Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Kabla hujaona nakuchanganya kwa sentensi inayokinzana yenyewe, yaani uvumilivu usio na subira, tuwaangalie wahenga, waliosema; ‘kawia ufike’, lakini hao hao wakasema; ‘chelewa chelewa utakuta mwana si wako.’

Ninachotaka kukuonyesha hapo rafiki yangu ni kwamba, kila jambo linapaswa kuchukuliwa kwa muktadha wake. Tunapaswa kutumia kila kitu kama rasilimali kwetu kupata mafanikio makubwa tunayoyataka.

Na kwenye barua hii tunaenda kuangalia dhana hizo mbili, ambazo zinaweza kuonekana kupingana, lakini zote zinamaanisha kitu kimoja na ni muhimu sana kwenye safari ya mafanikio makubwa.

Dhana ya uvumulivu usio na subira ni kitu ambacho kinapaswa kueleweka vizuri na kufanyiwa kazi kama njia ya sisi kuchukua hatua sahihi na kupata matokeo makubwa tunayoyataka.

Tatizo Aliloliona Bill Gates.

Bill Gates, bilionea na mwanzilishi wa kampuni ya Microsoft amewahi kunukuliwa akisema; ‘Watu wengi hukadiria kwa ukubwa wanachoweza kufanya ndani ya mwaka mmoja na kukadiria kwa udogo wanachoweza kufanya ndani ya miaka kumi.’

Alichomaanisha ni watu huwa wanafikiria wanaweza kufanya makubwa sana ndani ya muda mfupi, yaani mwaka mmoja, kuliko ilivyo uhalisia. Na hili huwa linaonekana wazi kwa jinsi watu wanavyotarajia mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi. Na wanapoyakosa, wanaona kama wameshindwa.

Na kwa upande wa pili, watu huwa hawafikirii matokeo wanayoweza kupata ndani ya muda mrefu wa miaka 10. Hivyo wanajikuta wakienda tu bila mpango kwenye huo muda mrefu na matokeo yake ni kupoteza fursa ya kupata matokeo makubwa kwenye hicho kipindi.

Hili ni tatizo ambalo lipo kwa watu wengi, na linachangia kwa wengi kushindwa kupata mafanikio makubwa ambayo yapo ndani ya uwezo wao. Kwa muda mrefu, kila mtu anaweza kupata mafanikio makubwa kadiri anavyotaka. Lakini wengi hawaweki mipango ya muda mrefu. Badala yake wanataka mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi. Wanapoyakosa, wanakimbilia kuanza kitu kingine.

Watu wengi wamekuwa wanajikuta wanapoteza maisha yao kwa kuhangaika na mambo mengi ya muda mfupi na ambayo hayatokei. Wakati wangechagua jambo moja la muda mrefu, na kulifanyia kazi kwa uhakika, wangepata mafanikio makubwa.

Alichosema Bill Gates ni njia nyingine ya kuwa na uvumilivu wa muda mrefu kwa sababu muda huo unaleta matokeo ya uhakika, lakini kukosa subira kwenye utekelezaji wa yale ambayo mtu anayapanga ili kuweza kupata matokeo.

Kwenye barua hii tunaenda kuangalia jinsi tunavyoweza kutumia hali zote mbili, yaani uvumilivu na kukosa subira kwenye safari yetu ya mafanikio makubwa. Utajua ni eneo gani ambalo unahitaji uvumilivu kwenye hii safari, ili uweze kuwa nao na kupata matokeo makubwa. Na muhimu zaidi, unapaswa kujua wapi ambapo hupaswi kuwa na subira, ili usije ukamkosa mwana ambaye ni mafanikio unayoyataka.

1. Uvumilivu Ni Muhimu Kwenye Kuyafikia Mafanikio Makubwa.

Huwa kuna kauli sahihi sana kwenye hili, lakini ambayo watu wengi wanaijua lakini hawaitumii kwa usahihi kwenye safari ya mafanikio. Kauli hiyo inasema; mipango siyo matumizi. Unachopanga siyo kinachotokea, hasa kwa namna unavyofikiria.

Hata upange kwa namna gani, kinachokuja kutokea ni tofauti kabisa na ulivyotarajia. Lakini hilo halimaanishi kwamba umeshindwa, bali ni sehemu ya mchakato mzima. Kwa bahati mbaya sana, hapa ndipo safari ya mafanikio ya watu wengi huwa inaishia. Wanaweka mipango, wanaitekeleza, matokeo yanapokuwa tofauti wanaachana na mipango hiyo na kwenda kwenye kitu kingine.

Ambacho kingehitajika siyo kubadili mipango, bali kuboresha utekelezaji. Kwa sababu kila mtu huwa anapata matokeo ambayo ni tofauti kabisa na matarajio ambayo alikuwa nayo. Bila kuwa na uvumilivu kwenye matokeo, hakuna mafanikio yoyote makubwa yanayoweza kufikiwa.

Ukiangalia, kila kitu ambacho umepata matokeo kwenye maisha yako, hakikuenda kama ulivyotarajia. Hata unapofanya kitu cha maendeleo, kama ujenzi, huwa inachukua muda mrefu na gharama kubwa kuliko ulivyopangilia awali. Hata pale unapokuwa umejiandaa gharama na muda kuzidi, bado kwenye uhalisia vitazidi kuliko ulivyotarajia.

Kama tunayataka mafanikio makubwa, ni lazima tuwe na uvumilivu mkubwa kwenye kuyapata. Tunachopaswa kuhakikisha ni tunakaa kwenye mchakato sahihi wakati wote, na kuendelea kubiresha kile tunachofanya. Matokeo, tusiwe na wasiwasi nayo, tuwe na uhakika kwamba yatakuja, kwa sababu tupo kwenye njia sahihi.

Tunapoyalazimisha matokeo yaje kama tunavyotaka sisi, tunakuwa kwenye hatari ya kushindwa kwenye safari nzima. Tuwe na uvumilivu mkubwa, kwa sababu mambo mazuri huwa hayataki haraka.

2. Tumia Kipimo Cha Muongo Kwenye Kuamua Unachofanya.

Kosa moja kubwa sana ambalo nimekuwa naliona kwenye maamuzi ambayo watu wanayafanya, ni kuangalia matokeo ya muda mfupi. Wengi wanaopanga kazi au biashara ya kufanya, huwa wanaangalia ni matokeo gani watakayoyapata kwa muda mfupi.

Watu huwa wanauliza, bila aibu yoyote, ni biashara gani wafanye ambayo itawapa faida kubwa ndani ya miezi sita mpaka mwaka mmoja. Ni kitu ambacho hakijawahi kuacha kunishangaza, kwa sababu ni sawa na mtu anayepanga kupata mtoto, halafu anauliza afanye nini ili mtoto huyo aweze kujitegemea mwenyewe ndani ya miezi sita mpaka mwaka. Jibu unalijua, hakuna kitu kama hicho.

Hili pia limeenda mpaka kwenye mahusiano, ndiyo maana kumekuwa na changamoto nyingi kwenye mahusiano, hasa ya ndoa. Watu wanachagua wenza, siyo kwa kigezo cha muda mrefu, bali matokeo ya muda mfupi. Wanaangalia zaidi mwonekano na kipato chao cha sasa, kuliko inavyoweza kuwa kwa kipindi kirefu kinachokuja.

Kipimo sahihi cha kuamua ni nini ufanye kinapaswa kuwa muongo, yaani miaka 10. Je unajiona ukifanya kitu hicho kwa miaka kumi bila hata kupata matokeo, lakini bado ukaendelea kufanya? Kama jibu ni hapana, basi jua kupata mafanikio kwenye kitu hicho ni vigumu.

Tafiti nyingi za mafanikio, na hata ukiangalia watu wanaoshinda tuzo mbalimbali, zinaonyesha miaka 10 ndiyo muda wa chini kabisa kwenye kupata matokeo ambayo mtu anayatarajia. Kwenye jambo lolote lile, unahitaji miaka 10 ya kulifanya ndiyo upate mafanikio unayoyataka.

Kwenye biashara ndipo kipimo cha muongo kinapaswa kueleweka sana. Maana wengi hudhani biashara ni rahisi na itawapa matokeo ya haraka. Miaka 2 ya mwanzo kwenye biashara mtu hujui hata ni nini unafanya. Hivyo hakuna matokeo makubwa unayoweza kupata.

Miaka mitatu mpaka mitano ndiyo unaielewa biashara kwa kina na kujua nini unapaswa kufanya ili kupata matokeo makubwa unayoyataka. Mwaka wa tano mpaka wa saba ndiyo unajenga msingi imara wa mafanikio makubwa, hasa baada ya kukosea kosea kwenye miaka ya mwanzo.

Na mwaka wa saba mpaka wa kumi ndiyo unayatengeneza mafanikio makubwa yanayowezekana kutoka kwenye biashara hiyo. Hapa ndipo biashara inapoaminika na wengi na kuwa na sifa inayoaminika na wengi.

Unaweza kuona hapo kwa nini wengi hawafanikiwi, kwa sababu ndani ya miaka 10 wanakuwa wameanzisha na kuacha biashara zisizopungua tano. Hivyo, muda unaenda, ila mafanikio hawayapati, kwa sababu walikosa uvumilivu unaohitajika.

Wewe kuwa na uvumilivu wa angalau miaka 10 kwenye kitu chochote unachopanga kufanya. Usifikirie chini ya hapo, utakuwa unajidanganya wewe mwenyewe. Miaka 10 ndiyo muda mfupi kwako wa kupanga kitu. Na ikiisha na bado hujapata matokeo, unapanga tena miaka mingine 10. Hiyo ndiyo maana halisi ya uvumilivu, haijalishi itachukua muda mrefu kiasi gani, wewe unaendelea kuvumilia mpaka uyapate mafanikio unayotaka.

Soma barua kamili hapa; #BZK054; ‘Uvumilivu Usio Na Subira’ Unaohitajika Kwenye Mafanikio Makubwa.