Rafiki yangu Mpendwa,

Leo tarehe 28 mwezi Mei ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwangu. Kila ninapokuwa naendea siku hizi za kumbukizi ya kuzaliwa, huwa natenga muda wa kutafakari kwa kina safari ya maisha yangu hapa duniani. Huwa naangalia kule nilikotoka, pale nilipo sasa na kule ninakokwenda. Baada ya kuangalia maeneo hayo kwa kina, huwa nafikia maazimio ambayo nakwenda kuyatekeleza kwa kipindi kinachofuata.

Awamu hii nimepata muda wa kufanya zoezi hilo, ambapo niliangalia zaidi mambo yote ambayo nimewahi kufanya na yapi yaliyonipa matokeo na ambayo hayakunipa matokeo. Nimeangalia kwa kina sana, kwangu mwenyewe na kupitia hadithi za watu wote waliofanikiwa ili kuona ni kitu gani ambacho hakikosekani kwenye mafanikio yoyote yale.

Baada ya tafakari ya kina, imenijia wazi kwamba mafanikio ni matokeo ya kurudia rudia mambo yanayochosha bila kuchoka. Hicho ni kitu kinachoweza kuonekana ni kidogo na rahisi, lakini kina uzito mkubwa sana kwenye safari ya mafanikio makubwa kwenye maisha.

Nimejaribu kuangalia kwangu mwenyewe, kwa vitu vyote ambavyo nimewahi kufanya, vilivyonipa matokeo ni vile nilivyorudia rudia kufanya kwa muda mrefu, hata kama ni vidogo sana. Nimeangalia pia kwa watu ambao nimepata bahati ya kujihusisha nao kwa miaka 13 ambayo nimekuwa kwenye hii tasnia ya kuandika, kufundisha na kukochi. Nimeona watu wanaokimbizana na mambo mapya kila wakati na jinsi wanavyoshindwa vibaya, huku wale wanaorudia rudia mambo yanayochosha wanavyofanikiwa.

Tafakari yangu imenionyesha jinsi ambavyo adui wa mafanikio yetu binadamu ni sisi wenyewe, hasa hitaji la kukimbizana na vitu vipya kila wakati. Hebu fikiria tu wewe mwenyewe, kuna watu wawili, mmoja anachagua kufanya biashara moja kwa miaka 10 bila kuhangaika, huku mwingine akibadili biashara kila fursa mpya inapojitokeza na kujikuta amefanya biashara 5 ndani ya miaka 10. Unadhani ni nani atakayekuwa amepiga hatua kubwa? Ni wazi kabisa yule aliyeweka muda mrefu kwenye biashara moja, atakuwa na matokeo makubwa kuliko anayehangaika na biashara mpya kila wakati.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye maeneo yote ya maisha, kuanzia mafanikio kwa ujumla, yaani kujenga tabia na nidhamu ya mafanikio, fedha, kujenga utajiri na uhuru wa kifedha na biashara ambapo ni kujenga biashara inayojiendesha bila kukutegemea. Sijaona kitu kimoja kinachowatofautisha watu kama uwezo wa kufanya mambo yanayochosha (‘kuboa’), kwa muda mrefu bila kuchoka (‘kuboreka’).

Baada ya tafakari hiyo ya kina, nimefikia maazimio ambayo yatakwenda kuweka nguvu kubwa kwenye kurudia rudia kufanya mambo yanayochosha bila kuchosha. Siyo mambo mapya kabisa ambayo sijawahi kuyafanya, bali ni kuhakikisha nayafanya mambo hayo kwa msimamo mkali zaidi.

Mambo hayo niliyochagua kuyafanya kwa kurudia rudia bila kuchoka nimeyaita MAKIRITA 10 X 10 KILA SIKU.

Hayo ni mambo 10, ambayo nitayafanya kwa kipimo cha 10 kila siku bila kuacha. Na siyo tu kujiambia nitafanya, bali kuwa na ushahidi wa kuyafanya kweli na kutuma ushahidi huo kwenye kundi la JUMUIA YA WASHIRIKA WA MAFANIKIO. Hilo ni eneo ambalo pia unapaswa kuwepo ili uweze kushirikiana na watu sahihi kwenye safari yako ya mafanikio.

Mambo hayo 10 niliyoazimiakufanya kwa kurudia rudia kila siku bila kuchoka ni kama ifiatavyo;

1. KUSOMA KURASA 10+

Kitu kimoja ambacho kimenipa mafanikio makubwa sana kwenye maisha yangu ni usomaji wa vitabu. Nimesoma na kusikiliza maelfu ya vitabu tangu nimeanza safari hii ya mafanikio. Nimekuwa nikisoma wastani wa vitabu 2 kila wiki, ambapo inakuwa vitabu 100 kila mwaka.

Usomaji umekuwa ndiyo nguzo ya mambo yote ambayo nimeweza kufanya. Vitabu vyote nilivyoandika, programu zote nilizoanzisha na mengine mengi, yameanza na usomaji.

Bado sehemu kubwa ya kila siku yangu inachukuliwa na usomaji, japo siyo wa vitabu pekee, bali wa vitu mbalimbali.

Katika kuhakikisha nabaki kwenye misingi sahihi, nimeazimia kusoma angalau kurasa 10 za kitabu kilichochapwa kila siku. Zingatia hapo ni kitabu kilichochapwa (hardcopy), ndipo penye uzito mkubwa.

Nitaendelea kusoma vitabu vya nakala yeye, kulingana na hitaji ninalokuwa nalo kwa wakati. Lakini kila wakati nitapaswa kuwa na nakala ngumu ya kitabu ambayo nasoma kurasa zisizopungua 10.

Ushahidi wa hili ni kurasa 10 + nilizosoma kwenye kitabu ninachokuwa nasoma.

2. KUANDIKA MANENO 1000+

Kitu cha pili ambacho kimenipa mafanikio makubwa kwenye maisha yangu ni uandishi. Kwa kipindi cha miaka 10, nimeweza kuandika vitabu zaidi ya 30. Hivyo ni vitabu ambavyo vimeenda kwa kina kabisa kwenye eneo la mafanikio, fedha na biashara. Uandishi ndiyo umezalisha programu zote ambazo nimekuwa nazifanya.

Maendeleo ya teknolojia na ujio wa zana mpya kama akili mnemba (AI) imeonekana kuwa nyenzo ya kusaidia sana kwenye uandishi. Na siku za karibuni nimejikuta natumia nyenzo hizo kurahisisha uandishi wangu. Lakini baada ya kutafakari kwa kina, nimeona nyenzo hizo zinashusha ubora wa uandishi wako.

Hivyo nimeazimia kuandika maneno yasiyopungua elfu 1 kila siku, bila kutumia nyenzo yoyote kurahisisha uandishi huo. Ni kukaa chini na kuandika kwa kutumia akili yangu, kama ambavyo nimekuwa nafanya kwa miaka yote 13 ambayo nimekuwa kwenye tasnia hii.

Nitaendelea kutumia teknolojia hizi mpya kwenye mambo mengine, lakini inapokuja kwenye uandishi, nitaandika kwa akili yangu mwenyewe na vidole vyangu mwenyewe.

Ushahidi wa hili ni idadi ya maneno niliyoandika kila siku, ambayo ndiyo yatakuwa BARUA ZA KOCHA. Hakikisha unapata nafasi ya kusoma barua hizo kila siku.

3. KUREKODI SAUTI DAKIKA 10+

Tangu mwaka 2016 nimekuwa napanga kuwa na vipindi vya sauti na video ili kufikisha mafunzo yangu kwa wengi zaidi na kwa mifumo tofauti na maandishi. Lakini nimekuwa sipati msimamo mzuri kwenye kufanya hayo. Hiyo ni kwa sababu kurekodi sauti na video kunahusisha watu wengine, na kitu kikishategemea watu wengine, nafasi za kukwama ni nyingi.

Nimekuwa sikwami kwenye kuandika kwa sababu sitegemei mtu mwingine yeyote isipokuwa mimi mwenyewe. Ili nisikwame kwenye njia hizo nyingine za kutoa mafunzo, nimeazimia kurekodi dakika 10+ za sauti kila siku. Nimeandaa vifaa vya msingi, simu na maiki ili kuhakikisha zoezi hilo naweza kulikamilisha mwenyewe bila kutegemea mtu yeyote.

Ushahidi wa hili ni vipindi vitakavyoenda hewani kila siku kwenye majukwaa ya podcast, ambavyo nitakuwa nashirikisha.

4. KUTEMBEA HATUA 10,000+

Afya ndiyo mtaji namba moja kwenye maisha na safari ya mafanikio. Na mazoezi ni moja ya vitu muhimu kwenye kujenga afya imara.

Kutokana na kutingwa na mambo mengi ya kufanya kwenye hii safari, mazoezi ni kitu kingine ambacho nimekuwa sikifanyi kwa msimamo. Nimekuwa naweka programu mbalimbali za mafanikio, lakini zimekuwa hazidumu kwa muda mrefu, kwa sababu zinaingiliwa na majukumu mengine ninayokuwa nayo.

Sasa nimeazimia kufanya mazoezi ya msingi kabisa kila siku, ambayo ni kutembea hatua zisizopungua elfu 10 kila siku. Kuna aina nyingi za mazoezi, lakini mazoezi ya kutembea ndiyo ambayo nimeona yatanifaa zaidi, kwa sababu pia nayafanya pamoja na vitu vingine. Wakati wa mazoezi hayo ya kutembea pia nakuwa nasikiliza vitabu vilivyosomwa (audio books) au vipindi vya mahojiano (podcasts). Lakini pia nimegundua ni muda wangu mzuri wa kutafakari kwa kina mambo yote ninayofanya.

Zoezi hili la kutembea ninalifanya kwenye mashine na kuhesabu hatua kwa kutumia app za simu. Hivyo ushahidi ni hatua zilizosomeka kwenye app inayopima utembeaji.

5. KUFANYA KAZI KWA KINA (DEEP WORK) MASAA 10+

Kabla ya rafiki yangu wewe, yupo rafiki aliyetuleta mimi na wewe pamoja. Rafiki ambaye huwa namheshimu na kumpenda mno. Rafiki huyo ni kazi. Nimefika hapa nilipofika siyo kwa sababu ya bahati, upendeleo au kingine chochote. Bali ni kwa kuweka kazi kwa juhudi kubwa sana.

Nimeazimia kuliendeleza hilo, kwa kuhakikisha napata masaa yasiyopungua 10 ya kufanya kazi kwa kina kila siku. Ninaposema kazi kwa kina maana yake ni muda ninaotenga kwa ajili ya jukumu la kazi nautumia kwa jukumu hiyo tu. Siyo kuhangaika na usumbufu wakati kuna majukumu ya kazi yaliyo mbele yangu.

Majukumu yangu ya kazi yanarudi kwenye mambo machache ya msingi, ambayo ni Kusoma, Kuandika, Kufundisha na Kukochi. Hayo ndiyo ninayoyapa muda wa kufanya kwa kina kila siku, kwa sababu ndiyo yanayonisogeza mbele zaidi.

Ushahidi wa hili ni ratiba yangu ya kazi ya kila siku na app ya kwenye simu ya kupima muda wa kazi kwa kina.

6. KUTANGAZA KWA DOLA 10+

Hii tafakari ya kumbukizi ya mwaka huu imekutana na taarifa za kifo cha aliyekuwa mwanzilishi washirika la habari la CNN, Ted Turner. Kuna kauli yake maarufu ambayo imekuwa inashirikishwa sana kipindi hiki. Alinukuliwa akisema; ‘early to bed, early to raise, work like hell and advertise’. Ikimaanisha; ‘lala mapema, amka mapema, fanya kazi kwa juhudi sana na tangaza.’

Nimeichukua kauli hiyo kama sehemu ya mambo yanayoniongoza na ndiyo maana nimeazimia kulipia matangazo kwa angalau dola 10 kila siku. Huwa natangaza mara kwa mara na kwa viwango vikubwa kuliko hicho. Lakini siyo kitu ambacho nimewahi kufanya kila siku kwa msimamo bila kuacha.

Hivyo nimeandaa programu maalumu ya vitu ambavyo nitakuwa navitangaza kila siku kwa kutumia kiasi hicho. Matangazo mengine ya biashara na huduma tunazotoa yataendelea kulingana na mipango iliyopo. Hili la kufanya kila siku kwa kiwango hicho ni kwa programu maalumu.

Ushahidi wa hili ni tangazo lililolipiwa la huduma maalumu na kiasi kilichotumika kwenye tangazo hilo kila siku.

7. KUONGEA NA WATU 10+

Kazi yangu kubwa ni watu, kuanzia kwenye uandishi ninaofanya, mafunzo ninayotoa na ukocha ninaofanya. Hivyo kila siku nimekuwa najihusisha na watu mbalimbali.

Katika tafakari niliyofanya, nimeazimia kila siku kuongea na watu wasiopungua 10. Hawa ni watu tofauti na wale ambao tayari najihusisha nao mara kwa mara. Lengo la azimio hili ni kujisukuma kuwafikia watu wengi wapya na ambao wataipeleka huduma ninayofanya mbali zaidi.

Ushahidi wa hili utakuwa mazungumzo niliyofanya na watu, kwa njia ya simu au ana kwa ana.

8. KUWEKEZA TSH 10,000+

Kama kuna kitu kimoja ambacho kimeweza kuyabadili kabisa maisha yangu, basi ni uwekezaji. Uwekezaji ndiyo ulionipa nguvu ya kuacha kazi ya udaktari na kuingia moja kwa moja kwenye hii tasnia ya kuandika, kufundisha na kukochi.

Nimekuwa nafanya uwekezaji kwa viwango mbalimbali, hasa kwa kutumia kanuni ya sehemu ya kila kipato ninachoingiza. Kwenye tafakari niliyofanya nimeazimia kujisukuma kuwekeza kila siku, kwa angalau shilingi elfu 10. Na ili kutimiza hilo nimechagua mfumo rahisi wa uwekezaji, ambao ni rahisi kuwekeza kila siku na pia kuona thamani ya uwekezaji huo kwa urahisi.

Uwekezaji mwingine wa kiwango kikubwa ambao nimekuwa nafanya utaendelea bila kuathiriwa na programu hii mpya ya uwekezaji mdogo mdogo wa kila siku.

Ushahidi wa hili ni ujumbe wa muamala wa uwekezaji ninaofanya kila siku.

9. KUWEKA AKIBA DOLA 10+

Akiba ni eneo jingine la kifedha ambalo limeniletea matokeo makubwa, lakini nimekuwa naifanya akiba kama uwekezaji. Ambacho nimekuwa nafanya ni kuwa na mifuko mbalimbali ya uwekezaji. Kuna ambayo nimeifanya uwekezaji wa muda mrefu na ambayo nimeifanya akiba, ninapokuwa nakusanya kiasi fulani kwa lengo nililonalo au kwa ajili ya dharura.

Kwa muda nimekuwa napanga kuwa naweka akiba kwa mfumo wa dola badala ya shilingi na kwenye akaunti ya benki badala ya mifuko ya uwekezaji. Nimefungua mpaka akaunti ya dola kwa zaidi ya mwaka, lakini nilikuwa sijaweka akiba hiyo kwa msimamo.

Kwenye tafakari niliyofanya nimeazimia kuweka akiba ya angalau dola 10 kila siku. Akiba hii naiweka kwenye akaunti ya benki ya dola.

Ushahidi wa hili itakuwa ujumbe wa miamala ya benki. Kwa sababu akaunti ya dola inahusisha kwenda benki na kubadilisha fedha shilingi kuwa dola ndiyo kuweka, ushahidi hautawezekana kupatikana kila siku. Ila utapatikana kwa wiki au mwezi. Ambacho nitahakikisha ni kila mwezi nimeweka akiba ya dola isiyopungua dola 300.

10. KUISHI KWA KINA (DEEP LIFE) MASAA 10+

Nimeamini na kuishi kwa kufanya kazi kwa kina, kitu ambacho mara nyingi kimenifanya nisahau kuishi. Ndiyo, nakuambia hilo wazi kabisa, nimekuwa nasahau kuishi. Huko nyuma nilianza kwa kujaribu kutafuta mlinganyo wa maisha na kazi (work life balance), lakini nikaja kugundua ni kitu kisichowezekana, hasa pale unapokuwa unajenga misingi.

Nakiri wazi kwamba maisha yangu yote yamekuwa ni kazi. Kutumia masaa 16 mpaka 18 kwa kazi kila siku imekuwa ni kitu cha kawaida. Na hilo ndiyo limeweza kunifikisha hapa nilipo. Lakini sasa umri unakwenda na mifumo mingi nimeshaijenga.

Tafakari niliyofanya, nimeazimia kuishi kwa kina kwa angalau masaa 10 kwa siku. Na kuishi kwa kina kunajumuisha mambo mengi kwa wakati mmoja.

Kitu cha kwanza ni muda wa kulala kwa kina na utulivu, huu hautapungua masaa 6 kwa usiku na muda wa kupumzika mchana.

Kitu cha pili ni muda binafsi wa kutafakari kwa kina mambo mbalimbali, ambao pia utaungana na zoezi la kutembea.

Kitu cha tatu ni muda wa familia, ambapo napata muda tulivu na wa kina wa kuwa na familia bila kuingiliwa na usumbufu wowote.

Kwa kutenga na kulinda muda huo wa kuishi kwa kina, itasaidia kuleta mlinganyo kwenye maisha yangu, hasa baada ya kipindi kirefu cha kukosekana kwa mlinganyo huo.

Ushahidi wa hili ni muda ninaotumia kila siku kuishi kwa kina, kama unavyopimwa na app ya kwenye simu ninayoseti kwa ajili ya hilo.

Rafiki, kama ambavyo umeona hapo, mambo hayo kumi siyo ugunduzi mpya, wala siyo mambo ya kishujaa. Bali ni mambo ya kawaida kabisa na yanayoweza kuchosha. Jambo la msingi ni mimi kuyafanya kila siku bila kuacha.

Na ninaposema kila siku ni siku nilizotenga kwa ajili ya kazi, ambazo ni jumatatu mpaka jumamosi. Siku ya jumapili nimeitoa kabisa kwenye kazi na kuifanya kuwa siku binafsi na familia.

Kupitia kundi la JUMUIA YA WASHIRIKA WA MAFANIKIO nitakuwa nashirikisha ushahidi wa mambo hayo ninayotekeleza kila siku.

Nikualike na wewe ushirikishe mambo unayojisukuma kufanya kila siku na kutuma ushahidi wake. Siyo lazima yawe 10 kama yangu na wala siyo lazima yawe kwa vipimo kama vyangu. Chagua mambo ambayo ukiyafanya kila siku, hata kama ni kwa udogo, yatakufikisha kwenye mafanikio unayotaka. Kisha chagua kipimo kidogo ambacho hakiwezi kukushinda kabisa kila siku na ukazane kutimiza kila siku.

Nikukaribishe sana rafiki yangu kwenye kushirikiana pamoja kwenye safari hii ya mafanikio. Kama bado hujaingia kwenye JUMUIA YA WASHIRIKA WA MAFANIKIO, fanya hivyo sasa kwa kuwasiliana na namba 0717101505.

Kocha