Pata picha umepanda meli ambayo haina nahodha na imeachiwa iondoke tu, ama nahodha yupo ila hana ramani mtaelekea wapi? Kama mpira wa miguu kusingekuwa na magoli ungechezwaje? Ushindi ungepimwaje? Au pata picha umekwenda msituni kuwinda una silaha za kutosha, je utaanza tu kurusha silaha ovyo imkute mnyama yeyote au utasubiri umwone mnyama ndipo umlenge? Kwa mifano hiyo ya maisha ya kawaida inatuonesha kwamba lazima uwe na lengo ili kupata kitu fulani. Lazima kuwe na magoli ili kupima ushindi, lazima umwone mnyama na kujua umbali wake ili kuweza kumlenga. Hii ina maana kwamba bila ya kuwa na malengo ni vigumu kupata unachotaka, na utajuaje unachotaka bila ya malengo?
  Sio mara ya kwanza kusikia kuhusu malengo, kila mtu anajua kuhusu malengo na wengi wetu tumejiwekea malengo kwenye maisha. Wengi wetu tunafikiri malengo ni kufanikiwa kifedha tu ndio maana ukimuuliza mtu malengo yako baadae ni nini atakwambia kuwa tajiri mkubwa, kuwa rubani, daktari ama mwalimu na mengineyo. Je maisha yako yana vipengele hivyo tu? Tatizo jingine la uwekaji wa malengo ni kwamba watu wengi hawana mipango ya muda mrefu, watu wengi wana mipango ya miaka miwili kushuka chini, ukimuuliza kuhusu miaka mitano, kumi, ishirini ijayo hana.
  Hapa tutaangalia aina za malengo na mpango wa muda wa maisha yako.
1. Malengo ya kiafya.
  Hapa unaweka malengo juu ya afya yako kwa kipindi kirefu. Unataka uishi miaka mingapi? kutokujua tu miaka unayotaka kuishi ni kujipunguzia muda wa kuishi. Namaanisha kwamba kama utapanga kufika miaka mia moja utaijenga afya yako ili kufikia miaka hiyo. Hutokula hovyo, hutokaa kwenye mazingira hatarishi, utajikinga na magonjwa.
2. Malengo ya kitaaluma/utaalamu
  Hapa unajiwekea malengo ya elimu unayotaka kufikia kama unasoma ama utataka kujiendeleza. Na pia utaweka malengo ya kazi unayotaka kufanya, kama uko kazini unakuwa na malengo ya ngazi unayotaka kuwa umefikia miaka kumi, ama ishirini ijayo. Huwezi kufanya kazi kwa kiwango kilekile na ngazi ileile maisha yako yote halafu utegemee kufanikiwa zaidi.
3. Malengo ya kifedha.
  Hapa ndipo wengi wanapoweka malengo ila hawayaweki vizuri. wengi huweka malengo ya kuwa na hela nyingi ama kuwa matajiri lakini hawachambui malengo hayo vizuri. Inabidi uwe na malengo ya lini utastaafu kufanya kazi(hata kama hujaajiriwa), utakuwa na kiwango gani cha fedha cha kukuwezesha kuishi vizuri baada ya kustaafu na pia mali utakazotaka kumiliki kwenye maisha yako.
4. Malengo mahusiano na familia.
  Ni vizuri kuwa na malengo ya mahusiano yako na watu wanaokuzunguka, ndugu jamaa na marafiki. Jua ni watu gani watakuwa marafiki zako wa karibu ambao utashirikishana nao kuhusu maendele yako. Pia ni vizuri kupanga aina ya famili utakayotaka kuwa nayo ili kuweza kuwa na furaha maishani. Hakuna kitu muhimu duniani kama mahusiano na watu wengine na familia yako.
5. Malengo ya kijamii.
  Weka malengo ya jinsi utakavyojihusisha na jamii inayokuzunguka, utanufaiki vipi na pia utainufaisha vipi. unataka kuwa na ushawishi gani katika jamii? unataka kuwa kiongozi wa wananchi? yote hayo lazima uweke kwenye malengo yako ili uweze kujua jinsi ya kuyafikia.
6. Malengo ya maendeleo binafsi na imani.
  Katika maisha ni muhimu kuwa na malengo ya maendeleo binafsi, lazima ukue kila siku kwa kujifunza mambo mapya, kuongeza ujuzi binafsi na pia kukua kiimani. Ni lazima imani yako iwe imara ili usijekuyumbishwa na watu wanaoibuka kila siku na vitu vipya.
  Kwa kifupi hayo ndio maeneo makuu ya kuweka malengo yako ya maisha, unaweza kuwa na mengi zaidi ya hapo ila usiwe na malengo chini ya hapo. Maisha yaliyo na furaha ni maisha yaliyosawa katika nyanja hizo. Utakuwa na maisha gani kama utakuwa tajiri wa kwanza nchini ila huna mahusiano mazuri na familia yako? Watu waliokuzunguka wanaona wewe umewadhulumu na hawataki hata kukuona?
  Unaweza kusema cha msingi ni hela ukishakuwa nazo nyingi kila kitu kitakuwa sawa, usijaribu kucheza hiyo kamari.