Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Pesa ndiyo lugha inayoeleweka na watu wote duniani. Ndiyo dini inayowaunganisha watu wote. Watu watatofautiana kwenye mambo yote, lakini inapokuja kwenye pesa, wote wanakubaliana kwenye kitu kimoja.
Pesa ni muhimu kwenye kuendesha maisha yetu ya kila siku. Ndiyo inatuwezesha kupata yale tunayotaka na kuendesha maisha yetu kwa namna tunavyotaka. Ukitoa pumzi unayopumua bure, pesa ndiyo kitu cha pili kwa umuhimu kwenye maisha.
Pesa pia ni moja ya vipimo vya mafanikio. Japo wengi huwa hawapendi sana kipimo hicho, lakini ni vigumu sana ukawa na maisha ya mafanikio wakati una shida ya pesa. Japo pesa haiwezi kuwa kipimo pekee cha mafanikio, hakuna mafanikio ambayo hayawezi kuhusisha kabisa pesa.
Kwa umuhimu huo wa pesa, imekuwa sehemu kubwa ya majukumu yetu kwenye maisha. Muda wetu mwingi tumekuwa tunautumia kwenye kujihusisha na mambo ya pesa. Iwe ni kwenye kuzitafuta, kuzitumia au kuzitunza, kila siku tunajihusisha na pesa kwa muda mrefu.
Tunapanga na kusema kwamba tunataka kupata pesa zaidi. Tunakimbizana na kila aina ya fursa ambayo tunaona itatupatia pesa zaidi. Lakini tunapokuja kuangalia kwa undani, tunagundua tunapoteza pesa nyingi kuliko ambazo tunapata.
Najua unaweza usiamini hilo, kwa jinsi ambavyo unapambana kupata pesa na kuzitunza, unaona wewe hupotezi pesa, kwa sababu bado una uhitaji nazo mkubwa.
Lakini kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukuonyesha jinsi ambavyo umekuwa unapoteza pesa nyingi kuliko unavyopata. Na ukiweza kuona hilo na kulirekebisha, utaweza kubadili hali yako ya kifedha na kujenga utajiri unaotaka kuwa nao.

1. Muda Ni Zaidi Ya Pesa.
Huwa kuna kauli kwamba muda ni pesa, ikiwa na maana kwamba muda una thamani sawa na pesa. Kauli hiyo haisemi ukweli wote, ambao ni muda ni zaidi ya pesa.
Ukipoteza pesa, unaweza kupata nyingine, lakini ukipoteza muda, huwezi kupata tena mwingine. Kwa jinsi muda ulivyo na ukomo, thamani yake ni kubwa kuliko pesa.
Cha kushangaza sasa, pamoja na thamani hiyo kubwa ya muda, bado watu wengi wamekuwa wanapoteza muda bila kujali. Watu wengi wamekuwa wanaruhusu muda wao upotee bila ya kuwa na tija yoyote. Na hapo ndipo upotevu wa pesa unapoanzia, kwa sababu kama muda ni zaidi ya pesa, kuupoteza ni zaidi ya kupoteza pesa.
Sehemu ya kwanza ya kudhibiti upotevu wa pesa zako ni kudhibiti upotevu wa muda. Unapaswa kuanza na kusimamia vizuri muda wako, ili uupeleke kwenye mambo yenye tija na ambayo yana mchango kwako kifedha.
Na ili uweze kusimamia vizuri muda wako ili usipoteze pesa, ni lazima ujue thamani halisi ya muda wako.
2. Thamani Halisi Ya Muda Wako.
Muda huwa ni rahisi kupotezwa kwa sababu watu wengi hawajui thamani halisi ya muda wao. Wao wanaona muda kama sekunde, dakika, masaa na siku ambazo zinaenda. Kwa kuwa hakuna thamani kwenye huo muda, hata unapopotea mtu haoni akiwa amepoteza.
Kila muda wako una thamani ya kifedha, hata kama huijui. Na kila unapopoteza muda, hata kama ni dakika, unapoteza pesa, hata kama huoni hilo moja kwa moja. Tunaweza kusema upotevu wako wa muda ndiyo umekuzuia kupata kiasi cha pesa ambacho umekuwa unakitaka.
Kama usingekuwa unapoteza muda kabisa, yaani kama ungejua thamani ya muda wako na kuiheshimu, tayari ungekuwa na pesa nyingi kuliko ulizonazo sasa.
Kama hukujua hilo, leo una nafasi ya kujua na utaamua kama utathamini muda wako au la.
Kukokotoa thamani halisi ya muda wako, anza na lengo lako la kipato unachotaka kuingiza. Kipato ambacho unaona kitatosha kuendesha maisha yako kwa namna unavyotaka na kuweza kuweka akiba na kuwekeza. Jua lengo hilo kwa mwezi. Kama hujui upangeje lengo hilo, anza na kipato chako cha sasa na zidisha mara mbili.
Baada ya kupata lengo la kipato chako kwa mwezi, ligawe kwa idadi ya siku ambazo unafanya kazi kwenye mwezi. Kama unafanya kazi kwa siku 6 za wiki, kwa mwezi utakuwa na siku 26 za kufanya kazi. Hivyo utachukua lengo la mwezi na kugawa kwa siku hizo.
Hapo utapata kiasi cha kipato unachopaswa kuingiza kila siku. Gawa lengo la siku kwa masaa, kwa kutumia masaa unayofanya kazi kwa siku. Kama unafanya kazi masaa 8, chukua lengo la siku na ugawe kwa 8. Hapo unapata thamani ya saa yako moja.
Kwa thamani ya pesa kwa saa moja ya kazi uliyopata, hiyo ndiyo unayopaswa kuitumia kwenye kufanya maamuzi yako yote. Kwa kila muda ambao umetenga kwa ajili ya kazi, unapaswa kutumika kwenye mambo ambayo yanaleta kiasi hicho cha pesa.
Unapopoteza muda wa kazi, unapoteza kiasi hicho cha pesa. Sasa unaweza kuona ni kwa nini nakuambia upotevu wa muda ndiyo umekukwamisha kuwa na kipato ambacho umekuwa unataka kuwa nacho.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK146; Hivi Ndivyo Unavyopoteza Pesa Nyingi Kuliko Unavyopata Na Kujizuia Kujenga Utajiri Unaotaka