campbell anasema shujaa ni mtu ambaye ametafuta au kupata au kufanya kitu ambacho kipo nje ya uwezo wa kawaida wa watu kufikia. Ni mtu ambaye ameyatoa maisha yake kwa ajili ya kitu kingine ambacho ni kikubwa kuliko yeye. Shujaa hajakamilika, lakini ameweza kwenda zaidi ya ilivyozoeleka.
Kwa maana hii ya shujaa, unaona kabisa kwamba ni kitu ambacho kinawezekana kwa yeyote na siyo kwa wachache waliochaguliwa. Kwa sababu jambo muhimu kwenye ushujaa ni kwenda zaidi ya kawaida.
Hivyo unaweza kuchagua kuwa shujaa kwenye jambo lolote. Unaweza kuwa shujaa kwenye elimu kwa kupaya ufaulu ambao siyo wa kawaida, shujaa kwenye kazi kwa kutoa matokeo yasiyo ya kawaida, shujaa kwenye biashara kwa kuwa na biashara isiyo ya kawaida na pia unaweza kuwa shujaa kwenye maisha kwa kuchagua kuishi maisha ambayo siyo ya kawaida. Kuweza kuvuka vizingiti vikubwa ambavyo wengi wameshindwa.
Chagua ni eneo lipi la maisha yako unataka kuwa shujaa, kisha fanyia kazi hatua hizi saba na utaweza kufikia ushujaa huo.
HATUA SABA ZA SAFARI YA SHUJAA.
Zifuatazo ni hatua saba za safari ya shujaa, kuanzia anapoanza mpaka anapofika kwenye kilele cha mafanikio. Hatua hizi zinawezekana kwa kila mtu, muhimu ni kuzijua na kuchukua hatua kwenye kila hatua.
Karibu tujifunze hatua hizi saba za safari ya shujaa na yale ya kufanyia kazi ili kufikia ushujaa na mafanikio makubwa kwenye maisha.
HATUA YA KWANZA; WITO WA SAFARI.
Hatua ya kwanza kwenye safari ya shujaa ni wito wa safari, hapa shujaa anakutana na kitu ambacho kinamlazimu abadili aina ya maisha yake. Kabla ha hatua hii, shujaa anakuwa na maisha ya kawaida kabisa, huku akifanya kile ambacho kila mtu anafanya.
Lakini kuna hali ya tofauti inajitokeza ambayo inamlazimu shujaa kubadili maisha anayoishi. Inaweza kuwa ni mambo kuwa magumu na hivyo kuhitaji kubadilika au kuona wengine ambao wamefanya makubwa na yeye akaamua lazima afanye makubwa.
Wito wa safari unaweza kutokana na maumivu ambapo shujaa anashindwa kuyavumilia na hivyo kuhakikisha anayaondoa, mfano kukosa kazi, kupata ugonjwa, kupitia hali ya mateso n.k.
Pia wito wa safari unaweza kutokana na zawadi ambayo shujaa anataka kupata, hapa shujaa anavutiwa na matokeo mazuri ambayo atayapata kwa safari ambayo anaiendea.
Kwa vyovyote vile, safari ya shujaa inaanza pale shujaa anapoamua kwamba hawezi tena kuendelea kama alivyokuwa, lazima afanye na kufikia hatua za tofauti.
HATUA YA PILI; KUVUKA KIZINGITI.
Baada ya shujaa kuamua kwamba hawezi tena kuendelea na maisha yake kama yalivyokuwa awali, anajikita njia panda. Upande wa kwanza ni maisha ya kawaida ambayo ameyazoea, haya yanamvuta kubaki kuwa kawaida. Upande wa pili ni maisha mapya ya safari ya ushujaa, ambayo hajawahi kuyaishi, hivyo yanampa hofu kwa sababu ni kitu ambacho hana uhakika nacho.
Huu ni wakati mgumu sana kwenye safari ya shujaa kufanya maamuzi, kwa sababu anachagua kuiacha dunia aliyoizoea na inayojulikana na kwenda kwenye dunia mpya na isiyojulikana.
Ili safari iendelee, lazima shujaa avuke kizingiti hiki, aamue kuachana na dunia ya kawaida na kwenda kwenye dunia isiyo ya kawaida. Hapa shujaa anakuwa amedhamiria kweli kufika kule anakotaka kufika na kutoruhusu yeyote au chochote kuwa kikwazo.
