Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Eneo la mafanikio ndiyo ambalo lina maarifa, taarifa, mafunzo na ushauri mwingi kuliko mengine yote. Na kwa sehemu kubwa sana, mengi yamekuwa yanakinzana yenyewe kwa yenyewe.
Watu wamekuwa wanatafuta maarifa ya mafanikio kwa nia njema kabisa ya kupata siri na kanuni ya kufanikiwa. Lakini wamekuwa wanashindwa kuchagua aina moja ya maarifa ya kufuata mpaka wapate mafanikio. Wanajikuta wakihangaika na kila maarifa, na kutokupiga hatua yoyote kubwa.
Kwa wingi wa maarifa ya mafanikio yaliyopo, na kwa jinsi ambavyo yanakinzana, mtu anaweza kuona kila wakati anapata siri za mafanikio zilizofichwa. Ambacho wanashindwa kuelewa ni kwamba wanakuwa wanapoteza muda kwa kufanya mambo ambayo yanakinzana.
Njia za kufanikiwa zipo nyingi sana, na zote zinafanya kazi. Kila maarifa ya mafanikio unayoyapata, yana watu ambao wameyatumia wakapata matokeo. Lakini hilo halimaanishi kwamba na wewe ukitumia njia hiyo utapata matokeo.
Njia sahihi ya mafanikio kwako ni ya kipekee kabisa kwako. Ni njia unayopaswa kuielewa, ambayo inaendana na wewe na inakupa matokeo sahihi kwako. Kutokujua njia hiyo sahihi kwa mafanikio ya mtu kumesababisha wengi kuhangaika sana lakini wasifanikiwe.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujikumbusha njia iliyo sahihi kwako kufanikiwa ili ukae kwenye hiyo na uache kuhangaika na njia nyingi zinazojitokeza kila wakati.

1. Kipimo Cha Kweli Cha Mafanikio
Hadithi za mafanikio zimefanya uharibifu mkubwa kuliko kuwa msaada. Wale waliofanikiwa wanaposhirikisha hadithi za safari zao, wengi wanaondoka na masomo yasiyo sahihi.
Wengi wanapojifunza kwamba mtu alipita njia fulani na akafanikiwa, na wao pia wanaiga njia hizo walizopita ili wapate mafanikio kama yao. Ambacho watu hawajui ni kwamba mafanikio ni kitu kinachotokea mara moja tu na hakiwezi kurudiwa tena. Hata mtu anayetoa hadithi yake ya mafanikio, akirudia kufanya kila alichofanya hataweza kupata matokeo aliyopata.
Kipimo cha kweli cha mafanikio ni kama umepata kile unachotaka kwenye maisha yako. Hiki ndiyo kipimo halisi, ambacho kinategemea na mtu mwenyewe anataka nini. Na kwa sababu mafanikio yana maana tofauti kwa kila mtu, basi njia za mafanikio zinakuwa tofauti kwa kila mtu.
Kuna watu huwa wanaanzia chini, wanapambana sana na kufanikiwa. Lakini wanapoyapata mafanikio, bado wanakuwa na hali ya kutokuridhika. Kinachosababisha hilo ni mtu kufanikiwa kwa vipimo vya wengine na siyo vipimo vya ndani yake mwenyewe.
Unaweza kujiuliza kama mafanikio ni rahisi kiasi hicho kwenye maelezo, kwa nini wengi bado hawafanikiwi? Na jibu lipo wazi, ni rahisi kuiga kile kinachofanywa na wengine kuliko kutafakari na kupata kile hasa kinachotoka ndani yako. Kwa sababu watu huwa wanapenda vitu rahisi, wanaishia kuingia kwenye njia inayowapoteza.
Kabla hujaendelea kukimbizana na mafanikio ambayo huyapati, jitafakari kwanza ni nini hasa unachotaka kwenye maisha yako. Ni nini kinachotoka ndani yako wewe, ambacho ukikitimiza au kukipata utaridhika sana. Hicho ndiyo utakachopaswa kupambania kwa maisha yako yote.
