Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kitu kimoja ambacho nimekuwa nakuambia kila wakati, na ambacho ninakiamini bila ya shaka yoyote ni kwamba mafanikio makubwa unayoyataka, yanawezekana.
Ndiyo, inawezekana kabisa kwa wewe kuwa na aina ya maisha ambayo umekuwa unayaota kwa muda mrefu. Lakini sasa, kabla hujayapata hayo mafanikio, cha moto lazima utakiona. Ndiyo, lazima upite kwenye moto mkali ili uondoe makapi yote ambayo yamekuwa yanakuzuia kufanikiwa.
Kama ambavyo chuma na dhahabu husafishwa kwa moto mkali, ndivyo sisi binadamu tunalazimika kupitishwa kwenye moto ndiyo tuweze kupata mafanikio makubwa tunayoyataka.
Kwa bahati mbaya sana, pale watu wanapopita kwenye moto huo, wanakimbia. Wanaacha kile ambacho kinawapitisha kwenye moto na kwenda kutafuta vitu ambavyo ni rahisi zaidi.
Yaani ni sawa na mgonjwa anayeenda hospitali na kupewa dawa za sindano, sasa kwa sababu sindano inauma, anaamua kuachana na hayo matibabu. Matokeo yake ni kutokupona ugonjwa aliokuwa nao.
Kinachowazuia wengi kupata mafanikio makubwa wanayoyataka ni kukimbia kipindi ambacho wanapitia moto wa kuwasafisha kwenda kwenye mafanikio hayo.
Kwa sababu, unaweza kuelezeaje mtu ambaye kwa zaidi ya miaka 10 amekuwa anapambana kufanikiwa ila hakuna hatua kubwa alizopiga? Maelezo pekee unayoweza kuwa nayo ni kwamba kuna nyakati ngumu amekuwa anakutana nazo na anazikimbia. Hakuna kingine kinachoweza kuelezea hali hiyo.
Na hatuwezi kuwalaumu sana watu kwa nini wanakimbia pale wanapokuwa wanapitia hali ngumu. Kwa sababu mwanzo wa hali ngumu kila mtu anaweza kuvumilia na kuendelea. Lakini huwa inafika mahali na mtu anaona hawezi kuendelea tena.
Huo ni wakati ambao mtu anakuwa ameelemewa kupita kiasi. Akiangalia mbele anaona giza na matumaini yote yanakuwa yamefutika. Hapo ndipo wengi hukata tamaa na kuacha kile walichokuwa wanapambania.
Ambacho wanakuwa hawajajua ni kwamba pale mtu unapojiona umeelemewa na huwezi tena, unakuwa karibu mno na mafanikio makubwa unayoyataka. Kama wanavyosema waswahili, kunapokaribia kukucha, giza ndiyo huwa kubwa zaidi.
Unanijua mimi rafiki yako, nimejipa wajibu wa mafanikio yako makubwa. Na najua wapi umekuwa unakwama, hasa unapoyapitia magumu ambayo ni sehemu ya hiyo safari. Huwa unafika mahali na kuwa umeelemewa sana kiasi cha kuona mambo hayawezekani tena.
Ni kwenye huo wakati ndiyo nakutaka ukumbuke mambo ya msingi sana, ambayo yatakupa nguvu ya kuendelea. Hata kama mambo yataonekana ni magumu kiasi gani, kwa kukumbuka haya unayokwenda kujifunza kwenye hii #BaruaYaKocha, utapata nguvu ya kuendelea.

1. Umeshapitia Mengi Magumu Kuliko Unayopitia Sasa.
Kitu kimoja kizuri, na pia kibaya kuhusu sisi binadamu ni kwamba huwa tunasahau. Kusahau ni kuzuri kwa sababu kunaondoa kumbukumbu za mabaya ambayo tumewahi kukutana nayo ili yasitukwamishe. Na pia kusahau ni kubaya kwa sababu kunafanya tuone magumu tunayokutana nayo kila wakati ni makubwa zaidi ya yaliyopita.
Unaweza kuwa unapitia magumu sana kwa wakati huu, na ukaona hayo ndiyo mambo magumu zaidi ambayo umewahi kupitia kwenye maisha yako. Lakini kama utavuta kumbukumbu zako vizuri, huko nyuma umewahi kupitia magumu zaidi ya unayopitia sasa. Umewahi kufika mahali na kuona hakuna kinachoweza kutokea tena. Lakini uliweza kuvuka magumu hayo na sasa uko hapo ulipo sasa.
Ukipita muda na ukapitia matatizo yote makubwa ambayo umewahi kuyapitia kwenye maisha yako, utagundua mengi sana yalishatatuliwa. Kuna ambayo uliyatatua wewe mwenyewe, kuna ambayo yalitatuliwa na wengine na kuna ambayo yalijitatua yenyewe.
Kitendo cha wewe kuwa hai mpaka sasa, ni uthibitisho kwamba umeshinda magumu na changamoto nyingi. Tangu utoto wako mpaka sasa umejaribiwa mara nyingi mno, lakini umekuwa unashinda, na ndiyo maana uko hai mpaka sasa.
Wakati wowote unapokuwa unapitia magumu na changamoto na ukaona kama ndiyo mwisho wa safari yako ya mafanikio, jikumbushe magumu ambayo uliwahi kupitia huko nyuma na ukayashinda. Hilo likupe moyo kwamba na hayo unayopitia utayashinda pia, kwa sababu una historia nzuri ya kufanya hivyo.
Kamwe usikate tamaa kwa sababu ya magumu na changamoto unazokutana nazo. Siyo kitu kigeni kwako, umekuwa unashinda na sasa utashinda pia. Wajibu wako ni kuendelea bila kukata tamaa.
2. Matatizo Yako Siyo Kitu Kipya Hapa Duniani, Wengi Wameyapitia Pia.
Huwa kuna kauli inasema hakuna tusi geni, matusi yote ni yale yale, lakini bado watu wakitukanwa wanakasirika na kujisikia vibaya.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye matatizo ambayo tunakutana nayo hapa duniani. Hakuna tatizo jipya, ambalo ndiyo linatokea kwako kwa mara ya kwanza kabisa. Kila tatizo unalokutana nalo, limewahi kuwatokea watu wengine wengi sana. Na kwa bahati nzuri sana, watu hao waliweza kutatua matatizo hayo na kupata wanachotaka.
Iwe ni kuondokewa na watu wa karibu, kupoteza kazi, biashara kushindwa, mahusiano kuvunjika, kulaghaiwa, kudhalilishwa na mengine mengi, hakuna kitu kipya. Na uzuri, matatizo uliyonayo wewe, wakiwa nayo watu wengine huwa unawafariji vizuri tu. Lakini yakifika kwako unaona kama ni ya kipekee sana na hayawezekani.
Simaanishi kwamba matatizo unayokutana nayo siyo matatizo, ni matatizo kweli na yana nguvu ya kukukwamisha. Ambacho nataka kukukumbusha ni kwamba siyo matatizo ya kipekee sana kwako au kwa wanadamu. Ni mambo ambayo yamekuwa yanatokea kwa wengine na huenda yamewahi kutokea kwako pia.
Na kwa sababu maisha yamekuwa yanaendelea licha ya matatizo hayo, ndivyo pia maisha yako yanavyopaswa kuwa. Hakikisha unaendelea na safari yako ya mafanikio bila kujali ni matatizo gani unayopitia. Wewe jifunze jinsi ambavyo wengine wamekuwa wanakabiliana na matatizo hayo na ukabiliane nayo pia. Muhimu ni chochote kisikwamishe safari yako.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK148; Mambo Yamekuelemea? Kumbuka Haya Ya Msingi Ili Usikate Tamaa