Umewahi kujilinganisha na mtu ama watu wengine? Watu wengi hupenda kujilinganisha na watu wanaowazunguka, yaweza kuwa ndugu, marafiki, wafanyakazi wenza, wanafunzi wenza na kadhalika. Maeneo ambayo watu wengi hutumia kujilinganisha ni mafanikio, elimu, mali, uwezo wa kufanya mambo na hata maisha ya kawaida. Kujilinganisha kunaweza kuwa kuzuri ila mara nyingi ni kubaya, kubaya sana.
   Kujilinganisha kunakuwa kuzuri pale ambapo anaejilinganisha anatamani kumfikia alieko juu. Hivyo kutakufanya ujitahidi sana ili uweze kufika kiwango alichofikia unaejilinganisha nae. Je ukishamfikia na kumpita nini kitatokea? Utaendelea kuweka juhudi zaidi? Ni ngumu sana kuendelea kuweka juhudi na kufikia kiwango cha juu zaidi ya hapo kwa sababu malengo yako yalikuwa kufikia kiwango hicho. Hivyo badala ya kujilinganisha ni bora kuamua kuwa bora kulingana na uwezo wako, kufanya hivi hakutakuwekea mwisho wa kiwango. Ukitaka kuwa bora kwa unalolifanya hutakuwa na mipaka wewe utataka kwenda juu tu na hapo ndipo utaugundua uwezo wako wa kweli.
  Kujilinganisha ni kubaya sana pale anaejilinganisha anapojishusha thamani kutokana na kutokuweza kufikia kiwango alichofikia anaejilinganisha nae. Hii inamfanya mtu kushindwa kujua uwezo wake. Huwezi kufanya kila kitu ila kuna kitu kimoja ama vichache unavyweza kuvifanya kuliko watu wote duniani. Dunia kwa sasa ina watu zaidi ya bilioni saba ila hakuna watu wawili wanaofanana kwa kila kitu duniani. Hii inamaanisha kwamba kila mtu duniani ni wa pekee na anauwezo wa kipekee usioweza kulinganishwa na mtu mwingine yeyote. Hivyo kujaribu kujilinganisha na mtu mwingine ni kuamua kutoutambua uwezo wako.
  Usijitharau kwa sababu kuna vitu wenzako wanaweza kufanya ila wewe huwezi, tafuta uwezo wako uko wapi na hapo ndio upange kuwa bora. Waangalie wengine wanafanya nini ili kujifunza kutoka kwao na kupata moyo kwamba inawezekana kufanyika. Ila usiwatumie wao ama mafanikio yao kama ndio malengo yako, malengo yako yawe ni kuwa bora kwa unachofanya. Una uwezo mkubwa sana ambao huutumii kwa sababu hakuna mwenye uwezo huo, amua mara moja kutaka kuufikia uwezo wako.
  Wewe ni wa pekee duniani, ila upekee wako hautaonekana kwa kujilinganisha na wengine. upekee wako utaonekana pale utakapofanya tofauti na wengine na kufanya tofauti kunatokana na malengo ya kuwa bora. Kama hutaki kuwa wa kawaida, kama unataka kuyafikia malengo yako, na kama unataka kuwa bora kwa unachokifanya ACHA SASA KUJILINGANISHA NA MTU YEYOTE.