Kila mtu anataka kufanikiwa, tunayapima vipi mafanikio ya mtu? Nini hasa maana ya mafanikio? Ili kuweza kupima mafanikio kwanza inabidi tujue maana hasa ya mafanikio. Unaweza fikiri ni swali rahisi kujibu ila inaweza kuwa unavyopima mafanikio sivyo. Kutokujua maana ya mafanikio kunaweza kukufanya ushindwe kujua kama umefanikiwa au la. Kutoka kwenye kamusi mbalimbali mafanikio yanaweza kuwa ya aina nne
1. Kupata hadhi ya kijamii ama kuwa maarufu.
  Watu waliopata hadhi fulani katika jamii kama viongozi wanaonekana wamefanikiwa. Vingozi wa kuchaguliwa ama wakuteuliwa wamefanikiwa kuwa na ushawishi mpaka kufikia kupata nafasi hizo za uongozi.
  Watu maarufu kama wasanii, wanamichezo, matajiri wakubwa nao wanaonekana wamefanikiwa katika jamii.
2. Kufikia malengo uliyojiwekea.
  Kama kuna malengo uliyojiwekea na ukaweza kuyafikia ndani ya muda ulioweka basi umefanikiwa. kwa mfano kama umepanga kusoma kitabu kimoja kila wiki na ukaweza kumaliza kukisoma basi umefanikiwa.
3. Matokeo mazuri ya jambo fulani.
  Kama kuna jambo unafanya na likaleta matokeo mazuri ambayo ulikuwa huyategemei ni mafanikio. Kwa mfano wanasayansi huwa wanafanya majaribio mbalimbali na mengi hutoa majibu mazuri mengine hutoa majibu yasiyotegemewa. Hivyo kama majibu ni mazuri ni mafanikio.
4. Kinyume cha kushindwa.
  Mafanikio pia hupimwa kwa kinyume cha kushindwa. Kwa mfano kwenye mtihani kuna kufaulu na kufeli, waliofaulu wanaonekana wameshinda na waliofeli wanaonekana wameshindwa.
  Katika maana zote hizo za mafanikio, mafanikio yanaanza na wewe binafsi, ina maana ni lazima uweke malengo ya kufanya jambo fulani ama kufikia hadhi fulani ndipo jamii nayo itaanza kukuona umefanikiwa.
Kwa mfano mimi kila siku nafanikiwa kwenye malengo yangu binafsi ninayojiwekea, ila jamii haijui hilo. Siku nitapofikia hadhi fulani labda ya utajiri, ama uongozi basi jamii nzima itakuwa inazungumza kuhusu mimi.
  Mafanikio ya aina yoyote yanakuja kwa malengo na utekelezaji wa malengo. Weka malengo sasa na anza kuyatekeleza mara moja. Maana kuu ya mafanikio ni kufikia malengo uliyojiwekea ndani ya muda uliopanga.