Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Malengo yote makubwa ambayo nimejiwekea kwenye maisha yangu, kuna kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho. Na kitu hicho ni kwamba siwezi kushindwa kamwe. Ndiyo, hakuna namna yoyote ninaweza kushindwa kuyafikia malengo makubwa niliyojiwekea.
Wengi wanaposikia hivyo wanaweza kudhani ni hali ya majivuno na kujipa matumaini hewa. Lakini ni uhalisia ambao upo kwa kila mtu, ni vile watu wengi wamechagua kutokukubaliana na uhalisia huo.
Ukiwaangalia watu wote walioshindwa, ni kwa sababu wamechagua wao wenyewe kushindwa. Hakuna sababu yoyote yenye mashiko ambayo inaweza kumfanya mtu yeyote ashindwe kupambania malengo makubwa aliyonayo.
Kwenye huu urafiki wetu, kitu kimoja ambacho nataka nikusaidie ukijenge ni huo mtazamo wa kwamba huwezi kushindwa kamwe. Nataka uamini na kuishi hilo, ili uweze kuishi maisha ya tofauti na kupata mafanikio makubwa.
Kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukushirikisha jinsi unavyopaswa kujenga huo mtazamo imara ili usishindwe kamwe.

1. Kufanikiwa Au Kufa Ukipambania Mafanikio.
Sisi binadamu ndiyo viumbe hai wa kipekee sana hapa duniani. Tunapoamua jambo na tukaliendea bila kusimama, kuna mambo mawili tu yanayoweza kutokea. La kwanza ni kupata kitu hicho, yaani kufanikiwa. Na la pili ni kufa tukiwa tunaendea jambo hilo.
Unajionea mwenyewe hapo, katika mambo hayo mawili, kushindwa ni kitu ambacho hakipo kabisa. Na kushindwa hakupo kwa sababu unashindwa pale unapokuwa umeacha kuendea kile unachotaka.
Wengi hudhani kushindwa ni kutokupata kile wanachotaka, lakini kwa uhalisia, kushindwa ni kutokuendelea kupambania kile unachotaka. Kama unaendelea kukipambania, hujashindwa. Na kama utaendelea bila kuacha, ni labda utapata unachotaka au utakufa ukiwa unakipambania.
Sasa rafiki yangu, hebu niambie tu, unakubalije kuishi maisha ya kushindwa. Kama kuna mambo mawili tu yanayoweza kutokea, kushinda au kufa, kwa nini unatengeneza jambo jingine lisilokuwepo, ambalo ni kuishia njiani?
Ninachotaka kwako rafiki yangu ni uchague mafanikio unayotaka kufikia, kisha uyapambanie kwa kipindi chote cha maisha yako bila kukubali kukwamishwa na kitu chochote. Jitoe kupambania hilo kwa maisha yako yote, iwe utapata au hutapata hizo siyo shida zako.
2. Chagua Tatizo Kubwa Unalotatua.
Wengi huwa wanaona kukata tamaa na kuacha ndiyo kimewakwamisha kufanikiwa. Lakini mkwamo ulianza kabla hata ya safari yenyewe ya mafanikio kuanza. Tatizo linaanzia pale ambapo watu wanakuwa hawajui nini hasa wanapaswa kufanya ili wafanikiwe.
Wengi wamekuwa wanaiga mafanikio wanayoyaona kwa wengine, wakijaribu kufanya yale ambayo yanafanywa na wengine. Wanapokutana na magumu kwenye kufanya, wanaona siyo njia sahihi na hivyo kuacha. Hivyo ndivyo wengi wamejikuta wakijaribu mambo mengi na wasipate mafanikio.
Mahali sahihi pa kuanzia, ili uweze kukaa kwenye njia yako ya mafanikio kwa kipindi chote cha maisha yako ni kuchagua tatizo kubwa ambalo unatatua. Tatizo hilo linapaswa kuwa ambalo linakugusa kwa namna fulani na kulitatua ni kitu ambacho una msukumo mkubwa wa kufanya.
Linapaswa kuwa tatizo linalowaathiri watu wengine na ambalo wanatamani sana kupata suluhisho. Linapaswa kuwa tatizo ambalo ukilitatua, utabadili kabisa hali ya watu walionalo.
Kwa kuwa na tatizo unalotatua, unakuwa na kitu cha kupambania, ambacho unataka kushinda. Na kwa sababu tatizo hilo linakuwa linakugusa kwa namna fulani, unajiona ukiwa na wajibu wa kulitatua, hivyo huwezi kukata tamaa na kuacha.
Na pia kwa sababu tatizo linawagusa watu wengine, unapokutana na magumu bado utaendelea kwa sababu unajua siyo kwa ajili yako mwenyewe. Kitu ambacho kimekuwa kinafanya wengi kukata tamaa na kuacha ni kwa sababu ya ubinafsi wa kujiangalia wao wenyewe.
Ni vigumu sana kuamka na kuendelea na mapambano kila siku kama kitu pekee unachotaka ni upate pesa ya kuendesha maisha. Kuna njia nyingi na rahisi unazoweza kuzitumia kutatua hitaji hilo. Kitakachokuwezesha kuendelea kupambana licha ya kupitia magumu ni tatizo kubwa unalokuwa unalitatua.
Soma #BaruaYaKocha hapa; #BZK153; Mambo Ni Mawili Tu, Kufanikiwa Au Kufa Ukipambania Mafanikio