Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Nikiri wazi kabisa mimi ni shabiki namba moja wa kufanya kazi kwa juhudi kubwa sana. Ninaamini, bila ya shaka yoyote kwamba chochote ninachotaka na bado sijapata ni kwa sababu bado sijaweka juhudi za kutosha ili kukipata. Na hilo linafanya niwe na wajibu mmoja tu, kuweka kazi kwa juhudi kubwa sana.
Kumekuwa na wimbi kubwa la watu kutafuta njia za mkato za kupata matokeo bila kufanya kazi kwa juhudi kubwa. Kila teknolojia mpya inapokuja, watu wamekuwa wanaamini inaenda kuondoa kabisa kazi. Lakini matokeo yake ni teknolojia zinarahisisha ufanyaji wa kazi, lakini kazi inayokuwa inahitajika ili kupata matokeo bado inabaki kuwa kubwa.
Tukichukua mfano wa Akili Unde (AI), imekuja kurahisisha sana utekelezaji wa majukumu mbalimbali. Lakini sasa, badala ya kazi kupungua ndiyo zimezidi kuongezeka. Kwa AI kuwawezesha kutekeleza majukumu ambayo hapo awali hawakuyaweza, kumewaongezea majukumu mengi ya kazi.
Pamoja na ushahidi huo, bado watu wanaendelea kuamini kuna siku teknolojia zitafuta kabisa kazi na watu kupata wanachotaka bila kuhitajika kuweka juhudi. Hizo ni ndoto ambazo zimekuwa zinawakwamisha watu kupata matokeo makubwa wanayoyataka.
Pamoja na kuweka kazi kwa juhudi kubwa kuwa hitaji muhimu la mafanikio, bado wengi wamekuwa hawaamini hilo. Na kinachowafanya wasiamini ni pale wanapowaangalia watu ambao hawajafanikiwa, lakini pia wanaonekana kufanya kwa juhudi kubwa sana.
Kwa kuona watu wanafanya kazi kwa juhudi kubwa sana na bado hawafanikiwi, kumewafanya wengi waone juhudi kubwa ya kazi siyo kiungo muhimu cha mafanikio. Unapoangalia wale wanaosemekana kuweka kazi kwa juhudi kubwa, unachoona ni wao kufanya kazi kwa masaa mengi.
Wengi wamekuwa wanadhani kufanya kazi kwa juhudi kubwa ni kufanya kazi kwa masaa mengi au muda wote. Japo muda wa kazi unachangia kwenye juhudi kubwa ambazo mtu anakuwa ameweka, peke yake hautoshi kuonyesha kwamba mtu amefanya kazi kwa juhudi kubwa.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kuangalia maana pana ya kufanya kazi kwa juhudi kubwa, ili uweze kuitumia kupata matokeo tofauti na yatakayokupa mafanikio unayotaka. Kwa kuelewa maana halisi ya juhudi kubwa ya kazi na kuiweka, kupata mafanikio makubwa inakuwa ni swala la muda tu.

1. Ni Kufanya Kile Unachosema Utafanya.
Kufanya kazi kwa juhudi kubwa ni kufanya kile ambacho umesema utafanya na kufanya kwa namna ambayo umesema utafanya au inavyohitajika kufanyika. Hilo linaweza kuonekana ni rahisi, lakini kama kuna sababu kubwa ya watu wengi kushindwa ni kutokufanya kile wanachosema watafanya na kwa namna kinavyopaswa kufanyika.
Inapokuja kwenye mafanikio, karibu kila mtu anajua kile anachopaswa kufanya ili ayapate mafanikio hayo. Lakini inapokuja kwenye kufanya hicho kinachopaswa kufanyika, ndipo ugumu unapotokea. Ugumu unatokea kwa sababu ya vikwazo na changamoto zinazokuwepo kwenye kitu chochote ambacho mtu anafanya.
Chochote kikubwa ambacho mtu utafanya, lazima utakutana na ugumu, vikwazo na changamoto. Wengi wanapofika kwenye hatua hiyo, huwa wanaacha kufanya na kwenda kwenye mambo mengine wanayoona ni rahisi zaidi. Na huo ndiyo unakuwa mwisho wa safari yao ya mafanikio.
Mafanikio makubwa yanataka ufanye kile kinachopaswa kufanyika, bila ya kujali ni nini unakutana nacho. Ni kuendelea na kitu hata pale unapokutana na ugumu na changamoto.
Hapo ndipo kufanya kazi kwa juhudi kubwa kunapohusu kutekeleza yale ambayo mtu umepanga, umeahidi au umekubali kufanya. Juhudi ya kazi inakuwa ni kujisukuma kuendelea hata pale unapokuwa na kila sababu ya kutokuendelea tena. Ni kwa kuendelea huko ndiko kunakowapa wachache matokeo makubwa ambayo wengi hawayapati.
Haijalishi ni masaa mangapi utafanya kazi, kama hutekelezi uliyopanga, uliyoahidi au uliyopangiwa, hakuna mafanikio makubwa utakayoweza kupata. Na kila unapokutana na watu wanaoonekana kufanya kazi kwa juhudi kubwa sana, kwa masaa mengi zaidi ya wengine na hawajafanikiwa, utakuta wakihangaika na mengi na kushindwa kutimiza ya msingi waliyopanga, kuahidi au kupangiwa.
Tayari unajua unachotaka na unajua unachopaswa kufanya ili upate hicho unachotaka. Sasa weka juhudi kubwa ya kazi kwa kuhakikisha unafanya kama inavyopaswa kufanyika bila ya kukubali kukwamishwa na kitu chochote.
2. Ni Kufanya Kazi Kwenye Muda Wa Kufanya Kazi.
Hakuna watu ambao huwa wanapoteza muda kama watu ambao wanafanya kazi kwa masaa mengi. Wengi wanaojisifia kufanya kazi kwa masaa mengi, sehemu kubwa ya hayo masaa wanayosema ni ya kazi, wanakuwa wanayapoteza kwa mambo yasiyokuwa na tija kabisa.
Unakuta mtu amepanga muda wa kutekeleza jukumu fulani, na muda huo unapofika anafanyia kazi jukumu hilo. Lakini sasa, anakuwa amezungukwa na usumbufu ambao unapunguza umakini wake kwenye kutekeleza jukumu hilo. Anafanya kazi kidogo, mara simu inaita, mara anajibu ujumbe, mara anaperuzi mitandao n.k. Ukihesabu muda ambao mtu anakuwa amepoteza kwenye mambo yasiyohusu kazi ila yanaingilia kazi unakuwa mkubwa.
Ni bora kupanga muda mfupi wa kufanya jukumu na kutumia muda huo kwenye jukumu hilo tu. Hapo utaweza kukamilisha kwa viwango vikubwa na usahihi kuliko ukitekeleza jukumu huku ukiwa na usumbufu. Ni kupeleka muda wa kazi kwenye kufanya kazi tu na siyo kitu kingine chochote.
Watu wengi wamekuwa wanalazimika kufanya kazi kwa masaa mengi kwa sababu wanapoteza muda mwingi kwenye mambo yasiyohusu kazi. Hata kama mtu hana usumbufu wa nje, bado anaweza kuwa na usumbufu wa ndani unaokwamisha kazi isikamilike vizuri.
Maisha ya wengi yamekuwa ni ya msongo muda wote, kwa sababu hakuna chochote wanachokifanya kwa umakini na ukamilifu. Unakuta mtu kwenye muda wa kazi anafikiria mambo yasiyohusu kazi, hivyo kazi haifanyi kwa ubora. Na muda ambao siyo wa kazi anafikiria kuhusu kazi, hivyo anajikuta haachani na kazi kabisa.
Kufanya kazi kwa juhudi kubwa ni kuwa na swichi ya kuwasha na kuzima. Wakati wa kazi unawasha hali ya kazi na kuzima nyingine zote. Kwa muda unaokuwa umewasha kazi, unahangaika na mambo ya kazi tu. Umakini wako wote unapeleka kwenye kazi unayofanya. Muda wa kazi unapoisha, unazima hali ya kazi na kuwasha vitu vingine. Ukishazima hali ya kazi huweki umakini wowote kwenye kazi tena.
Ukiweza kudhibiti umakini wako vizuri kwa muda unaopanga kufanya kazi, muda wowote ulionao unakutosha kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK157; Juhudi Kubwa Ya Kazi Ni Zaidi Ya Masaa Unayofanya Kazi.