2. Hakuna Jibu Moja Sahihi Kwa Watu Wote
Maisha ni shule isiyo na ukomo na mafanikio ni mitihani tunayopewa. Unapofaulu mitihani hiyo ndiyo unakuwa umefanikiwa. Kwa bahati mbaya sana, wengi wamekuwa wanafeli hiyo mitihani, kwa sababu moja kubwa, kuiga majibu ya wengine.
Fikiria umeingia kwenye chumba cha mtihani, wote mkapewa mitihani na kuanza kuijibu. Unasoma maswali na kuanza kujibu, lakini unapoangalia waliokaa karibu na wewe, majibu yao ni tofauti na yako. Unaona ni kama unakosea, hivyo unakata majibu yao na kuandika majibu kama ya hao wengine. Matokeo ya mtihani yanapokuja, unajikuta umefeli, wakati uliowaiga wamefaulu.
Katika hali kama hiyo unaweza kuona kama umechezewa mchezo fulani ili ufeli kwa makusudi. Lakini ukweli ni mmoja, japokuwa mlikuwa kwenye chumba kimoja cha mtihani, mlikuwa na mitihani tofauti. Hivyo majibu yaliyokuwa sahihi kwa wengine, hayakuwa sahihi kwako, kwa sababu mitihani yenu haikufanana.
Hivyo ndivyo safari ya mafanikio ilivyo. Watu waliofanikiwa wanaweza kushirikisha kwa ukweli kabisa kila walichofanya mpaka kufanikiwa. Na wewe ukaiga kila walichofanya kwa usahihi kabisa, na bado usifanikiwe.
Wengi wanapokwama kufanikiwa licha ya kuiga yale wanayosema waliofanikiwa, huwa wanaona kuna siri ambazo zimefichwa kuhusu mafanikio. Wanaamini waliofanikiwa wanasema mambo machache na mengine wanayaficha. Lakini huo siyo ukweli, waliofanikiwa wanaweza kusema kila kitu na bado visikusaidie kwa sababu kilicho sahihi kwao hakitakuwa sahihi kwako.
Unachopaswa kuelewa ni kwamba kwenye kila eneo la maisha, hakuna jibu moja sahihi kwa watu wote. Kitu ambacho kwa aina fulani ya watu kinaweza kuwa sahihi kabisa, kwa watu wengine kinaweza kisiwe sahihi kabisa.
Watu wamejipoteza sana kwenye kuiga tabia za mafanikio, wasijue siyo zote zinawafaa wao. Wapo wanaokazana kuiga tabia na nidhamu za waliofanikiwa na bado wanakwama, kwa sababu ni vitu vinavyokuwa haviendani na wao.
Kwenye eneo la fedha ndiyo kabisa watu huwa wanachanganyikiwa sana kwa kuwaiga wengine. Kuanzia kwenye njia za kuingiza kipato mpaka kuweka akiba na kufanya uwekezaji. Kinachofanya kazi kwa watu fulani hakiwezi kufanya kazi kwako.
Kwenye biashara ndiyo kuna matatizo makubwa zaidi. Mtu anaweza kuona watu wengine wanafanikiwa kwenye biashara ya aina fulani. Anapata msukumo wa yeye kufanya biashara hiyo pia, lakini hapati mafanikio kama ya hao wengine. Hiyo ni kwa sababu biashara hiyo inaweza isiendane nao.
Unachopaswa kukumbuka mara zote ni kwamba hakuna jibu moja sahihi kwa watu wote. Kila mtu ana jibu sahihi kwake, kulingana na kile anachotaka, na vile alivyo yeye. Kulazimisha kufanya wanachofanya wengine ili upate wanachopata wao ni kuchagua kujipoteza wewe mwenyewe.
Soma #BaruaYaKocha hapa; #BZK151; Njia Za Mafanikio Ni Nyingi, Lakini Sahihi Kwako Ni Hii