USHAURI; Njia Bora Ya Kupata Wateja Wengi Wa Kazi Za Ufundi.

Habari rafiki?

Karibu kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto ambapo tunapeana mikakati ya kuweza kuvuka changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio makubwa ambayo tunayatarajia kwenye maisha yetu.

Jambo moja kuhusu changamoto ni kwamba, mara nyingi unapokuwa ndani ya changamoto, hata majibu ya kawaida kabisa unashindwa kuyaona. Changamoto inakumeza kiasi cha kushindwa kuona vitu rahisi kabisa vya kufanya. Hivyo kwenye ushauri kama hivi, tunakumbushana vitu vya msingi kabisa vya kufanya ili kuondokana na changamoto zinazotukabili.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kuangalia changamoto ya kukosa wateja wa kazi za ufundi. Wapo mafundi wengi ambao wanafanya kazi nzuri, lakini wanakosa wateja wa vile wanavyotengeneza. Hili linawakwamisha kufanikiwa, kwa sababu bila ya wateja, biashara yoyote inakufa.

Leo tutaangalia njia bora kabisa ya kupata wateja wa kazi za ufundi. Lakini kabla hatujaingia kwa undani, tupate maoni ya msomaji mwenzetu kwanza.

Mimi ni fundi madirisha na milango ya aluminium nimefungua ofisi sasa changamoto yangu wateja hamna yaani kazi imekua ngumu sielewi nifanyeje ili wateja wapatikane na kukuza kazi yangu – Ahmad A. S.

Kama ambavyo mwenzetu Ahmad alivyotushirikisha hapa, wapo wengine pia ambao wamekwama kama alipokwama yeye. Wana ufundi mzuri lakini wateja hawapatikani.

picha ya ufundi
Picha kwa hisani ya Kagera Aluminium

Hapa nakwenda kukushirikisha mambo matano muhimu ya kufanya ili kupata wateja kwenye kazi zako za ufundi.

  1. Wafuate wateja walipo.

Dunia ya sasa imebadilika, hizi siyo zile zama za wateja kukutafuta wewe upo wapi, bali ni zama za kuwatafuta wateja wako wapi. Hata uwe na ufundi mzuri kiasi gani na ukawa na ofisi nzuri, siyo wateja wote watakaojua ofisi yako au uwepo wako.

Hivyo unahitaji kutoka na kwenda kuwafuata wateja kule walipo. Na kazi za ufundi ni rahisi kuwajua wateja wako wapi. Kwa mfano kama wewe ni fundi madirisha, wateja wako ni watu wenye nyumba. Hivyo popote penye nyumba mpya inayojengwa, panaweza kuwa na mteja wako. Nenda pale na tafuta kuongea na mmiliki wa nyumba au msimamizi mkuu wa mradi huo. Mweleze ufundi ulionao wewe, mweleze unawezaje kumhudumia na kwa kufanya kazi na wewe atanufaika kwa kiasi gani.

Ukichukua hatua hii siyo wote watakukubalia, lakini ukiongea na watu kumi, hutakosa hata mmoja wa kukupa kazi ya kufanya.

Usiendeshe kazi yako kwa mazoea ya kukaa ofisini mpaka mteja aje pale, dunia imeshabadilika, wateja wanafuatwa kule walipo.

Hii inafaa kwa kila aina ya ufundi, kama umeme, kupaua, bomba, rangi na kadhalika.

SOMA; USHAURI; Kama Wateja Hawaji Kwenye Biashara Yako, Wafuate Kule Walipo.

  1. Tembea na udhibitisho wa kazi zako nzuri.

Unapoenda kuongea na wateja wako watarajiwa, kuwaomba wakupe kazi, wanahitaji ushahidi kama kweli unaweza kufanya kazi nzuri kwao. Hapa unahitaji kuwa na kitu cha kuwadhibitishia kwamba unaweza kufanya kazi nzuri.

Hivyo unahitaji kuwa na picha za kazi zako nzuri sana umewahi kufanya. Picha hizi unaweza kuwa umezitoa kabisa na kutengeneza kijitabu cha kazi zako, au unaweza kuwa nazo kwenye simu yako.

Dunia ya sasa imeboreshwa, usitembee bila ya mifano ya kazi zako nzuri. Kuwa na simu nzuri yenye uwezo wa kutunza picha nzuri. Pia ikihitajika zaidi, safisha baadhi ya picha, tengeneza kijitabu cha kazi zako na hizi utawaonesha wateja wako watarajiwa.

  1. Fanya kazi iliyo bora sana, halafu itangaze.

Kwa dunia ya sasa ilivyo, kama hufanyi kazi bora, umechagua kuwafukua wateja wako wewe mwenyewe. Ushindani ni mkali sana, wateja wanachagua mafundi ambao wanaweza kufanya kazi bora kabisa.

Hivyo unahitaji kufanya kazi ambayo ni bora sana. Mara zote jifunze jinsi ya kuboresha kazi zako zaidi. Soma sana kuhusu kazi unazofanya, zijue mbinu mpya za ufanyaji. Weza kuwashauri vizuri wateja wako kulingana na mahitaji yao, na hilo litaongeza thamani kubwa kwenye kazi zako.

SOMA; Hawa Ndio Maadui Makubwa Wa Mafanikio Yako Unaowabeba Sana.

  1. Watumie wateja wako kama sehemu ya kutangaza kazi zako.

Uzuri wa ufundi ni kwamba, kazi huwa zinaonekana, tena kwa wateja wenyewe. Unapofanya kazi ya mteja, kumbuka kwamba mteja ana ndugu, jamaa na marafiki. Iwapo utafanya kazi bora sana, watu hao wataiona na watataka kujua nani kafanya kazi ile. Hapa ndipo unapoweza kuitumia nafasi hiyo vizuri.

Waombe wateja wako wakuunganishe na watu wao wa karibu wenye uhitaji wa huduma unazotoa. Waulize kama yupo ndugu, jamaa au rafiki anayehitaji huduma zako basi amshauri mtu huyo kufanya kazi na wewe.

Pia unaweza kuwa unatoa zawadi kwa wateja ambao wanakuunganisha na wateja wengine. Labda unaweza kuwapa punguzo fulani kwenye kazi nyingine utakayofanya nao.

Wateja ambao wameridhika na kazi yako, ni wateja wazuri sana kwako kuwafikia wateja wengine.

  1. Tumia vizuri mitandao ya kijamii na intaneti.

Unapaswa kuwa kwenye mitandao ya kijamii, na huko jitambulishe kama fundi wa kile unachofanya. unafanya hivyo kwa kuweka picha za kazi zako, na hata kuwashauri watu mambo muhimu kuhusiana na ufundi wako. Tumia mitandao ya kijamii kuwafanya watu wajue uwepo wako na kazi unazofanya. Siyo lazima utangaze kila dakika, lakini isipite siku hujawashirikisha watu kuhusiana na ufundi wako.

fb instagram
Pata kitabu hichi kikusaidie kuweza kutumia mtandao wa intaneti kutangaza kazi zako za ufundi.

Pia tumia mtandao wa intaneti vizuri kutangaza kazi zako. Unaweza kuwa na blog ambayo utaitumia kama kijitabu chako kwa kuweka kazi zako bora za ufundi. Pia unaweza kutumia blogu hiyo kutoa elimu kwa watu kuhusiana na ufundi wako. Elimu ambayo itawasaidia kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Hii itakusaidia kupata wateja wengi kwa njia hiyo ya mitandao ya kijamii na mtandao wa untaneti.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kupata Masoko Ya Biashara Yako Kwenye Intaneti Bila Ya Kutumia Gharama Kubwa.

Nyongeza; acha tabia za kiswahili za mafundi walio wengi.

Mafundi wengi watakulalamikia hakuna kazi lakini sasa mpe kazi, mtaanza kutafutana kila siku na kuishia kugombana. Wapo mafundi ambao wamekuwa na tabia za uongo, au kuahidi mambo ambayo hawana uhakika nayo. Wengine wanachukua kazi nyingi kuliko uwezo wao na wanawachelewesha wateja kwenye mahitaji yao.

Wewe usifanye hivi, kuwa mwaminifu, timiza ahadi unayotoa. Kama kitu huna uhakika nacho, ni bora usiahidi. Mwambie mteja ukweli kama una kazi nyingi na itabidi asubiri, kama mteja anakuamini kweli, atasubiri. Pambana kuhakikisha kwamba unakamilisha kazi kama ulivyopanga, ukikosea mwenyewe kwenye mipango au mahesabu yako, hiyo ni juu yako, usitake kurudi kwa mteja na kuanza kulalamika.

Wateja wa sasa hawataki kabisa usumbufu. Unaweza kuona ameshalipa na hivyo unaweza kufanya utakavyo, lakini jua ukimsumbua hatakuja tena kwako na atawaambia wengine pia wasifanye kazi na wewe. Hivyo humpotezi tu mteja mmoja, bali unapoteza ndugu, jamaa na marafiki zake.

Uaminifu utakusaidia sana kama fundi, utawafanya wateja wawe tayari kufanya kazi na wewe.

Zingatia mambo hayo matano na kwa hakika utaweza kutengeneza wateja wengi wa kazi zako za ufundi. Mambo yote hayo yanahitaji NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA kwa hali ya juu, hivyo fanya huo kuwa msingi mkuu wa kazi zako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: