Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu cha How to Win Friends and Influence People kilichoandikwa na Dale Carnegie. Hiki ni moja ya vitabu ambavyo watu wengi wanakitaja kuwasaidia katika kuimarisha mahusiano yao na watu wengine na hata kuongeza ushawishi wao.

Wote tunajua jinsi maeneo hayo mawili yalivyo muhimu kwenye kila eneo la maisha yetu. Kuanzia kwenye kazi, biashara na hata maisha ya familia, mahusiano na ushawishi ni vitu muhimu. Unahitaji kuwa na mahusiano bora na wengine ili waweze kukupa kile unachotaka. Lakini pia unapaswa kuwa na ushawishi utakaowafanya wengine wakubaliane na wewe.

dale carnegie..jpg

Kwenye kitabu hiki, tunajifunza misingi mbalimbali ambayo ukiizingatia itakusaidia sana kwenye maeneo hayo mawili.

Kuhusu mwandishi.

Dale Carnegie (kuzaliwa 1888 kufariki 1955) alikuwa mwandishi na mhadhiri wa nchini Marekani ambaye aliendesha mafunzo mbalimbali kwenye maeneo ya maendeleo binafsi, mauzo, uneni na mahusiano hasa kwenye maeneo ya kazi.

Dale alikuwa akiendesha kozi mbalimbali vyuoni na hata kwa wale ambao wapo kwenye kazi na biashara kwenye eneo la uneni (Publick Speaking) na mahusiano.

Ujumbe mkuu unaopatikana kwenye mafunzo na vitabu vya Dale ni kwamba inawezekana kubadili tabia za watu wengine kama mtu atabadili tabia zake kwa watu hao.

Utangulizi kutoka kwa Mwandishi.

Kukabiliana na watu ni moja ya jukumu gumu ambalo kila mtu anapitia kwenye maisha. Haijalishi kama upo kwenye ajira, biashara au mama wa nyumbani, kuna nyakati unajikuta kwenye wakati mgumu kutokana na wale unaokabiliana nao.

Tafiti zinaonesha kwamba asilimia 15 ya mafanikio ya mtu inatokana na ujuzi alionao, huku asilimia 85 ikitokana na mahusiano yake na ushawishi kwa wengine. Kwenye kila tasnia, watu wanaolipwa zaidi ni wale wanaoweza kuendana na watu wengine vizuri, wanaoweza kuongoza na kuibua hamasa kwa wengine.

Wakati wa uhai wake, na akiwa kwenye kilele cha mafanikio, John D. Rockefeller aliwahi kunukuliwa akisema; “uwezo wa kuendana na watu ni ujuzi ambao unaweza kununuliwa kama sukari au kahawa na niko tayari kulipa zaidi kwa mwenye uwezo huo kuliko kitu kingine chini ya jua.”

Pamoja na umuhimu huu mkubwa na thamani iliyopo kwenye uwezo wa kujenga mahusiano na kushawishi wengine, bado ni elimu ambayo imekuwa haitolewi kwenye mfumo rasmi wa elimu.

Kupitia kitabu hiki, unakwenda kujifunza kanuni ambazo zinafanya kazi na matokeo yake yanaonekana. Kanuni ambazo ni za uhakika na zimewapa wengi matokeo mazuri kwenye eneo la mahusiano na ushawishi kwa wengine.

Kupitia kanuni hizi, watu wa mauzo wameweza kuuza zaidi kwa wateja walionao na kupata wateja wapya. Wakurugenzi wameweza kuimarisha mamlaka yao na kuongeza kipato huku wengine wakiokoa kazi ambazo walikuwa wazipoteze.

William James amewahi kunukuliwa akisema; “ukilinganisha na vile tunavyoweza kuwa, ni kama tuko usingizini. Tunatumia sehemu ndogo sana ya uwezo mkubwa wa kiakili na kimwili tulionao. Kila mtu anaishi kwa kiwango cha chini mno ukilinganisha na ukomo wake, kila mtu ana nguvu kubwa ambazo anashindwa kuzitumia.”

Lengo la kitabu hiki ni kukuwezesha wewe kutumia nguvu hizo kubwa zilizopo ndani yako ambazo mpaka sasa hujazijua na kuanza kuzitumia.

John G. Hibben amewahi kusema elimu ni uwezo wa kukabiliana na hali mbalimbali za maisha. Kama ukimaliza kusoma sura tatu za mwanzo za kitabu hiki na ukawa hujajifunza kitu ambacho kitakuwezesha kukabiliana na hali za maisha, basi kitabu hiki kitakuwa kimeshindwa kukusaidia. Lengo la kitabu hiki ni kukupa wewe hatua za kuchukua na siyo tu kukufanya ujue.

Ili uweze kunufaika kweli na kitabu hiki, lazima ufanye maamuzi sahihi, ambayo ni kuwa tayari kujifunza na kuwa na msukumo mkubwa wa kutaka kuboresha mahusiano yako na ushawishi wako kwa wengine. Kila mara jiambie; “Umaarufu wangu, furaha yangu na utajiri wangu vinategemea uwezo wangu wa kuendana na wengine.”

Kwa kila unachojifunza kwenye kitabu hiki, nenda kakijaribu kwenye maisha yako na uone matokeo utakayoyapata. Kila mara rudia kujifunza misingi hii na kuitumia kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako.

Angalizo.

Mwandishi anatupa angalizo kwamba kanuni na mbinu tunazokwenda kujifunza kwenye kitabu hiki zina nguvu kubwa ya kuwashawishi na kuwabadili watu. Lakini unapaswa kufanya hivyo kutoka ndani ya moyo wako na kwa nia njema. Usitumie kanuni hizi kuwalaghai watu au kujinufaisha binafsi. Utafanikiwa hivyo mara moja, lakini baadaye watu watajua ukweli na mahusiano yataharibika.

Njia bora ya kunufaika na kanuni hizi ni kuchagua kuishi maisha mapya, maisha ya kujali wengine kama unavyojijali wewe mwenyewe.

Kwenye uchambuzi wa kitabu hiki utajifunza haya makuu;

MISINGI MITATU YA KUKABILIANA NA WATU.

Kanuni Ya Kwanza; Usikosoe, Kuhukumu Au Kulaumu.

Kanuni Ya Pili; Toa Sifa Na Shukrani Za Kweli Na Za Dhati.

Kanuni Ya Tatu; Tambua Hitaji La Msingi La Mtu.

NJIA SITA ZA KUWAFANYA WATU WAKUKUBALI.

Njia Ya Kwanza; Wajali Wengine Kutoka Ndani Ya Moyo Wako.

Njia Ya Pili; Tabasamu.

Njia Ya Tatu; Tambua Kwamba Jina La Mtu Ndiyo Kitu Muhimu Zaidi Kwake.

Njia Ya Nne; Kuwa Msikilizaji Mzuri.

Njia Ya Tano; Ongelea Kile Ambacho Mtu Anapendelea.

Njia Ya Sita; Mfanye Mtu Mwingine Ajione Ni Wa Muhimu Na Fanya Hivyo Kwa Dhati.

KANUNI 12 ZA KUWAFANYA WATU WAKUBALIANE NA MAWAZO YAKO.

Kanuni Ya Kwanza; Njia Pekee Ya Kushinda Mabishano Ni Kuyaepuka.

Kanuni Ya Pili; Heshimu Maoni Ya Wengine, Usimwambie Mtu Amekosea.

Kanuni Ya Tatu; Unapokosea, Kubali Haraka Na Kwa Dhati.

Kanuni Ya Nne; Anza Kwa Njia Ya Urafiki.

Kanuni Ya Tano; Mfanye Mwingine Aseme NDIYO, NDIYO Mapema.

Kanuni Ya Sita; Mpe Mtu Nafasi Ya Kuongea Zaidi.

Kanuni Ya Saba; Mfanye Mtu Aone Ni Wazo Lake.

Kanuni Ya Nane; Jiweke Kwenye Nafasi Ya Mtu Mwingine.

Kanuni Ya Tisa; Wahurumie Wengine Kwa Mawazo Na Matakwa Yao.

Kanuni Ya Kumi; Tumia Nia Njema Ya Mwingine.

Kanuni Ya Kumi Na Moja; Weka Igizo.

Kanuni Ya Kumi Na Mbili; Wape Watu Changamoto.

KUWA KIONGOZI: KANUNI TISA ZA KUWABADILI WATU BILA KUIBUA HASIRA AU CHUKI.

Kanuni Ya Kwanza; Anza Kwa Kusifia.

Kanuni Ya Pili; Usiende Kwenye Kosa Moja Kwa Moja.

Kanuni Ya Tatu; Ongelea Makosa Yako Kabla Ya Kumkosoa Mwingine.

Kanuni Ya Nne; Toa Mapendekezo Badala Ya Maagizo.

Kanuni Ya Tano; Usimkosoe Mtu Mbele Ya Wengine.

Kanuni Ya Sita; Tafuta Kitu Cha Kusifia.

Kanuni Ya Saba; Mpe Mtu Sifa Kwenye Kile Unachotaka Awe.

Kanuni Ya Nane; Wape Watu Moyo Na Onesha Kosa Ni Rahisi Kusahihisha.

Kanuni Ya Tisa; Wafanye Watu Wengine Kufurahia Unachopendekeza Wafanye.

Karibu upate uchambuzi wa kitabu hiki na vingine vizuri kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA. Kujiunga na channel hiyo fungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.