Karibu mwanamafanikio kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kupiga hatua kwenye maisha yetu na kufanikiwa.

Changamoto huwa hazikosekani na hizi ndizo zinazotuwezesha kujisukuma zaidi ili kuweza kufanikiwa. Changamoto zinaweza kuanzia nje au ndani.

Watu wengi wamekuwa wanaona changamoto za nje, lakini siyo za ndani. Hivyo changamoto za ndani zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wengi kufanikiwa.

Leo tunakwenda kupata ushauri kwenye moja ya changamoto za ndani kuhusu eneo la uandishi.

uandishi.jpeg

Kama wewe ni mwandishi au umekuwa unafikiria kuandika, basi ushauri wa leo ni maalumu kwa ajili yako, usome na kufanyia kazi. Na hata kama siyo mwandishi, bado ushauri huu utakusaidia kuvuka changamoto zinazoanzia ndani yako na kupata msukumo wa kuchukua hatua bila kujali wengine wanakuchukuliaje.

Karibu tupate maoni ya mwanamafanikio mwenzetu ambaye aliandika kuomba ushauri juu ya changamoto ya ndani yake katika uandishi.

Habari kocha,

Naomba ushauri wako. Nimeanza kuandika kitabu juu ya mafanikio ya kifedha kwa Wakristo. Kitabu hiki kinalenga kutoa elimu ya msingi ya fedha kwa mtazamo wa Kikristo (kibiblia).

Baada ya kuanza kuandika nimepata wasiwasi kama kitabu hiki kitapata soko. Wasiwasi wangu unatokana na ukweli kwamba, mimi binafsi bado sijafanikiwa sana kifedha. Ninayo maarifa ya kutosha juu ya elimu ya fedha kutokana na kusoma vitabu na kuhudhuria semina mbalimbali. Tayari nimeshaanza kufanyia kazi maarifa hayo na nina uhakika baada ya miaka michache ijayo yataniwezesha kuwa tajiri na huru kifedha kupitia miradi mbalimbali ya kuniingizia kipato ambayo nimeianzisha. Hivyo, nimeona haja ya kuwashirikisha wengine elimu hiyo kupitia kitabu.

Hata hivyo, kwa sasa bado sina mafanikio makubwa yanayoonekana wazi kiasi cha kutosha kuwafanya watu wavutiwe kusoma kitabu changu maana miradi yangu bado haijaanza kuzaa matunda. Wasiwasi wangu ni kwamba watu wanaonifahamu na hawajui mipango gani naifanyia kazi, watakuwa wanaangalia maisha yangu ya sasa na kulinganisha na kile nilichokiandika watajua ni nadharia tu na hivyo wanaweza wasinunue kitabu hicho. Watu wanaweza kuwa wanajiuliza  “kama aliyoyaandika yanafanya kazi kwa nini yeye hayajamsaidia?”

Baada ya kutafakari juu ya hilo, nimepata mawazo mawili. Ama nisubiri kwanza nifikie mafanikio ya yanayoonekana ndipo niandike kitabu au niendelee kuandika kwa kuwa nilishaanza lakini nikitoe baada ya kuwa na mafanikio yatakayowavuta watu kununua kitabu.

Naomba ushauri wako katika hili.

Simeon

Kama tulivyosoma alichoandika mwanamafanikio mwenzetu hapo juu, amekwama kwenye uandishi kwa sababu kile anachotaka kukiandikia, bado yeye mwenyewe hajakifikia. Hivyo anafikiria kuacha kuandika mpaka pale atakapofikia kile anachotaka kuandikia.

Hivyo swali hapa ni je unawezaje kuandika kuhusu mafanikio au utajiri iwapo wewe mwenyewe bado hujafanikiwa na kuwa tajiri?

Hapa nakwenda kukushirikisha jinsi unavyoweza kuandika kuhusu kitu chochote, hata kama wewe mwenyewe bado hujawa na kitu hicho, na nitakuonesha aina mbalimbali za uandishi ambapo utachagua inayokufaa wewe kwa hali uliyonayo.

Karibu tujifunze jinsi tunavyoweza kuandika chochote hata kama hatujawa na uzoefu nacho.

Moja; Uandishi Ni Kama Uzazi.

Mwandishi wa kitabu cha The War of Art, Steven Pressfield anatuambia kwamba uandishi ni sawa na uzazi. Unapopata wazo la kuandika kitu, ni sawa na mwanamke ambaye amebeba ujauzito. Unapofika wakati wa kujifungua hakuna kinachoweza kuzuia asijifungue, iwe ni uzoefu au mazingira, wakati ukifika umefika.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye uandishi pia, pale unapopata wazo la kitu unachotaka kuandika, ni kama asili inakupa jukumu au kusudi la kufanyia kazi. Hivyo asili inakutumia wewe kama chombo cha kuwasilisha maarifa ambayo tayari yapo kwa namna rahisi kwa watu kuelewa.

Kama ambavyo mwanamke anazaa watoto, siyo kwa ajili yake bali kwa ajili ya asili kuendelea, ndivyo pia waandishi tunavyofanya kazi zetu, siyo kwa ajili yetu, bali kwa ajili ya asili kufikisha ujumbe kwa wengi.

Kwa kujua hili, unakuwa huru kuandikia wazo lolote ulilonalo, kwa sababu unajua wazo hilo siyo kwa ajili yako binafsi, bali ni kwa manufaa ya wengine. Unaweza kuwa hujafanyia kazi wewe, lakini umefanyia utafiti na mwingine akatumia na kunufaika sana. Hivyo kama hutaandika, utakuwa mbinafsi ambaye umewanyima wengine fursa ya kujifunza na kuwa bora.

SOMA; Nipe Fedha, Au Nipe Muda (Majibu Sahihi Kwa Wale Wanaokubeza Kwa Kutoza Huduma Unazotoa).

Mbili; Andika Kile Ambacho Ungependa Kusoma Lakini Hupati.

Sheria ya kwanza kwenye uandishi ni kuandika kitu ambacho ungependa kukisoma, lakini umekitafuta na hukipati. Kama unaandika kitabu au makala, basi hakikisha ni kitu ambacho wewe mwenyewe uko tayari kukisoma na kujifunza.

Tukitumia mfano wa kitabu anachotaka kuandika mwenzetu, cha elimu ya fedha kwa misingi ya Kikristo. Kama wewe ni Mkristo lakini una changamoto za kifedha, na unajiuliza Ukristo wako una mchango gani kwako kufikia utajiri, unatafuta vitabu juu ya hilo hupati. Hapo unachagua kuandika kitabu ambacho wewe mwenyewe utakuwa unakisoma na kujifunza.

Kwenye uandishi kuna kitu kimoja, wakati umetuliza akili yako na kuandika, kuna mawazo huwa yanakujia ambayo baadaye ukija kusoma ulichoandika unajifunza vitua ambavyo ulikuwa hujui. Hivyo unapoandika kitabu ambacho wewe mwenyewe unapenda kukisoma na kujifunza, unakuwa umejipa manufaa mwenyewe kabla hata ya wengine.

Pengine kuna kitu umekwama kwenye maisha yako, ukaamua kutafuta maarifa sahihi hivyo ukafanya utafiti mwingi. Ni dhahiri kwamba hutakumbuka utafiti huo uliofanya milele, hivyo unaweza kukusanya matokeo uliyopata kwenye kitabu, ambacho wewe mwenyewe utakuwa unairejea na pia unaweza kuwauzia wengine nao wakajifunza.

Tatu; Aina Tatu Za Uandishi.

Kuna aina tatu za uandishi na kila aina ina mahali ambapo wewe mwandishi unasimama katika kufikisha ujumbe wako kwa hadhira yako.

Aina Ya Kwanza; Mwanafunzi.

Hapa wewe unakuwa ni mwanafunzi ambaye unajifunza misingi na njia sahihi za kufanya kitu. Kisha yale unayojifunza unayaweka kwenye mfumo ambao ni rahisi kwako kufanya rejea na kuelewa kile ulichojifunza. Rejea hiyo inaweza kuwa kwenye mfumo wa makala au kitabu, ambapo wengine pia wanajifunza.

Kumbuka wakati uko shuleni au chuoni, kuna watu ambao walikuwa wanasoma vitabu vikubwa, wanaandaa notisi za kufanya rejea, halafu wengine wanawaomba notisi hizo nao wasome. Hivi pia ndivyo unavyoweza kuwa kama mwandishi, unajifunza na kuwashirikisha wengine yale ambayo umejifunza na wao wakajifunza pia.

Kama mwanafunzi unawaambia wasomaji wako haya ndiyo niliyojifunza na ninaoyafanyia kazi, karibu na wewe ufanyie kazi.

Aina Ya Pili; Mtafiti.

Hapa unaandika kama mtafiti ambaye anakutana na swali au hali fulani ambayo inamfanya atake kujua kwa undani, kisha unafanya utafiti na kuripoti matokeo ya utafiti wako.

Kama mtafiti siyo lazima ufanyie kazi kile ambacho umetafuta, wewe unasukumwa na kujibu swali kwa nini hali fulani iko kama ilivyo.

Mfano umeona Wakristo wengi wanaona utajiri ni dhambi na umasikini ni usafi. Hili linaweza kukupa swali, je ni kweli? Na je nini kimepelekea watu kuamini hivi? Na hapo sasa unaingia kwenye utafiti wako, unasoma Biblia kwenye maeneo yote ambayo yanazungumzia utajiri na umasikini. Unawafuatilia waandishi bora wa Kikristo, unafuatilia misingi ya kanisa pamoja na viongozi mbalimbali walioleta mabadiliko kwenye dini hiyo.

Baada ya utafiti wako wa kina, unakuja na majibu kwa nini hali iko kama ilivyo, ukweli ni upi na hatua sahihi za kuchukua ni zipi.

Kama mtafiti unawaambia wasomaji wako kutokana na utafiti niliofanya, ukweli ni huu na hatua sahihi za kuchukua ni hizi, ukiambatanisha ushahidi.

Aina Ya Tatu; Mzoefu.

Hapa unakuwa na uzoefu kwenye jambo fulani na kisha unaandika kushirikisha uzoefu wako. Hapa sasa ndiyo unakuwa umefika au kufanikiwa kwenye eneo fulani na kisha kuwashirikisha wengine jinsi ulivyofika pale, ukiwaonesha njia ambazo wanaweza kupita na kufika pale ambapo umefika.

Kwenye uandishi huu, unashirikisha kile ambacho wewe unajua na kimefanya kazi kwako na hatua za wengine kuchukua kama wanataka kufika ulipofika wewe.

Kama mzoefu unawaambia wasomaji wako hivi ndivyo nilivyofika hapa nilipo sasa, kama na wewe unataka kufika, fanya hivi.

Ni aina ipo bora zaidi?

Hakuna aina ya uandishi ambayo ni bora kuliko nyingine, kila aina ina uimara na udhaifu wake.

Kama mwanafunzi kuna uimara wa kujifunza na kuchukua hatua, lakini udhaifu wake ni kufanya majaribio mengi na kushindwa mara nyingi kabla hujafanikiwa, hivyo wewe na wasomaji wako mnahitaji uvumilivu.

Kama mtafiti kuna uimara wa kuujua ukweli baada ya kuangalia vyanzo sahihi kwa kina, lakini udhaifu wake ni utafiti kushindwa kuendana na uhalisia, hasa pale mazingira ya chanzo cha maarifa yako yanatofautiana na eneo la utekelezaji.

Kama mzoefu kuna uimara wa kuwa na uzoefu halisi katika kufanya kitu husika hivyo siyo nadharia wala kujaribu, lakini udhaifu wake ni kutokuweka nafasi ya bahati na kushindwa kujua kwamba kilichofanya kazi kwa mtu mmoja, kinaweza kisifanye kazi kwa mtu mwingine. Kwenye mafanikio ya kila mtu, kuna bahati fulani anakuwa amekutana nayo, lakini kwenye kuandika kuhusu mafanikio yao, wengi huwa hawaelezi bahati hizo, hivyo kuwapotosha wale wanaojifunza kwao.

Hivyo chagua ni aina ipi ya uandishi ambayo utaifanya, na hakikisha wasomaji wako wanaelewa wazi unasimama wapi na wajue nini wanategemea kutoka kwako.

SOMA; Hatua Saba (07) Za Safari Ya Shujaa Na Jinsi Ya Kuzitumia Kupata Chochote Unachotaka Kwenye Maisha.

Nne; Tambua Upinzani Upo Kazini.

Kwenye kitabu cha The War of Art mwandishi Steven Pressfield anaendelea kutuambia kwamba kila unapotaka kufanya kazi yoyote ile ya sanaa au ubunifu, kuna nguvu fulani inajitokeza na kukupinga usichukue hatua. Nguvu hii inaweza kuanzia ndani yako au nje yako. Steve anaiita nguvu hii UPINZANI (RESISTANCE) na kwenye kitabu hicho amejadili kwa kina dalili za nguvu hiyo na jinsi inavyotuhadaa tusifanye kazi za kibunifu (NB; Uchambuzi wa kina wa kitabu hicho utapatikana kwenye www.t.me/somavitabutanzania usiukose)

Unapopata wazo la kuandika, halafu sauti ndani yako inakuambia hustahili kuandika kwa sababu bado hujawa kile unachoaka kuandika, jua ni upinzani upo kazini. Kwa kuwa unakaribia kufanya kazi ya kibunifu, upinzani unakuja na kila hila kuhakikisha hufanyi kazi hiyo.

Steve ameeleza kwa kina jinsi nguvu hii inafanya kazi, anasema unaweza kujipanga kabisa kwamba utaandika na hakuna kitakachokuzuia, mara ghafla mtu wa karibu anaugua na inabidi uwe karibu naye, akipona mwingine anaingia kwenye matatizo inabidi umsaidie. Yaani ni drama juu ya drama, lengo ni wewe tu usiandike.

Hivyo kama unataka kuandika, au kufanya kitu kingine chochote kile, amua kufanya na puuza sauti ya ndani au ya nje inayokuzuia usifanye ulichopanga. Jitoe kufanya na fanya kweli, utashangaa unapoanza kufanya sauti hizo zinakimbia zenyewe.

Tano; Huwezi Kumridhisha Kila Mtu.

Upo usemi kwamba haijalishi unafanya nini, theluthi moja ya watu watakukubali, theluthi moja watakupinga na theluthi moja hawatajisumbua na wewe, yaani watakupuuza.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye uandishi, haijalishi umeandika nini na wewe umefika wapi kwenye kile ulichoandika, kuna watu watakubaliana na wewe na kujifunza, kuna ambao watakupinga na kuna wengi ambao hawatajali umeandika nini.

Lengo lako ni kwenda na wale ambao wanakubaliana na kile unachofanya na kuwapa kwa namna ambayo itawasaidia. Usijisumbue kabisa na wale wanaokupinga, hakuna namna unaweza kuwageuza.

Ukiandika kabla hujapata kile ulichoandika wanaokupinga watasema anajua nini huyo, ameandika nadharia tu.

Ukisubiri mpaka ufanikiwe ndiyo uandike wanaokupinga watasema alichoandika siyo sahihi, kuna siri amezificha, hawa watu waliofanikiwa hawatoagi siri zao.

Usipoandika kabisa wanaokupinga watasema wewe ni mbinafsi, unajua mambo mengi lakini hutaki kuwafundisha wengine.

Hivyo chagua unataka kufanya nini, walenge wale wanaokubaliana na wewe na hao wengine achana nao.

SOMA; Unastahili Kulipwa, Usione Aibu Kuwaambia Watu Wakulipe.

Sita; Nabii Hakubaliki Kwao.

Hii ni kauli maarufu sana na ambayo ipo kila mahali, lakini huwa tunasahau kuiangalia.

Iko hivi rafiki, watu wako wa karibu, ndugu, jamaa na marafiki, siyo wanunuaji wazuri wa chochote unachouza. Watu wa mbali kabisa watanunua na kunufaika na kile unachofanya, lakini watu wa karibu watakuchukulia kawaida kabisa.

Hivyo usije ukaacha kufanya kitu kwa sababu unaona watu wa karibu yako hawatakubaliana na wewe. Tambua hawa siyo wateja wazuri wa chochote unachouza. Labda kwa vile walishakuzoea sana hivyo hawawezi kukupa uzito unaostahili.

Usijaribu kupambana na hili, usijaribu kuwabadili kwa namna yoyote ile, wewe fanya kile unachopanga kufanya na walenge wale ambao wanaona thamani yake.

Ukitaka kuthibitisha hili, angalia kitu chochote ambacho umewahi kuuza, watu wako wa karibu watakuwa nacho, lakini hawajanunua kwako. Kama unauza nguo, watu wako wa karibu wataenda kununua nguo kwingine na kama wamenunua kwako labda ni kwa mkopo, ambao mpaka sasa hawajakulipa.

Hivyo ndivyo binadamu tulivyo, wala usiruhusu hilo likuumize.

Rafiki, hivi ndivyo unavyoweza kuandika kuhusu mafanikio hata kama wewe mwenyewe bado hujafanikiwa.

Kitu kimoja ninachoshauri kwenye uandishi ni hiki. FUNGA MDOMO, KAA CHINI NA ANDIKA. Kama kuna msukumo ndani yako wa kuandika, wewe kaa chini na andika, usisikilize sauti yoyote inayokuambia hupaswi kuandika au watu hawatakubali. Wewe kama mwandishi ni chombo cha kufikisha kwa watu maarifa ambayo tayari yapo, tumia vizuri nafasi hiyo. Jiamini wewe mwenyewe na amini kwenye kile unachoandika na utaweza kuwavutia watu sahihi kukuamini pia. Na jua, huwezi kumridhisha kila mtu, hivyo chagua wale wanaoendana na uandishi wako na wahudumie vizuri.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania