Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Safari ya mafanikio makubwa ni moja ya safari rahisi sana kwa mtu anayejua jinsi ya kuiendea. Lakini kwa walio wengi, imekuwa ni safari ngumu na inayowafanya wengi washindwe na kukata tamaa.
Unaweza usielewe pale ninapokuambia ni safari rahisi, wakati wewe umekuwa unapambana sana na bado hufanikiwi. Utakuwa sahihi kwa upande wako kuona ni ngumu, lakini hilo haliifanyi safari kuwa ngumu kwenye uhalisia.
Unajua kuna kitu kimoja ambacho watu huwa hawakielewi, ugumu na urahisi ni vitu vinavyotegemea yule anayesema. Kama ilivyo uzuri unamtegemea anayeuona, kinachoonekana kigumu kwa mtu mmoja, kwa mwingine kinaweza kuwa rahisi.
Inapokuja kwenye mafanikio, ni rahisi kwa sababu moja, yana mchakato. Kitu chochote ambacho kina mchakato, ambao mtu akiufuata anapata matokeo, hakiwezi kuwa ni kigumu.
Ila watu watasema ni kigumu, kwa sababu wanataka wapate kitu kwa njia zao badala ya kufuata mchakato. Ni pale watu wanapohangaika na njia zao na kukosa matokeo ndiyo hulalamika kwamba kitu ni kigumu.
Huwa kuna kauli ya Kiswahili inayosema; “Mzoea vya kunyonga, vya kuchinja haviwezi.” Hii ni kauli yenye maana kubwa sana, hasa inapokuja kwenye safari ya mafanikio.
Ukisikiliza mazungumzo ya watu ambao hawajafanikiwa na wanapambana sana ila hawafanikiwi, kisha ukasikiliza mazungumzo ya watu ambao wamefanikiwa, ni kama watu hao wapo kwenye dunia tofauti kabisa.
Wengi ambao hawajafanikiwa licha ya kupambana unawakuta wakihangaika na njia za mkato za kupata mafanikio, kitu ambacho kinawafanya wapoteze zaidi. Lakini wale waliofanikiwa wanaujua mchakato wao na wanaufanyia kazi bila kutafuta njia za mkato.
Hili linaweza kueleweka kwa ujumla, na njia za mkato zikaonekana kama njia za udanganyifu. Lakini ni kitu ambacho kinagusa maeneo mengi na hizo njia za mkato siyo lazima ziwe za udanganyifu. Hata njia ambazo ni halali kabisa, lakini havifuati mchakato sahihi, ni kikwazo kwa mafanikio makubwa.
Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia jinsi kuzoea vya kunyonga kunavyokukwamisha kufanikiwa, ili uachane na njia hiyo na ufanikiwe.

1. Usiibe, Jenga.
Kuna njia mbili za kupata kitu unachotaka, kuiba au kujenga.
Kuiba siyo lazima iwe kwa kuchukua kwa hila, bali inamaanisha kuchukua kitu ambacho tayari kipo. Inaweza kuwa kwa kuiga au kwa kupewa. Unakuwa umepata kitu bila ya kupita kwenye mchakato wa kukijenga hatua kwa hatua.
Kujenga ni kuanza na kitu upya kabisa, kisha kufuata mchakato wa kukifanya kitokee. Kujenga ni kuleta kitu kipya, ambacho hakijawahi kuwepo kabisa.
Kuiba ni rahisi, hakuhitaji kazi kubwa wala muda mrefu. Ni kuona kitu ambacho kipo na kisha kuamua kuwa na kitu kama hicho, kama kilivyo. Kwa wengi huwa ni kuiga kitu kwa jinsi kinavyoonekana nje.
Kujenga ni kugumu, kunahitaji kazi na muda mpaka kitu kipya kiweze kutokea. Kuna makosa mengi ambayo mtu atayapitia wakati wa kujenga mpaka aje apate kile anachotaka. Kujenga ni kupambania maono ambayo yapo ndani yaweze kutokea kwenye uhalisia.
Kama ilivyo kwenye asili, kitu chochote kinachopatikana kwa urahisi huwa kinapotea kwa urahisi pia. Chochote unachoiba, kinaibiwa kutoka kwako pia. Ukiiga kile ambacho wengine wanacho, wengine pia wataiga kutoka kwako au kutoka ulikoiga wewe. Hivyo licha ya kupata kwa haraka na urahisi, unapoteza hivyo hivyo pia.
Kwa kanuni hiyo hiyo ya asili, kujenga ni kugumu, hivyo chochote kinachojengwa huwa kinakuwa kigumu kuangusha au kupotea. Kadiri inavyokuwa ngumu kujenga, ndivyo wengi wanavyoshindwa kufanya hivyo. Na kwa wale wanaokuja kuiga kwa nje kile kilichojengwa, wanaishia kuanguka vibaya kwa sababu hawajui kilichojengwa ndani.
Kwenye safari yako ya mafanikio, mara nyingi utakutana na njia mbili mbele yako, ya kuiba na ya kujenga. Wewe chagua njia ya kujenga mara zote, itakuwa na wachache, lakini pia ndiyo itakayokupa matokeo makubwa na yatakayodumu.
Kwa wengi ambao hawajafanikiwa, wameshazoea sana vya kunyonga, ambapo ni kuiba na kuiga. Ni rahisi kuangalia kile wengine wanafanya na kukiiga. Lakini kufikiria kitu kipya na kukijenga, hatua kwa hatua, huko ni kuchinja na wengi hawataki huo mchakato mrefu wa kuchinja. Wewe usiwe wa kuendeleza kunyonga, anza kujifunza kuchinja ili upate nyama safi.
2. Usiibe Wafanyakazi, Jenga Timu Yako.
Unapotaka kujenga biashara, wafanyakazi ni sehemu muhimu. Ukuaji wa biashara yoyote ile unategemea wafanyakazi walio ndani ya biashara hiyo. Kama ni wenye uwezo mzuri na wanaoendelea kukua, biashara nayo inakua. Lakini kama wana uwezo mdogo na hawakui, biashara pia haiwezi kukua.
Ili kuharakisha matokeo, biashara nyingi huwa zinakimbilia kuiba wafanyakazi wakati wa kuajiri. Zinafanya hivyo kwa kuchukua wafanyakazi wenye uzoefu kutoka kwenye biashara nyingine. Wanachodhani ni wakichukua wafanyakazi wenye uzoefu, wataweza kuhamisha uzoefu walionao na kuleta matokeo makubwa kwa haraka.
Lakini, mara nyingi sana hicho siyo kinachotokea. Wafanyakazi wanaweza kuwa na uzoefu mkubwa kwenye biashara moja, lakini wanapopelekwa kwenye biashara nyingine, uzoefu wao hauwasaidii kabisa. Hiyo ni kwa sababu biashara huwa zinatofautiana sana.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanashindwa kuelewa pale wanapoajiri watu wenye uzoefu na ambao waliahidi makubwa, lakini hawaleti matokeo waliyotegemea.
Tatizo linarudi pale pale kwenye kuiba badala ya kujenga. Kama unataka kuwa na wafanyakazi wanaokupa matokeo, ni lazima ujenge timu bora ya biashara. Ni lazima uajiri watu sahihi, kisha uwajenge kwa uzoefu wa biashara yako.
Hata kama mtu ana uzoefu mkubwa kwenye biashara nyingine, anapokuja kwenye biashara yako ni lazima ajengwe upya. Hata kama ni aina moja ya biashara, bado ndani ya kila biashara kuna mambo ya kipekee. Maono na tamaduni zinatofautiana sana. Bila ya watu kujengwa kwenye maono na tamaduni hizo, hawawezi kuleta matokeo.
Iwe utaanza na wafanyakazi wapya ambao hawana uzoefu, au utaajiri wafanyakazi wenye uzoefu kutoka kwenye biashara nyingine, tambua kwamba kujenga hakukwepeki. Ni lazima uweke kazi kwenye kuijenga timu yako kwa namna ambayo itakupa matokeo ambayo unayataka.
Usitafute njia ya mkato ya kupata wafanyakazi wa biashara, hakikisha una programu sahihi ya kuwajenga wafanyakazi kwa mafunzo na usimamizi mzuri ili walete matokeo yanayotarajiwa.
Soma #BaruaYaKocha hapa; #BZK147; Kupenda Vya ‘Kunyonga’ Kunavyokuzuia Kupata Mafanikio Makubwa Unayoyataka