Kumekuwa na misemo mingi mitaani ambayo kwa namna moja au nyingine inaathiri au inaua kabisa ndoto za watu wengi. Watu wamekuwa wakiiga vitu katika jamii bila hata kuuliza kwa nini mtu huyu anafanya hivi. Kuiga mitindo ya kimaisha nalo limekuwa ni jambo ambalo linawaathiri watu wengi sana. Kuishi nje ya malengo uliyojiwekea na kukata tamaa ya maisha limekuwa tatizo sana. Kuishi maisha ambayo hayana furaha, upendo, amani ni tatizo miongoni mwa watu wengi.
Watu wanaamini ili uweze kuishi maisha ya furaha ni lazima uwe na kiasi kikubwa cha fedha, usidanganyike ili uwe na furaha ya kweli ya kutoka moyoni anza kuwa na shukrani kwa kile ambacho unacho sasa na ishi maisha yako halisi usiige maisha ya mtu. Na siku zote furaha ya kweli hainunuliwi bali inatoka moyoni .Tafuta furaha ya kweli na ya kudumu mara nyingi furaha za muda mfupi huwa zina madhara sana na zina gharama sana, mfano mtu mwingine ili apate furaha ya muda mfupi lazima atumie kilevi na siku zote hakuna kilevi cha bure na ambacho hakina athari hasi kwa afya yako.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA.

 
Usikate tamaa katika maisha kukata tamaa ni dhambi na usiogope changamoto unazokumbana nazo bali jitahidi kukabiliana nazo. Changamoto ni sehemu ya maisha ya mwanadamu hakuna maisha yasiyokuwa na changamoto. Kila binadamu hapa duniani ana matatizo yake hakuna binadamu ambaye hana matatizo. Hivyo basi, usifananishe matatizo yako na mtu mwingine ndio maana Waswahili wanasema nyumba usiyolala hujui hila yake.
Kila mtu anahitaji kuishi maisha ya mafanikio ili kuishi katika namna ambayo inaleta ukamilifu. Mafanikio katika maisha ni vile unavyotaka kuwa na unaweza kuwa vile kama unavyotaka kuwa kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Binadamu hawezi kuishi sawa kimwili bila ya chakula kizuri, mavazi ambayo yanamfanya mtu ajihisi huru na malazi pia.
Mtu hawezi kuishi kikamilifu kiakili bila ya vitabu na muda wa kuvisoma vitabu hivyo. Maarifa yanapatikana kwa kusoma vitabu ukiwa ni mtu wa kusoma unaokoa gharama nyingi sana. Pia ili kuishi kiroho kikamilifu binadamu anatakiwa kua na upendo. Upendo una nguvu na upendo huvumilia yote mpende mwenzako kama unavyojipenda wewe.
Sasa tuangalie kiini cha makala yetu ya leo. Zifuatazo ni kauli/misemo ambayo inaua ndoto yako
1. Kila Kukicha Afadhali Ya Jana;
Huu msemo unatumika sana kwa watu. Watu waliokata tamaa, watu wenye mtazamo hasi katika maisha. Kuna baadhi ya daladala wameandika usemi huu ambao ni msemo unaokataisha tamaa na ni msemo wa watu ambao hawajui maana ya wao kuwepo hapa duniani. Kwa mtu anayetengeneza maana kwake huu ni msemo hasi ambao haumpi hamasa yoyote katika maisha.
Watu wanaopenda mafanikio wanaamini kuwa unatakiwa kua bora kila siku zaidi ya jana yaani kila siku upige hatua mbele zaidi. Kwa mtazamo huu wa mtu kuamka na kuanza kusema haya maisha kila kukicha afadhali ya jana ni ngumu sana mtu kufikia mafanikio makubwa kwani anakua amefunga kufuli akili yake ya kufikiri kirefu zaidi ili aweze kua bora. Mtu anayependa maendeleo anaona kila siku ni siku mpya katika maisha yake ni sawa na ukurasa mpya wa maisha yake ambapo inampasa aache alama katika ukurasa wake mpya.
SOMA; Kama Una Tabia Hii Moja Una Uhakika wa Zaidi ya 90% Wa Kufanikiwa Kwenye Chochote Unachofanya.
Kwa kweli kama hujajitambua ,hujajua nini dhumuni lako la wewe kua hapa duniani basi nakusihi amka sasa. Kuna watu wanatafuta jinsi gani anaweza kupoteza muda, utasikia ngoja niangalie movie nipoteze poteze muda, lakini kuna watu wanatamani kupata hayo masaa unayotumia kupoteza muda katika kuangalia movie lakini kila binadamu ana utajiri wa rasilimali muda sawa siyo masikini wala tajiri wote tuna wakati sawa. Usichezee wakati kwani maisha ni muda tengeneza maana kila siku katika maisha yako na achana na misemo hasi inayoua ndoto yako.
2. Bado Nipo Nipo Kwanza;
Hii kauli ni moja ya misemo ambayo inaua ndoto za watu wengi hususani vijana. Bado upo upo kwanza unasubiri nini? Unasubiri upewe ruhusa? Msemo huu ni msemo ambao unapoteza wakati wako. Unataka kuanza kujitegemea, kuanza biashara, kuwa na familia au bado upo upo kwanza unapoteza wakati. Ukisema unajipanga unasubiri ukamilifu hautopata ukamilifu bali wewe anza na uzoefu unapatikana ndani ya kazi na siyo nje ya kazi. Vijana wengi wanaupenda sana huu msemo wa bado nipo nipo kwanza. Mwanafalsafa Seneca alisema maisha ni marefu kama ukitumia muda wako vizuri hapa duniani. Hivyo basi maisha ni muda. Umri unakwenda mbele na haurudi nyuma jinsi unavyoendelea kusubiri kuanza jambo lolote katika maisha yako unajitengenezea mazingira magumu sana hapo mbeleni ni bora ukubali kulipa gharama sasa kuliko kulipa baadaye tena kwa riba kubwa. Usikimbie majukumu, majukumu ni kama changamoto hayakimbiwi bali unakabiliana nayo ukikimbia ndio unaongeza matatizo.
SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Vijana Wanaokwenda Kuanza Maisha Ya Kujitegemea Kwa Mwaka Huu 2016.
3. Fedha Ni Shetani;
Kwanza kabisa fedha siyo shetani fedha ina hitaji nidhamu ya hali ya juu ukisoma nidhamu ya fedha ndio utasema fedha ni shetani. Ushetani uko katika matumizi yako wala usiilaumu fedha bure. Fedha ni chombo ambacho kila mtu anapaswa kuwa nacho ni chombo muhimu kwa kila mtu anayeishi hapa duniani ili kukidhi mahitaji yake. Kwanini sasa useme fedha ni shetani? Kama ulikuwa hujui kuwa fedha zina tabia jua leo katika kitabu cha zaburi katika biblia kinaelezea tabia za fedha nazo ni hufuata mbunifu, hutoroka mvivu, hutembea huku na kule, ina macho na miguu, hupenda mtu msafi, huchukia bahili, hupenda mwerevu, hukomesha maneno, jibu la mambo yote, zina vinywa lakini havisemi, zina macho lakini hazioni na zina masikio lakini hazisikii. Kwa hiyo umeona fedha siyo shetani kama ilivyozoeleka kwa watu wenye mtazamo hasi.
4. Tumia Pesa Ikuzoee/Ukipata Tumia Ukikosa Jutia;
Hata uwe mtafutaji mzuri kiasi gani kama wewe ni mtu ukipata tumia ukikosa jutia utaishia kuwa masikini tu. Mfano ukipata kipato chako unatumia chote halafu ukikosa unajutia hahaha! Hii ni kauli ya maarufu ya watu wanaojiita wala bata au timu amsha popo wakikesha kwenye kumbi za starehe wakitumia pesa ili ziwazoee. Huwezi kuwa na uhuru wa kifedha kama wewe una tabia hii unatakiwa kuweka akiba, kuishi chini ya kipato chako, kuwekeza, kupunguza starehe zisizo za kilazima na kuwa na nidhamu ya pesa ndio njia nzuri ya wewe unatakiwa kua nayo katika matumizi ya pesa. Yaepuke sana makundi haya ya starehe ya tumia ukikosa jutia kama ni rafiki yako mkimbie anakupeleka shimoni kabisa ishi maisha yako.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Pesa Zako Na Kuwa Tajiri.
5. Aliyekupa Wewe Ndiye Aliyeninyima Mimi;
Hii si kauli ya mtafutaji kila mtu ana uhuru wa kufika popote katika mafanikio bila ya kupewa kikomo chochote ni wewe tu kujituma kwako. Ukijituma kufanya kazi halali bila sababu kwa kuweka juhudi na maarifa utakua kama vile unavyotaka. Ukimuona mwenzako kafanikiwa jifunze kutoka kwake kamwe usijifunze kupitia mtu aliyefeli jifunze kwa aliyefanikiwa ndio njia nzuri huwezi kupotea kamwe. Tabia ya kumchukia mtu aliyefanikiwa na kumwambia eti aliyekupa wewe ndiye aliyeninyima mimi haifai kwa watu wenye mtazamo chanya mambo ya ajabu waachie watu wenye mtazamo hasi wasiopenda maendeleo ya watu.
Kwa hiyo, watu wanatakiwa kuacha kuzitumia kauli hizi na kubadili mtazamo wa fikra, mambo ya kuamini mafanikio ni kwa watu waliosoma tu, au watu wa ukoo Fulani au kabila Fulani ndio wana haki ya kufanikiwa siyo kweli. Hakuna mafanikio ya haraka, usidharau biashara ndogo na usijidharau wewe mwenyewe bali jiamini katika kuwa mshindi na siyo mshindwa.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com