Rafiki yangu mpendwa,

Huwezi kufikia utajiri mkubwa na mafanikio kwenye maisha bila ya kutoa kafara.

Na kinachowazuia wengi kufanikiwa ni kutokuwa tayari kutoa kafara.

Wengi wanapenda kuwa na maisha yanayowapendeza, hawataki kuumia wala kukosa chochote.

Maisha ni kupata na kukosa, kupoteza kitu fulani ili kupata kitu kingine, au kuliwa eneo fulani ili uweze kula eneo jingine. Hii ni dhana inayoitwa tradeoff, huwezi kupata vyote unavyotaka kwa wakati mmoja, lazima uwe tayari kupoteza kitu fulani unachopenda ili kupata kingine unachopenda zaidi.

things-to-sacrifice-1.jpg

Watu wengi wanaposikia kuhusu kutoa kafara ili kupata utajiri, akili zao zinaenda kwenye kuua watu wao wa karibu kwa imani za kishirikina ili kupata utajiri.

Hiyo siyo maana halisi ya kutoa kafara, hapa utakwenda kujifunza kafara unayopaswa kutoa ambayo haihusishi kuua watu wala kuharibu maisha ya wengine, bali ni kafara ya kukujengea wewe nidhamu itakayokusaidia kufanikiwa sana.

Kwenye kitabu cha KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI, nimekushirikisha sababu 25 zinazokuzuia kufikia utajiri. Na sababu ya 23 inasema hivi; HUJATOA KAFARA.

Wengi wakisikia kafara na utajiri masikio yanawasimama kweli kweli, wanajua hapa ndipo penye ile siri ambayo matajiri wanaijua lakini masikini hawaijui. Hivyo kutegemea kuambiwa wawaue watu wao wa karibu ili kupata utajiri na mafanikio.

Kafara ya kweli na itakayokufikisha kwenye mafanikio makubwa haimhusishi mtu yeyote, bali inakuhusisha wewe mwenyewe.

Iko hivi rafiki, kuna rasilimali mbili muhimu sana ambazo unazo kwa uhaba mkubwa kwenye maisha ambazo ni nguvu na muda.

Muda ulionao ni masaa 24 tu kwa siku, huku simu ulizonazo ni 365 tu kwa mwaka, na miaka yako ina ukomo hapa duniani.

Kadhalika unapoianza siku yako unakuwa na nguvu nyingi, lakini unavyofanya mambo mbalimbali, nguvu hiyo inapungua na hivyo kushindwa kufanya kila unachotaka kufanya.

Sasa kutokana na ukomo wa rasilimali hizi mbili, jinsi unavyozitumia ndiyo kunaamua mafanikio ambayo utayapata kwenye maisha yako.

Kwa maneno mengine, jinsi unavyopangilia vipaumbele kwenye matumizi yako ya muda na nguvu, itaamua kama utafanikiwa au la.

Kwenye maisha yako, kuna vitu ambavyo unapenda sana kuvifanya, vinachukua muda wako mwingi na sehemu kubwa ya nguvu zako, lakini havina mchango wowote kwenye mafanikio yako.

Hivi ndiyo vitu ambavyo unapaswa kuviondoa mara moja kwenye maisha yako.

Kwa kuwa unapenda sana kuvifanya, kuondokana nako vitakuumiza sana, na hapo ndipo unapopaswa kuwa tayari kutoa kafara ili ufanikiwe.

Kafara tatu unazopasa kutoa kwenye maisha yako.

Kuna aina tatu za kafara unazopaswa kutoa kama unataka kufikia utajiri na mafanikio makubwa kwenye maisha yao.

Moja; vitu unavyofanya.

Kama tulivyoona hapo juu, kuna vitu vingi unavyopenda kufanya lakini havina mchango wowote kwenye mafanikio unayotaka kufikia kwenye maisha.

Hivi ni vitu ambavyo unapaswa kuacha kuvifanya mara moja kama unataka utajiri na mafanikio.

Jinsi ya kujua vitu hivyo vya kuacha fanya zoezi hili;

Chukua karatasi na kalamu, kisha gawa karatasi hiyo kwenye pande mbili. Upande wa kwanza orodhesha vitu vyote ulivyofanya ndani ya wiki moja iliyopita. Kila kitu ulichofanya orodhesha, usiache hata kimoja. Uliingia kwenye mitandao ya kijamii, andika, ulibishana na mtu andika, orodhesha vyote kabisa.

Upande wa pili orodhesha malengo unayofanyia kazi kwenye maisha yako, kule unakotaka kufika au kile unachotaka kupata.

Baada ya kuwa na orodha hizi mbili, pitia upande wa kwanza kwenye kila ulichofanya kisha jiulize kinakusaidia kufikia kipi kilichopo kwenye upande wa pili, yaani malengo yako. Kama kina mchango weka alama ya vema mbele yake. Kama hakina mchango weka alama ya mkasi mbele yako.

Ukishakamilisha kupitia orodha yote ya kwanza, yale yote uliyoyawekea alama ya mkasi usiyafanye tena kwenye maisha yako, hayo ndiyo unayoyatoa kafara. Hata kama unayapenda kiasi gani, hayana mchango kwako, acha kuyafanya mara moja. Fanya yale uliyoyawekea alama ya vema tu.

Mbili; matumizi yako ya fedha.

Huwa unatumia fedha kwa mambo mengi, lakini mengi kati ya hayo siyo muhimu. Hivyo ni kama unachagua kupoteza fedha zako, na hicho kinakuwa kikwazo kwako kufikia utajiri na mafanikio makubwa.

Kanuni rahisi ya kufikia utajiri kama tunavyoshauriwa na bilionea Charlie Munger ni matumizi yako kuwa madogo kuliko kipato chako, kuweka akiba na kisha kuwekeza akiba hiyo ili izalishe zaidi.

Ili matumizi yako yawe madogo kuliko kipato chako, lazima utoe kafara, lazima ujinyime vitu vizuri ambavyo umezoea kupata sasa.

Na hapa kuna zoezi jingine muhimu kwako kufanya.

Orodhesha manunuzi yote ambayo umefanya ndani ya mwezi mmoja uliopita, kila senti uliyotoa kulipia kitu chochote kile iandike. Baada ya kuorodhesha kila ulichonunua, pitia kimoja kimoja na jiulize je ni kitu muhimu kabisa kwenye maisha yako? Je kisingeweza kusubiri? Je maisha yako yasingeweza kwenda kama kisingekuwepo?

Kwa kile ambacho maisha yangeweza kwenda bila ya kuwa nacho, kiwekee alama ya mkasi na usinunue tena kitu cha aina hiyo. Hata kama unakipenda kiasi gani, hata kama kila mtu ananunua, kama siyo muhimu kabisa kwako, usinunue. Ndiyo itakuumiza, ndiyo itakufanya uonekane wa ajabu, lakini kumbuka ni kafara unatoa, ili ufanikiwe zaidi baadaye.

Tatu; watu unaojihusisha nao.

Mafanikio yako ni wastani wa mafanikio ya watu watano unaotumia nao muda wako mwingi. Utajiri utakaoweza kufikia kwenye maisha ni wastani wa utajiri wa watu watano unaotumia nao muda wako mwingi. Huwezi kamwe kuvuka nguvu ya watu watano wanaokuzunguka. Hivyo unahitaji kuwatoa baadhi ya watu kafara.

Hapa unahitaji kufanya zoezi hili, orodhesha watu wote ambao huwa unatumia muda wako mwingi kuwa nao. Wale ambao unafanya nao kazi au biashara, na wale ambao mnakuwa pamoja mara nyingi.

Anza kupitia maisha ya mtu mmoja mmoja, angalia kiwango cha mafanikio ambacho wanacho, kisha angalia malengo na mipango waliyonayo. Angalia ni watu wa kujituma kiasi gani kwenye maisha yao, kama ni watu wenye kiu ta mafanikio makubwa au wameridhika pale walipo sasa.

Waondoe kwenye maisha yako wale wote ambao hawana kiu ya mafanikio makubwa, wakatisha tamaa na walioridhika na pale walipofika. Usiendelee tena kutumia muda wako kuwa nao, huna haja ya kugombana nao, bali acha kuwapa muda wako. Acha kuwaambia mambo yako, maana watakukatisha tamaa. Kwa kifupi wafute kabisa kwenye maisha yako.

Hili linaweza kukuumiza, maana wengi watakuwa ni marafiki ambao mmejuana tangu utotoni, wengine watakuwa ni ndugu wa karibu ambao mmekuwa pamoja kwa muda mrefu. Utaona huwezi kuachana nao, hawatajisikia vizuri. Lakini kumbuka hapa unatoa kafara, haitakufurahisha hata kidogo, na ili upate unachotaka, lazima kuna vitu utapoteza.

Hatua ya kuchukua.

Umejifunza hapa umuhimu wa kutoa kafara, ambapo ni moja ya sababu zinazokuzuia kufikia utajiri na mafanikio makubwa. Kuna sababu nyingine 24 zinazokuzuia kufikia utajiri kwenye maisha yako. Unapaswa kujua sababu hizo na hatua za kuchukua kwa kila sababu ili uweze kuondoka kwenye umasikini.

Kwenye kitabu cha KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI, unakwenda kujifunza kwa kina sababu zote 25 na hatua za kuchukua kwa kila sababu. Hivyo jipatie na kusoma kitabu hiki leo ili uweze kutoka pale ulipokwama sasa.

Jinsi ya kupata kitabu cha KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI.

Kitabu hiki ni nakala tete (softcopy) na kinatumwa kwa email. Bei ya kitabu hiki kwa kawaida ni tsh elfu 5 (5,000/=), lakini kama utakilipia leo, utakipata kwa bei ya zawadi ambayo ni tsh elfu 3 (3,000/=)

Kupata kitabu hiki, tuma tsh elfu 3 (3,000/=) kwenda namba 0755 953 887 au 0717 396 253 kisha tuma ujumbe wenye email yako na maelezo umelipia kitabu cha KWA NINI SIYO TAJIRI na utatumiwa kitabu hicho.

Pata leo kitabu cha KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI uweze kujua sababu 25 zinazokuweka kwenye umasikini na jinsi ya kuzivuka.

Zawadi ya vitabu nane vya mafanikio.

Rafiki, nikukumbushe pia kwamba zawadi ya vitabu nane nilivyotoa inaendelea na karibu itafika ukingoni.

Kwenye zawadi hii, unapata vitabu nane nilivyoandika, katika mfumo wa nakala tete kwa kulipa nusu ya bei pale unapochukua vitabu vyote.

Vitabu hivyo na bei zake za zawadi ni kama ifuatavyo;

  1. KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI, bei ya zawadi elfu 3.
  2. JINSI YA KUTENGENEZA KIPATO MTANDAONI KWA KUTUMIA BLOG, bei ya zawadi elfu 7.
  3. JINSI YA KUNUFAIKA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA, bei ya zawadi elfu 3.
  4. KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO, bei ya zawadi elfu 7.
  5. BIASHARA NDANI YA AJIRA, TOLEO LA KWANZA, bei ya zawadi elfu 7.
  6. MIMI NI MSHINDI, AHADI YANGU NA NAFSI YANGU, bei ya zawadi elfu 7.
  7. IJUE BIASHARA YA MTANDAO (NETWORK MARKETING), bei ya zawadi elfu 3.
  8. PATA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU, bei ya zawadi elfu 3.

Ukichukua vitabu vyote nane kwa pamoja, unalipa tsh elfu 30 badala ya elfu 40 kama utachukua kimoja kimoja kwa bei ya zawadi.

Karibu sana upate zawadi hii, tuma fedha kwenda namba 0755 953 887 au 0717 396 253 kisha tuma ujumbe wenye email yako na jina la kitabu au vitabu ulivyolipia kisha utatumiwa kwenye email yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania