Rafiki yangu mpendwa,

Tunapotafuta kufanikiwa kwenye biashara, huwa tunahangaika na mambo makubwa sana. Ambayo yanaweza kuwa muhimu, lakini hayapo kwenye uwezo wetu kuyaelewa wala kuyafanyia kazi.

Ndiyo maana tunahitaji kuwa na wataalamu mbalimbali kwenye biashara zetu, ambao wanaelewa maeneo yao. Lakini sisi kama waanzilishi na viongozi wa biashara, tunahitaji kuwa na maarifa na ujuzi wa msingi sana unaoiwezesha biashara kufanikiwa.

Hivi karibuni nimekutana na mjadala ukieleza jinsi ambavyo biashara nyingi huwa zinayumba baada ya waanzilishi kuondoka na zikaongozwa na wataalamu. Uwepo wa wataalamu hao, ambao wanajua vizuri maeneo yao, bado unakuwa hauna msaada mkubwa kwenye biashara.

Hilo ni kweli kabisa, ni vigumu sana kwa biashara kufanikiwa kwa kutegemea kanuni za kitaalamu pekee. Biashara ni kama kiumbe hai, ndiyo maana hata kwenye sheria biashara inaposajiliwa inachukuliwa kama kitu cha kujitegemea.

Ili biashara inapofanikiwa, lazima tutumie viungo vyetu sisi binadamu, kutusaidia kuielewa biashara kwa kina na kufanya maamuzi yote muhimu.

Kwenye hii #BaruaYaKocha nimekuonyesha viungo vitano vya mwili wako ambavyo unapaswa kuvitumia kuijua biashara yako na kufanya maamuzi yenye tija. Viungo hivyo tayari unavyo, ni wewe uweze kuvitumia vizuri ili biashara iweze kunufaika.

1. Tumia Ubongo Kufikiri Na Kufanya Maamuzi.

Tunaanzia juu kabisa, kichwani, kwenye ubongo. Maamuzi muhimu ya biashara yanapaswa kufanyika kwa kufikiri kwa kina. Biashara nyingi zimeshindwa kwa sababu ya maamuzi kufanyika kwa kuiga, kufuata mkumbo na mihemko.

Ili maamuzi yaweze kufanyika kwa kufikiri, ni lazima taarifa sahihi za biashara ziweze kupatikana. Kwa kuchakata taarifa hizo, na kutumia uzoefu na maono yanayokuwepo, ndiyo maamuzi sahihi yanaweza kufikiwa.

Unao ubongo ambao unafanya kazi vizuri sana, hebu upe kazi ya kufanya maamuzi bora kwa biashara yako. Tenga muda tulivu kila siku kuifikiria biashara yako kwa kina. Kusanya taarifa sahihi za biashara yako na zitumie kwenye maamuzi yote unayofanya.

Ifikirie biashara yako kwa msingi wa kwanza (first principle), badala ya kuangalia kilichopo na kuboresha, angalia kama kingekuwa hakipo kabisa, nini kingefanyika. Biashara nyingi zimekwama kwa sababu ya kuboresha vitu ambavyo havipaswi kuwepo kabisa. Kwa kuanza kufikiria upya, unaona fursa ya kuleta matokeo ya tofauti kabisa na yale ambayo yapo kwa sasa.

Haya yote yanaweza kufanyika kwa ubongo wako tu, na taarifa ambazo tayari zipo kwenye biashara yako. Hakuna cha ziada unachohitaji, hasa ukipata kalamu na daftari kwa ajili ya kuandika. Hivyo usije ukakwama kufanya maamuzi ya biashara yako kwa sababu yoyote ile.

2. Tumia Macho Kuangalia Namba Za Biashara.

Macho yako ni kwa ajili ya kuona, na biashara yako kuna vitu vingi ambavyo inakuonyesha, lakini ni kama tu utakuwa tayari kuviona vitu hivyo. Ili biashara yako iweze kukua, macho yako yanapaswa kuwa kwenye namba za biashara hiyo.

Usiridhike tu kwa kujiambia biashara iko vizuri. Vizuri inamaanisha nini? Hapo ndipo pa kuanzia na kuhakikisha una kipimo cha kila kinachofanyika kwenye biashara.

Kila biashara inaweza kuonekana inafanya vizuri kwa sababu ina wateja na wananunua. Lakini kila biashara inayokufa huwa inaonekana hivyo. Kitu pekee kitakachoonyesha kama biashara inafanya vizuri ni namba zake. Na siyo tu namba za kukusanya mara moja, bali namba za kukusanya kwa mwendelezo na kulinganisha.

Biashara yako inapaswa kukusanya namba za msingi kila siku, kisha kulinganisha siku kwa siku ili kuona kama zinapanda au kushuka. Namba za siku zinapimwa kwa wiki, mwezi na kuendelea. Na kote kikubwa inakuwa ni kulinganisha namba za sasa na za kipindi cha nyuma, huku pia kuangalia lengo ambalo lipo.

Hayo macho uliyopewa usiyatumie tu kuvuka barabara, bali yafanye kuwa kiongo kikuu cha kupima mwenendo wa biashara yako. Hakikisha unaziona namba za biashara yako na kuchukua hatua haraka kabla mambo hayajawa mabaya zaidi.

Hakuna biashara inayoamka siku moja na kujikuta haina kabisa mauzo, au haina kabisa wateja, au haina kabisa faida, au ipo kwenye madeni makubwa. Hivyo ni vitu ambavyo huwa vinajengeka kidogo kidogo kwa muda mrefu. Kwa kuziangalia namba zako na kuona mwenendo usio sawa, unaweza kubadili mwelekeo kabla biashara haijaathirika zaidi.

Biashara inakuonyesha mengi, chagua kutumia macho yako kuyaona yote na kufanya maamuzi ambayo yataiwezesha biashara kupiga hatua kubwa.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK107; Tumia Viungo Hivi Vya Mwili Wako Kujenga Biashara Yenye Mafanikio Makubwa