Kwenye biashara, unaweza kuwa na bidhaa za kutosha kumuuzia kila aina ya mteja, na usiuze sana.

Unaweza kutumia muda na pesa kutengeneza mikakati mbalimbali kukuza mauzo na zisifanye kazi kwa ukubwa.

Unaweza kuwa na wauzaji wenye uwezo mkubwa wa kushawishi wateja na wasiuze sana.

Sababu inayofanya wasiuze sana au mikakati kutofanya kazi ni kukosekana kwa upendo.

Kama huwezi kuwapenda wateja, ni ngumu kuwauzia. Tafiti nyingi zinaonesha binadamu anajiona yupo sehemu salama pale anapopendwa au kuonyeshwa anapendwa.

Kwa kawaida kupendwa ni asili yetu binadamu. Mtu ukimuonyesha upendo, katika kumkaribisha, kuongea naye, kumsikiliza anajihisi vizuri na yupo sehemu salama kuliko kitu kingine chochote.

Chukulia mfano tu katika maisha yako ya kawaida je, unapenda kuzungukwa na watu wanaofanya ujisikie vizuri au vibaya, watu wanaokupenda au kukuchukia?

Majibu unayopata yaweke katika fikra za mteja wako. Maana yake ni kwamba, kama unasikia faraja unapooneshwa upendo kadhalika na mteja wako yupo hivyo.

Je, ni kwa namna gani biashara inaweza kuonyesha upendo kwa wateja wake?

Moja; Kuwapiga simu
Simu unayopiga hapa isiwe ya kuuza moja kwa moja iwe ya salamu, mengine yatakuja mbele ya mazungumzo.

Mbili; Kutuma barua pepe
Hii ni kwa taasisi au kampuni mbalimbali ukiwatakia utendaji mwema, kuwashirikisha ofa na vitu vingine.

Tatu; kutuma ujumbe mfupi
Hii ndiyo sehemu rahisi wateja kukupa mrejesho. Inaweza kuwa siku za matukio tofauti au kama sehemu ya salamu.

Nne; Kuwatembelea katika biashara zao
Wateja unaoweza kuwafikia, watembelee kuona maendeleo ya biashara zao ili uwape ushauri na mengine mengi.

Tano; Kushiriki nao katika shughuli za kijamii.
Shughuli zinaweza kuwa misiba, harusi au shughuli zingine.

Jinsi ya kumjua mteja uliyemuonyesha upendo;

Moja; Kufanya manunuzi ya pili na zaidi
Hata kama ni wewe, sehemu ulilopata huduma mbovu huwezi kurudi tena. Hivyo, wateja wanafanya manunuzi mengine kwa sababu wamepata huduma nzuri.

Mbili; Kukupatia wateja wa rufaa
Wateja wanapenda marafiki zao kupata huduma nzuri na kitu kilichobora.

Tatu; Kuitangaza biashara yako.
Tupo kwenye zama za sayansi na teknolojia ambapo taarifa nyingi tunazipata mitandaoni. Hivyo, wateja wakifurahia huduma yako, wataitangaza kwenye mitandao ya kijamii.

Usiruhusu wateja wapendwe na washindani wako, onyesha upendo, wajali, wathamini. Watakupenda na kununua katika biashara yako.

Hatua za kuchukua leo; Jifanye tathimini juu ya namna unavyowahudumia wateja wako, wapi unakwama katika kuwaonyesha upendo ili ukuze mauzo yako. Pokea simu au toa mrejesho kwa wateja wako. Kuwa msikilizaji mzuri utaenda kuuza zaidi.

Imeandaliwa na Lackius Robert

Mkufunzi na Mwandishi

0767702659 |mkufunzi@mauzo.tz