Wale ambao hawafikii ushujaa, huwa wanashindwa kuvuka kizingiti hiki, wengi wakifikiria kuacha maisha waliyozoea na kwenda kuanza maisha mapya ambayo hawajazoea, inakuwa vigumu kwao kufanya maamuzi.
Lazima wewe uwe tayari kufanya maamuzi kwamba hutaendelea tena na maisha ya zamani, kwamba umechagua maisha mapya na umejitoa kweli kuhakikisha unapata kile unachotaka.
HATUA YA TATU; NJIA YA MAJARIBU.
Baada ya shujaa kuvuka kizingiti, anakaribishwa na uhalisia wa ulimwengu mpya wa safari ya shujaa. Ulimwengu huu siyo rahisi, kwani umejaa majaribu ya kila aina.
Kwanza kabisa shujaa anaanza kupingwa na wale wanaomzunguka, wengi wanamwambia hawezi au haiwezekani, wanamkatisha tamaa kwamba atashindwa na wengine wanamkosoa kwa aina ya njia aliyochagua. Hili linamsumbua sana shujaa, na kuona huenda kuna makosa anafanya.
Pili shujaa anashindwa kwenye mambo mengi anayojaribu, kwa kuwa mengi ni mapya kwake, anakuwa hajayajua vizuri, hivyo anashindwa kwa wengi. Kupitia kushindwa huku ndiyo shujaa anajifunza njia sahihi, anakutana na walimu na mamenta ambao wanamwongoza. Pia shujaa anakutana na marafiki wapya kwenye safari yake ya ushujaa.
Katika hatua hii ya majaribu, shujaa anakutana na watu ambao wanamfanya aijue vizuri dunia, anakutana na watu ambao wanamsaliti, watu ambao walikuwa wanakubaliana naye mwanzo lakini baadaye wanamgeuka.
Hatua hii ya majaribu lengo lake ni kupima kama kweli shujaa amejitoa kufikia ushujaa. Kwa wale ambao hawajajitia kweli, hawawezi kuvuka hatua hii. Lakini pia hatua hii inamfanya shujaa kuwa imara zaidi kwa hatua zinazofuata kwenye safari hii.
HATUA YA NNE; ANGUKO KUU.
Majaribu ambayo shujaa anayapitia kwenye hatua ya tatu ni makubwa na magumu, lakini siyo hatari sana. kwenye hatua ya nne, shujaa anakutana na anguko kuu. Hapa shujaa anafanya makosa ambayo yanaharibu kabisa safari yake, yanabomoa kila ambacho alikuwa amejenga. Katika hatua hii, shujaa anapoteza kila kitu na analazimika kuanza upya.
Hatua hii huitwa kufa na kuzaliwa upya. Hapa shujaa anayazika kabisa maisha yake ya awali na kuja na maisha mapya, shujaa anakuwa amezaliwa upya.
Shujaa anapofika kwenye anguko kuu, anatumia masomo yote aliyojifunza kwenye hatua ya majaribu na kuanza upya. Kwa kuwa shujaa alishajijengea misingi kwenye hatua za nyuma, anapoanza upya hachukui muda mrefu kama awali, badala yake anafuata misingi aliyojifunza na kuweza kurudi juu haraka.
Anguko kuu ndiyo linalomzika au kumzaa shujaa upya. Wale wanaovuka anguko hilo ndiyo wanafika kwenye ushujaa. Wale ambao anguko hili linawazika kabisa wanapotea.
Jiandae kwa anguko hili kama bado hujalipitia kwenye safari yako ya mafanikio, lakini lisikutishe, kwa sababu ndiyo linakuzaa upya kama shujaa.
SOMA; Kata Mguu Kuokoa Maisha; Maamuzi Magumu Unayopaswa Kufanya Ili Kufanikiwa.
HATUA YA TANO; MAGEUZI.
Shujaa anapovuka hatua ya nne ya anguko kuu, anapata mageuzi makubwa kwenye maisha yake, anakuwa kama nyoka ambaye amejivua magamba au nzige ambaye ametoa jumba lake la zamani na kutengeneza jumba jipya (metamorphosis).
Hapa ndipo shujaa anapozaliwa, kwa kuvuka anguko kuu na kuweza kujenga upya kila ambacho amekipoteza kwenye anguko hilo.
Katika hatua hii, shujaa hana tena analohofia, kwa sababu ameshakutana na makubwa ambayo hajawahi kukutana nayo. Tunaweza kusema shujaa amekutana na kifo uso kwa uso na kukishinda, hivyo hana tena anachohofia.
Kufikia hatua hii, shujaa anachagua kuishi maisha yake kwa kile ambacho ni sahihi na hajali tena wala kusumbuka na mambo ambayo yalikuwa yanamsumbua awali, mfano kuwafurahisha wengine au kutaka kupendwa na wengine.
Anguko kuu linakuwa limembadili kabisa shujaa na kumfanya ajue hana muda wala nguvu za kuhangaika na kila kitu, badala yake anapaswa kukazana na safari yake ya kuelekea kwenye ushujaa na mafanikio makubwa.
HATUA YA SITA; KUIJUA SIRI.
Mageuzi ambayo shujaa anayapitia baada ya kuvuka anguko kuu yanamfundisha shujaa siri kuu ya mafanikio. Hapa shujaa anakuwa amejifunza kilicho sahihi na kisicho sahihi kufanya kwenye safari yake ya ushujaa. Hivyo anajijengea misingi ambayo anaifuata kila wakati na ambayo inamzuia asirudi tena kwenye anguko kuu.
Hapa shujaa anakuwa ameijua kanuni kuu ya mafanikio na kuifuata kila wakati, kitu ambacho kinampa matokeo mazuri kila wakati.
HATUA YA SABA; KUFUNDISHA WENGINE SIRI.
Hatua ya mwisho kwenye safari ya shujaa ni kuwafundisha wengine ile siri ambayo amejifunza kwenye safari yake ya ushujaa. Kadiri shujaa anavyoendelea kufanikiwa, mafanikio yake binafsi yanakuwa hayampi kuridhika kama ilivyokuwa awali.
Kuwaona wengine nao wakifanikiwa linakuwa ndiyo lengo jipya la shujaa, hivyo anawashirikisha wengine siri na misingi ya mafanikio ambayo amejifunza na imemsaidia. Hapa ndipo shujaa anapotumia safari yake kuwasaidia wengine kufanikiwa bila kupitia magumu ambayo yeye ameyapitia.
Katika hatua hii pia shujaa anatumia mafanikio yake kuwasaidia wengine. Kama ni mali anatoa misaada kwa wengine, misaada ambayo inawajengea wengine uwezo wa kupiga hatua kwenye maisha yao pia.
Shujaa akishafundisha wengine siri na misingi ya mafanikio na kuwasaidia wengine kufanikiwa kama alivyofanikiwa yeye, anakuwa huru na maisha yake. Anaweza kuchagua kuishi kama atakavyo yeye na kifo siyo hofu tena kwake, kwa sababu ameshaona na kufikia kila ambacho angeweza kufikia kwenye maisha yake na hata kuwasaidia wengine pia.
Kwenye hatua ya saba, ndipo maisha ya shujaa yanakamilika, na kila alichopitia kwenye safari hiyo kinakuwa na maana kwake na kwa wengine pia.
Rafiki, hizo ndizo hatua saba za safari ya shujaa, leo napenda nikuache na maswali muhimu ya kutafakari na kisha kuchukua hatua ili ufike kwenye ushujaa na mafanikio makubwa;
- Ni eneo gani ambalo umechagua kufikia ushujaa na mafanikio makubwa?
- Kwa sasa upo kwenye hatua ipi ya safari ya ushujaa?
- Je umejitoa kweli kwa ajili ya safari hii? Upo tayari kuvuka yote utakayokutana nayo ili kufikia ushujaa?
Jipe maswali ya majibu hayo, na itapendeza kama utayaandika kabisa kisha yaishi majibu hayo katika safari yako ya kuelekea kwenye ushujaa na mafanikio makubwa.
Kupata uchambuzi kamili wa kitabu PRINCIPLES; Life and Work cha Ray Dailo ambapo ametushirikisha misingi sahihi ya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha, fungua hapa; https://www.t.me/somavitabutanzania kisha jiunge.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania