Habari za leo rafiki yangu?

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio ambayo tunatarajia. Changamoto ni sehemu ya safari ya mafanikio, hivyo uwezo wetu wa kuzitatua ndiyo utatusaidia kufanikiwa.Kwenye makala ya leo nitakwenda kukushauri jinsi ya kutumia mtandao wa intaneti katika kutafuta masoko ya bidhaa au huduma unazouza. Hii ni njia bora kabisa ambayo kila mmoja wetu anaweza kuitumia na haihitaji gharama kubwa kuitumia.

Kabla hatujaangalia hatua zipi uchukue, kwanza tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili.

Tatizo ni upatikanaji wa masoko ya bidhaa na hiyo blog unayotangaza naona itanisaidia sana ila gharama zako ni kubwa mno kwa start up – Catherine

Masoko ni eneo muhimu sana la biashara yoyote ile. Masoko ndiyo yanapelekea mauzo kufanyika na mauzo ndiyo yanaiwezesha biashara kuendelea kuwepo, kwa kukua zaidi. 

Bila mauzo hakuna biashara na bila masoko hakuna mauzo. Kwa maana hiyo basi, tunaweza kusema bila masoko hakuna biashara.

Kama watu hawajui upo na unatoa huduma au bidhaa wanayohitaji, hutaweza kuuza na hivyo huwezi kuwa na biashara. Ndiyo maana masoko ni muhimu sana.

Kwa umuhimu huu wa masoko, ingepaswa kila mfanyabiashara kutenga muda wa kutosha kujifunza vizuri eneo hilo na kulifanyia kazi, lakini wengi wamekuwa hawafanyi hivyo. 

Badala yake wanaendesha biashara kwa mazoea, kitu ambacho kinawagharimu sana.

Kwenye ushauri wa leo, naenda kuwashirikisha jinsi ya kutumia mtandao wa intaneti katika kutafuta masoko ya biashara yako, kwa gharama ambazo ni nafuu sana ukilinganisha na biashara yako.

Kama alivyotuandikia msomaji mwenzetu Catherine, kwamba changamoto ni masoko na gharama za kuweza kuwa na blog, nitakwenda kuyajibu na kushauri vizuri yote mawili, ili kila mtu aweze kuchukua hatua leo hii.

Zama zimebadilika.

Zamani ilikuwa ukitaka kutangaza biashara yako, basi inabidi utumie redio, tv, gazeti au kuwa na mabango kwenye maeneo yenye watu wengi. Njia hizo za kutangaza zina gharama kubwa sana na wengi hawawezi kulingana na uchanga wa biashara zao.

Lakini sasa hivi zama imebadilika, ukuaji wa mtandao wa intaneti ambao unakwenda kwa kasi, umefungua njia mpya ya kutangaza biashara. Sasa hivi watu wengi sana wanatumia mtandao wa intaneti, hasa mitandao ya kijamii, hivyo kupitia njia hii, unaweza kuwafikia watu wengi sana.

Kupitia mtandao wa intaneti unaweza kuwafikia wateja wengi, na kwa gharama kidogo sana. Pia mtandao huu wa intaneti umewezesha biashara kuweza kufanyika hata na watu ambao ni wa mbali na hamjuani. Ukishakuwa na njia sahihi ya kuaminika, unaweza kufanya biashara na watu wengi.

Njia ambayo siyo sahihi ya kutumia mtandao wa intaneti kupata masoko.

Watu wengi wanapenda kufanya vitu rahisi, wanapenda kuweka juhudi kidogo wapate matokeo makubwa. Wanapenda wafanye kitu leo na kesho waone matokeo makubwa. 

Hawapo tayari kuweka juhudi kubwa na kuwa na subira kuweza kukuza biashara zao.

Kwa sababu hizi, wanatafuta njia rahisi ya kutumia mtandao wa intaneti kutangaza biashara zao. Tatizo linakuja kwamba njia hizo hazileti matokeo mazuri kama ambavyo walikuwa wanategemea. Hivyo wanaona kama mtandao wa intaneti hauwezi kuwasaidia.

Kwa mfano, watu wengi wamekuwa wanatangaza biashara zao kwenye mitandao ya kijamii kwa kuweka picha nyingi za bidhaa au huduma zao. kila baada ya dakika au masaa kadhaa wanatuma picha nyingine. Kila muda wanachofanya ni kuwaambia watu nauza hichi, nunua hichi…. Wanasahau kwamba kilichowapeleka watu kwenye mtandao siyo kununua, bali kupiga soga, kujifunza, kuona mambo gani yanaendelea. Sasa unapowapigia watu kelele kwamba nunua hichi, nunua hichi, wanajifunza kukupuuza na wakiona chochote unachoweka, wanaachana nacho. Kwa sababu wanajua wewe unataka kuwauzia tu.

Njia sahihi ya kutafuta masoko kwa kutumia mtandao wa intaneti.

Kwanza kabisa siyo njia rahisi, na majibu yake siyo ya hapo kwa hapo. Ila ni njia inayofanya kazi, na baada ya muda, matokeo yanakuwa makubwa kuliko juhudi unazoweka.

Nia hii ni kuwafundisha watu, kuwashauri na kupiga nao hadithi. Kujali yale mambo ambayo wao wanajali. Kuwasaidia kutatua changamoto ambazo wanakutana nazo, ambazo zinaendana na ile biashara ambayo unaifanya. Kwa njia hii wafuatiliaji wako kwenye mitandao hii wanakuamini, wanajenga imani kubwa kwako, wanapata hisia kwamba upo kwa ajili yao ni siyo tu kuwauzia. Sasa wanapokuwa na shida zaidi, watahitaji uwasaidie kutatua, na hapo ndipo unawauzia. Wakifika hatua hiyo, wala hutahitaji kutumia nguvu nyingi, utawaeleza bidhaa uliyonayo ambayo inaweza kuwasaidia, na kwa kuwa tayari wanakuamini, watanunua bila ya kusita.

Hii ni njia ambayo inakupasa wewe kuijua vizuri biashara yako na kuwajua vizuri wateja ambao unawalenga kwenye biashara yako. Unahitaji kuwa na malengo ya muda mrefu na kuwa na uvumilivu. Unahitaji kuwatumia wafuasi wako kwenye mitandao ya kijamii kuwa mabalozi wako.

Kuhusu gharama za kuweza kutafuta masoko kwenye mtandao wa intaneti.

Gharama ni sifuri kabisa, yaani unaweza usitoe hata mia moja, bali tu ile gharama yako ya kuingia kwenye mtandao. Hivyo ukaweka juhudi kubwa na kuanza kupata matokeo madogo na kuendelea kukua.

Lakini ili usitumie gharama yoyote, lazima uweke muda wa kujifunza vitu vingi kwa muda mfupi, na pia uweze kutumia nguvu zako kusambaza maarifa unayoyatoa kuhusu biashara unayofanya.

Hivyo unahitaji ujifunze jinsi ya kutengeneza blog yako mwenyewe, jinsi ya kuiunganisha kwenye mitandao ya kijamii, na kujifunza jinsi ya kupata wasomaji wengi zaidi kwenye blog yako. Pia unapaswa ujifunze jinsi ya kuwageuza wasomaji wako wa kawaida kuwa wanunuaji wa huduma zako mbalimbali, huku wao wakifurahia kufanya hivyo.

Yote haya unaweza kujifunza bure kabisa, ukishakuwa tu na ‘bando’. Unaweza kuingia kwenye mtandao wa google na kutafuta kila kitu, kinapatikana kwa urahisi sana. pia ukiona huelewi vizuri, unaingia kwenye mtandao wa youtube, unatafuta kile unachotaka kujifunza, hapo utaona kwa maelekezo ya video kabisa.

Kama huwezi hayo, ndiyo sasa utahitaji kumlipa mtu akusaidie, ambaye anajua namna ya kuyafanya.

Kwa mfano, kupitia mimi unaweza kulipa tsh elfu kumi, ukapata kitabu kinachoitwa JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, kupitia kitabu hichi utaweza kujifunza mwenyewe hayo yote na kufanya, au ukalipia tsh elfu 30 nikakuandalia blog ya mtaalamu ambayo unaweza kuitumia vizuri, au ukalipia laki tatu na nikakuandalia blog kamili ambayo unaweza kuitumia kwa nafasi kubwa zaidi.

Kwa vyovyote vile, chagua pale unapoweza kuanzia, kama ni bure wewe mwenyewe au kwa kulipa gharama, muhimu ni uanze.

Mfano halisi wa jinsi unaweza kutumia mtandao kupata masoko ya biashara yako.

Watu wengi, hasa ambao wamekuwa wanafanya biashara za bidhaa za kawaida, wamekuwa wakiona kama mtandao hauwezi kuwa na manufaa kwao.

Hapa nataka nichague mfano wa biashara ya bidhaa za kawaida kabisa, kwa mfano unauza nguo za watoto.

Hapa lazima kwanza ujue wateja wako ni watu wa aina gani. Na hapo ni wazazi, pia katika wazazi, unapaswa kujua wazazi wa kike ndiyo wanafanya manunuzi zaidi ya watoto kuliko wa kiume. Hivyo watu utakaowalenga kwenye mtandao, ni wazazi wa kile, ambao wana watoto wadogo wenye uhitaji wa mavazi.

Sasa ukishajua soko lako ni lipi, jua changamoto ambazo wazazi hao wanakutana nazo kwenye kufanya manunuzi ya mavazi ya watoto wao. Hapo utakutana na changamoto nyingi mno, kuanzia bei za mavazi, ubora wa mavazi, muda wa kuzunguka kutafuta mavazi hayo, na hata changamoto za kipindi cha sikukuu katika kupata mavazi bora kwa gharama nzuri.

Hapa sasa unahitaji kuwa na blogu yako ambayo utakuwa unaandika na kutoa maarifa na ushauri kuhusiana na mavazi ya watoto. Pia unahitaji kurasa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinaendana na jina la blogu yako.

Kupitia blog hii, weka makala na mafunzo mbalimbali kuhusu mavazi ya watoto, ushauri kuhusu changamoto mbalimbali. Weka maarifa ya namna ya kuchagua vizuri, namna ya kujua kipi bora na kipi siyo bora.

Nenda mbali zaidi ukiwashauri wazazi kuhusu usafi wa mavazi hayo, kwa sababu wengine wanaweza kuwa na changamoto ya watoto kuchafua sana na kuharibu mavazi mara kwa mara.

Wakati unawapa maarifa hayo, pia waeleze kuhusu huduma unayotoa, ya mavazi bora ya watoto kwa gharama rafiki. Wape huduma ya kuwafikishia mavazi hayo pale walipo hivyo kuwasaidia wasisumbuke na kuzunguka kwenye maduka au sokoni.

Kama una duka eneo fulani, basi elekeza watu wanafikaje pale, pia elekeza utaratibu wa kuwatumia wale ambao wapo mbali na hawawezi kufika moja kwa moja.
Kazana kuhakikisha watu wanapata maarifa sahihi kuhusiana na mavazi ya watoto, na matatizo yao unayatatua kupitia huduma na bidhaa ulizonazo wewe.

Unavyozidi kukua, unaweza kulipia matangazo kwenye mtandao kama facebook au google, matangazo ambayo utachagua yawafikie watu wa aina gani na waliopo wapi. 

Hivyo kama wewe upo dar es salaam buguruni, unaweza kuchagua tangazo liwafikie watu wa buguruni pekee. Yote hayo yanawezekana kwa popote ulipo.

Naishia hapo kwa leo, lakini nina imani umeipata picha ya hatua zipi za kuchukua. Usikae chini na kujiambia huwezi kupata masoko kwenye mtandao kwa sababu huwezi kumudu gharama. Badala yake chukua hatua na anza kidogo uwezavyo, na kwa hakika utapiga hatua.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog