Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Tumekuwa na hali ya kujisahau na kulazimisha mambo yaende kwa mazoea, wakati kwenye uhalisia ni kitu ambacho hakiwezekani. Matokeo ya kujisahau huko yamekuwa ni kubweteka au kukata tamaa.
Kubweteka kunatokana na kujisahau pale mambo yanapokuwa mazuri. Kwenye nyakati hizo, tunadhani kwamba mambo yataendelea kuwa mazuri hivyo kwa wakati wote. Matokeo yake ni kushindwa kuchukua hatua sahihi na kukosa maandalizi ya mambo yanapobadilika.
Kukata tamaa kunatokana na kujisahau pale mambo yanapokuwa mabaya. Kwenye nyakati hizo, tunadhani kwamba mambo yataendelea kuwa mabaya hivyo wakati wote. Matokeo yake ni kuona hatuwezi kuendelea tena na hivyo kukata tamaa.
Hali zote mbili, za kubweteka na kukata tamaa zimekuwa kikwazo kwa wengi kupata mafanikio makubwa wanayoyataka. Wengi hudhani kikwazo cha mafanikio ni hali mbaya pekee, lakini hata hali nzuri ni kikwazo, kwa sababu zinawafanya watu kuridhika na kukosa maandalizi sahihi ya kukabiliana na mabadiliko.
Ili kupata mafanikio makubwa tunayoyataka na tuweze kudumu nayo kwa muda mrefu, tunapaswa kuondoka kwenye hali hiyo ya kujisahau. Tunapaswa kujikumbusha kwamba kitu chochote tunachokuwa tunapitia, hakitadumu milele. Kwa kujua ukweli huo na kuuishi, tutaweza kutumia kila hali na wakati tunaopitia kufika kule tunakotaka kufika.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza jinsi ya kuondoka kwenye hali hiyo ya kujisahau ambayo imekuwa kama mazoea kwetu binadamu. Ni muhimu sana ujifunze haya na kuyafanyia kazi ili mafanikio yawe ya uhakika kwako.

1. Hakuna Kinachodumu Milele.
Ukweli kuhusu maisha ni kwamba hakuna kitu chochote kinachodumu milele. Najua hiyo siyo habari mpya, tunajua jinsi vitu vimekuwa vinakuja na kupita, hata pale tunapotaka sana vikae, vimekuwa havikai.
Lakini kulikubali hilo kwenye uhalisia huwa inakuwa vigumu. Pale tunapokitaka sana kitu, tunashawishika kuamini kwamba kitaendelea kuwepo na kuendelea kukifaidi. Tunajisahau na kukosa maandalizi ya mambo yataendaje pale kitu hicho kitakapokuwa kimeondoka.
Na hata kwa upande wa mambo magumu na changamoto. Tuna historia nzuri ya mambo magumu na changamoto ambazo tulishapitia huko nyuma na tukaweza kuzivuka, lakini kila changamoto mpya tunayokutana nayo tunaona kama ndiyo mwisho wa dunia. Tunaona ni kubwa sana kuliko uwezo wetu wa kuhimili. Hilo ndiyo limekuwa linasababisha watu kukata tamaa na kuacha, kwa kuona hawana tena namna nyingine.
Kitu ambacho tunapaswa kuendelea kujikumbusha kila wakati ni kwamba mabadiliko yanaendelea na kamwe hayatasimama. Kila wakati vitu vinabadilika na kuwa vipya, hakuna chochote kinachodumu milele. Hata pale inapoonekana kwa nje kwamba vitu vipo vile vile, kwa ndani vinabadilika.
Kuna vitu ambavyo mabadiliko yake ni ya haraka na yanaonekana wazi. Halafu kuna vitu ambavyo mabadiliko yake ni ya taratibu na hayaonekani. Haijalishi ni nini tunachoona, uhakika ni kwamba vitu vinabadilika.
Wakati mwingine tunayatambua na kuyaona mabadiliko, lakini tunaona kama ni mabadiliko mabaya. Pale mambo yanapobadilika kutoka yenye manufaa na kuwa yasiyo na manufaa, tunaona kama mabadiliko hayo ni mabaya.
Pamoja na mabadiliko kuleta hali ambazo hazitupendezi, kila mabadiliko ni mazuri, kama yakiweza kutambulika na kutumiwa vizuri. Kwa sababu, kama mabadiliko lazima yatokee, haina maana yoyote kuona ni mabaya na kuyachukia. Badala yake tunapaswa kuangalia ni uzuri gani upo ndani ya kila mabadiliko na kuutumia.
Kwa kuwa vitu vimekuwa vinabadilika kwa kipindi chote cha maisha yetu, na kwa kuwa tumeendelea kuwa hai kwenye mabadiliko yote hayo, ni dhahiri kwamba mabadiliko yote ni mazuri.
Mafanikio makubwa yanatutaka kuona uzuri wa kila mabadiliko yanayotokea na kuutumia kupata matokeo mazuri na makubwa zaidi.
2. Chochote Kinachotokea Sasa, Kamwe Hakitatokea Tena.
Kwa asili, hakuna kitu chochote ambacho ni cha uhakika. Kanuni ya kutokuwepo kwa uhakika inasema kitu pekee cha uhakika ni kwamba hakuna uhakika.
Lakini kuna uhakika mwingine wa maisha, ambao upo hivyo wakati wote, iwe tunakubali au hatukubali.
Uhakika huo ni kwamba; ‘Chochote kinachotokea sasa, kamwe hakitatokea tena.’
Maisha yetu yanaweza kuonenaka ni mwendelezo wa mambo yale yale, ambayo yamekuwa yanatokea kwa namna ile ile, lakini kwa uhalisia, hakuna kitu chochote kinachotokea kwa kujirudia, hakipo kabisa.
Huwa kuna kauli inayosema, ‘Huwezi kuvuka mto mmoja mara mbili, mara ya pili hautakuwa mto ule ule na wewe hautakuwa mtu yule yule.’
Kauli hiyo inaeleza vyema kwa nini hakuna kitu chochote kinachotokea mara mbili, hata kama maisha yako yanaonekana vile vile.
Kila kitu kinachotokea kwenye maisha yetu, huwa kinatubadili kwa namna fulani. Hivyo kinapoendelea kutokea, hakiwi tena kwa sisi vile tulivyokuwa. Na hata kinaporudia kutokea, tunaendelea kubadilika.
Kwa nje maisha yanaweza kuonekana ni yale yale, kazi au biashara ni ile ile, mahusiano yale yale, lakini kwa ndani kila wakati tunakuwa watu wapya na kukabiliana na mambo hayo kwa utofauti.
Na hilo ndiyo limekuwa linatengeneza uzoefu na matokeo tofauti kwa watu tofauti wanaokuwa kwenye kitu kimoja. Watu wawili wanaweza kuwa kwenye eneo moja na wakakutana na tukio moja, lakini matokeo yakawa tofauti kwa watu hao.
Kujikumbusha kwamba kilichopo sasa hakitakuja kutokea tena, hasa kwa namna kilivyo sasa ni kitu kinachotuondoa kwenye kubweteka na kukata tamaa. Na hilo ndiyo muhimu sana kwenye kujenga mafanikio makubwa tunayoyataka na kuweza kudumu nayo.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK145; Usijisahau Sana, Hili Halitakuja Kutokea Tena