Rafiki yangu mpendwa,
Nimekuwa naamini na kusema hili mara kwa mara na nilirudie tena hapa, kukosa mtaji siyo sababu ya kushindwa kuingia kwenye biashara. Ni kisingizio tu.

Sasa visingizio vyote huwa ni vya uongo, kwa sababu vinaficha kile ambacho mtu hataki kukikabili.

Wengi wanaotumia kisingizio cha mtaji, hawapo tayari kuukabili ukweli kwamba ni wavivu, wazembe, wasio tayari kujitoa na wanaopenda mazoea. Ni vigumu sana mtu kukiri una tabia hizo, hivyo kisingizio cha mtaji au muda kinakuwa rahisi.

Kwa zama tunazoishi sasa, hakuna kinachoweza kumzuia mtu aliyejitoa kweli kuingia kwenye biashara. Siyo wazo, siyo mtaji na wala siyo muda.
Kinachomzuia mtu hakitoki nje, bali kipo ndani yake.
Na yule ambaye hana kizuizi cha ndani, anaweza kuyafanya makubwa mno.

Chukua mfano wa biashara ya genge la mahitaji muhimu ya kila siku kwenye familia.
Ni biashara yenye uhitaji, kwa sababu watu kila siku wanakula.
Ni biashara unayoweza kuanza kwa mtaji kidogo.
Ni biashara ambayo huhitaji kuwa na eneo la gharama kubwa kuifanyia.
Na ni biashara ambayo haina vitu vingi, hivyo unaweza kuisimamia vizuri.

Hii ni biashara ambayo mtu ambaye hana shughuli nyingine ya kufanya anaweza kuianzisha, akaiendesha vizuri na ikawa sehemu ya yeye kupiga hatua na kuelekea kwenye biashara kubwa zaidi.

Unapochagua kufanya biashara kama hii, unapaswa kuifanya kwa tofauti, ili ikue na kuweza kuzalisha biashara nyingine kubwa zaidi.

Huenda unawajua wauza genge ambao miaka yote unawaona wakiwa pale pale. Siyo kwamba biashara hailipi, ila wanaifanya kwa viwango vya chini.

Kwenye makala hii unakwenda kujifunza jinsi ya kuifanya biashara ya genge kwa viwango vya juu sana na ikawa na manufaa makubwa kwako.

Kabla hatujaingia kwenye ushauri, tusome aliyotuandikia msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

“Nahitaji kufungua genge la matunda na mboga mboga napenda kuelimishwa namna ya kuboresha iliniweze kukuza biashara yangu na wateja wavutiwe na huduma yangu.” – Hussein B. M.

I. MAONO MAKUBWA.
Anza kidogo lakini fikiri kwa ukubwa. Japo unafanya biashara ya genge, kwenye fikra zako usione genge, bali ona biashara kubwa kabisa.
Ona ukiwa na maduka mengi ya kuuza mahitaji hayo ya msingi na ona ukifanya kwa kiwango kikubwa zaidi.
Ni maono makubwa unayokuwa nayo ndiyo yanakusukuma kupiga hatua kubwa pia.
Tunapata kile tunachoona, hivyo kuwa na maono makubwa na jisukume kuyafikia.

II. BIDHAA BORA.
Kwenye biashara ya genge wateja wanaangalia vitu vikuu viwili, bidhaa bora na kwa bei nafuu. Pambana kuwapatia wateja vitu hivyo viwili na watakuwa wako kwa muda mrefu.
Chagua bidhaa zilizo bora kabisa ndiyo uweke kwenye biashara yako.
Jua maeneo unayoweza kupata bidhaa hiyo bora kwa bei nafuu ili pia uweze kuwauzia wateja wako kwa bei nzuri.
Jiwekee viwango vya ubora wa bidhaa utakazouza ili wateja waweze kujenga imani kwako na kwa biashara yako.

III. ENEO ZURI.
Biashara yako inapaswa kuwa eneo ambalo ni rahisi kuwafikia wateja wako na hata wateja kuifikia pia.
Kwa kuwa unachouza ni mahitaji muhimu ya maisha ya kila siku, biashara itafanya vizuri pale inapokuwa eneo lenye watu wengi.
Lakini pia mazingira ya eneo lako la biashara yanapaswa kuwa safi na mazuri, yamfanye mteja aiamini na kuithamini biashara yako.
Wengi wanaofanya biashara ya genge hawaweki maeneo yao ya biashara kwenye mwonekano mzuri, ukifanyia kazi hilo unajitofautisha kabisa na wengine.

IV. HUDUMA BORA KWA WATEJA.
Wahudumie vizuri saba wateja wako ili waweze kurudi tena na tena. Wasikilize kwa umakini na wajali pia. Jua mahitaji yao na uwatimizie.
Usiuze tu na kuishia hapo, jenga mahusiano mazuri na wateja wako na hayo yataiwezesha biashara kukua zaidi.
Pale wateja wanapopata huduma nzuri, wanaendelea kuja na wanawaleta wengine pia.

V. KUWEKA MAFUNGU.
Unayajua mahitaji ya wateja wako, unaweza kutengeneza mafungu ya vitu vinavyonunuliwa kwa pamoja na kisha kumshawishi mteja anunue kama fungu badala ya kununua kimoja kimoja.
Kumsukuma kuchukua hatua, hakikisha bei ya fungu inakuwa na unafuu kuliko mteja akinunua kimoja kimoja.
Njia hii itakuwezesha kuuza zaidi kwa wateja ambao tayari unao, ambao ni wateja wazuri tayari.

VI. KUWAFIKIA WATEJA.
Usisubiri tu wateja waje, badala yake watuate kule walipo. Watu sasa wametingwa na mambo mengi wanaweza kusahau kabisa hata uwepo wako.
Hivyo watembelee wateja wako maeneo walipo na kuwashawishi kuja kununua.
Hapa pia unaweza kutoa huduma ya mteja kuagiza na kupelekewa bidhaa zake.
Na kama umeziweka bidhaa kwa mafungu na bidhaa zako ni bora, mteja anaagiza na kupelekewa, akijua anapata anachotaka na ambacho ni bora pia.

VII. KUWASILIANA NA WATEJA.
Omba mawasiliano ya wateja wako na wasiliana nao mara kwa mara.
Unajua wateja wa genge wanapanga mahitaji yao ya siku asubuhi. Unaweza kuwatumia ujumbe asubuhi kuwasalimia na kuwaomba oda pia. Mteja anapopata ujumbe wako, anakufikiria kwa muda mrefu na hilo linamshawishi kuja kununua kwako.
Tumia kila sababu na ushawishi kupata mawasiliano ya wateja wako na wasiliana nao kwa njia ambayo siyo ya usumbufu kwako.

VIII. KUWEKA AKIBA.
Kwa lengo lako la kufika kwenye mafanikio makubwa kibiashara, unapaswa kuweka akiba kwenye kila faida unayoingiza kwenye biashara yako.
Wakati biashara inafanya vizuri, usibweteke na kuona mambo yataenda hivyo wakati wote.
Weka akiba ambayo itakusaidia wakati biashara haiendi vizuri.
Akiba hiyo ndiyo itakusaidia kwenye ukuaji wa biashara yako.

IX. KUKUZA BIASHARA.
Kwa kuwa una maono makubwa ya biashara yako, kila wakati angalia fursa za ukuaji zaidi.
Kila wakati piga hatua kuikuza biashara yako zaidi.

X. KUJIFUNZA KILA SIKU.
Kujifunza kila siku ni hitaji muhimu la ukuaji wa biashara yako.
Kila siku hakikisha unajifunza kitu kwenye kuikuza biashara yako.
Biashara inahitaji ubobezi maeneo mbalimbali kama masoko, mauzo, fedha, ushawishi na uongozi.
Soma vitabu mbalimbali vya biashara na yake unayojifunza yafanyie kazi.
Vitabu viwili muhimu sana unavyopaswa kuvisoma ni;
1. The psychology of selling cha Brian Tracy.
2. Elimu ya msingi ya biashara cha Kocha Dr Makirita Amani.
Kupata vitabu hivyo tuwasiliane kwa namba 0717 396 253.

Fanyia kazi haya uliyojifunza kwenye hii makala ili uweze kuanzisha na kukuza biashara yako na kufika kwenye mafanikio makubwa.
Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.