Sikiliza hapa;
Rafiki yangu mpendwa,
Najua hili ninalokuambia hapa litakuchanganya, lakini ndiyo ukweli wenyewe, inapokuja kwenye kupata mafanikio makubwa. Kueleweka na kila mtu, au hata watu wengi ni dalili mbaya kwenye safari yako ya mafanikio.
Hilo linakuchanganya kwa sababu ya asili yetu sisi binadamu kupenda kukubalika na kila mtu. Na hilo kutufanya tufanye yale ambayo wengine watatusifia na kutukubali.
Sasa unafikiri ni vitu gani ambavyo ukivifanya wengine watakusifia na kukukubali? Iko dhahiri kwamba ni vitu ambavyo watu hao wanavielewa.
Je unadhani unaweza kujenga mafanikio makubwa kwa kufanya vitu ambavyo watu wengi wanavielewa?
Jibu ni hapana, hicho kitu hakiwezekani kabisa.
Kama kitu kinaeleweka na kila mtu, maana yake ni kitu cha kawaida sana, kisicho na hatari wala madhara yoyote.
Kama ulikuwa hujui, huwezi kujenga mafanikio makubwa kwa kufanya vitu vya kawaida. Angalia historia za watu wote waliowahi kufanya makubwa hapa duniani, hawakufanya mambo ya kawaida.
Walifanya mambo yaliyoonekana ya ajabu, ya hatari na yasiyowezekana. Walikatazwa na kuonywa na watu waliowazunguka.
Wapo walioenda mbali zaidi na kudhani watu hao walikuwa wamechanganyikiwa na hivyo kuwapeleka kwenye hospitali za magonjwa ya akili.
Lakini mwisho wa siku, watu hao ndiyo walioibuka washindi, kwa sababu waliamini na kufanya yale ambayo hayakueleweka na wengine.
Najua wewe umeshapitia hali kama hizo mara nyingi sana. Umekuwa na mawazo ya biashara au ya kibunifu, lakini watu wako wa karibu wakakuambia mawazo hayo siyo sahihi.
Ninachoamini bila shaka yoyote ni kwamba, wewe rafiki yangu, ungekuwa umepiga hatua kubwa zaidi ya hapo ulipo sasa, kama usingewasikiliza wale waliokukwamisha na kukukatisha tamaa.
Uliwasikiliza kwa sababu hukuwa na mtu mwingine unayemwamini wa kumsikiliza, ambaye angeweza kukuambia mawazo yako ni sahihi na hao waisokuelewa ndiyo wenye matatizo.
Sasa nipo hapa rafiki yako, ninayekupenda na kukujali sana. Na ninakuambia kitu kimoja, kile unachofikiria, kinawezekana kabisa kwako.
Ndiyo, ndoto zote kubwa ulizonazo, japo zinaonekana za ajabu kwa wengine, ndizo unazopaswa kuzipambania ili uache alama ya tofauti hapa duniani.
Na huo ndiyo wajibu wangu kama rafiki yako, kuhakikisha unajiamini na kupambania ndoto kubwa ulizonazo, bila kukubali kukwamishwa na yeyote.
Rafiki, kama umefanya zoezi la kujibu maswali matatu niliyokuelekeza kwenye somo hilo hapo chini, basi huo ndiyo unapaswa kuwa mwongozo wako.
SOMA; Jipe Majibu Ya Maswali Haya Matatu Kama Unataka Mafanikio Makubwa.
Usikubali kuyumbishwa na mtu yeyote anayekuambia kwamba unachowaza wewe siyo sahihi. Wewe jiamini na kujua ni sahihi kwako. Na wengine wana haki ya kuona siyo sahihi, kwa sababu hakijatoka ndani yao.
Nikupe tahadhari moja rafiki yangu, punguza ‘kamdomo’. Iko hivi, unapopata mawazo ya tofauti na unayoamini yataleta mapinduzi makubwa, unakimbilia kuwaambia wengine mawazo hayo. Kwa kuamini watayaelewa na kuyafurahia kama wewe.
Lakini hivyo sivyo mambo yanavyoenda. Badala ya watu kufurahia kama wewe, wanageuka kuwa kikwazo kwako. Shauku kubwa uliyokuwa nayo inayeyuka kama barafu iliyokutana na jua. Na huo unakuwa ndiyo mwisho wa mawazo na ndoto kubwa ulizokuwa nazo.
Kuondokana na hilo, unapaswa kuacha kumwambia kila mtu mawazo yako ya tofauti. Ukishawajua watu hawakuelewi, acha kuwashirikisha mambo yako makubwa. Kwa njia hiyo utajiepusha na hali ya kukatishwa tamaa na wasiokuelewa.
Rafiki, unachohitaji ni kujitambua na kujielewa wewe mwenyewe. Kama mawazo uliyonayo yametoka ndani yako, yanawezekana kabisa kwako. Wapuuze kabisa wale wasiokuelewa, kwa sababu hawawezi kuwa na mchango wowote kwako.
Kwenye Barua Ya Kocha hapo chini, nimeeleza kwa kina kwa nini unapaswa kufurahia pale wengine wanapokuwa hawakuelewi. Isome na utoke na nguvu ya kupambania ndoto zako za tofauti.
Soma; #BZK003; Furahia Pale Ambapo Watu Wengine Hawakuelewi
Rafiki, wewe ndiyo toleo pekee la wewe ambalo limewahi kuwepo hapa duniani. Haiwezekani toleo la kipekee kama wewe kueleweka na wengine. Jiamini na pambania ndoto zako. Inawezekana kabisa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
