Sikiliza hapa;

Tahadhari; Kama umekuwa unapata fikra za kujiua, pata msaada wa wataalamu wa afya ya akili kabla ya kuendelea kusoma barua hii.

Rafiki yangu mpendwa,

Barua ya leo imeanza na tahadhari, kwa sababu ninayokwenda kukushirikisha hapa ni ya kina sana na yanataka utimamu wako. Kama ambavyo chanjo huwa haitolewi kwa watu ambao tayari wameshapata ugonjwa, kama umeshafika hatua ya kuona hakuna tena haja ya kuendelea kuishi, pata tiba sahihi kwanza.

Kama uko sawa kwenye afya ya akili, karibu usome barua hii ambayo itakushtua kidogo, lakini mwisho itakuweka sawa na kuhakikisha unaishi maisha yenye maana kubwa kwako na kwa wengine.

Rafiki, kila siku unalalamika mambo ni magumu, changamoto ni nyingi, vikwazo vya kila aina. Una mengi sana ambayo yamekukwamisha kupata mafanikio ambayo unayataka. Na huenda kuna mengi umekata tamaa na kuacha kabisa kuyafanya. Mawazo mazuri ya biashara na maendeleo uliyokuwa nayo umeachana nayo kwa sababu ya kushindwa au kukataliwa na wengine.

Pamoja na hayo yote rafiki yangu, kuna kitu kimoja kinanishangaza kuhusu wewe. Unajua kabisa mwisho wa matatizo yako yote ni kifo, nini kimekufanya mpaka sasa hujachukua hatua hiyo? Ndiyo, nakuuliza kwa nini mpaka sasa hujajiua ili iwe mwisho wa hayo matatizo yote yanayokusumbua?

Rafiki, naomba ujibu swali hilo kwa umakini mkubwa, kwa sababu ndiyo somo lenyewe ninalotaka utoke nalo hapa. Kwa swali hilo siyo kwamba nakuambia ujiue kama njia ya kutatua shida zako. Bali najaribu kukuonyesha pamoja na yote unayopitia, pamoja na hayo maisha yako kuona yana magumu mengi, bado umeona yana thamani kuyaishi.

Na ndiyo maana nakupongeza sana, kwa sababu umeweza kuiona thamani ya maisha yako na ukayatunza mpaka sasa. Kwenye barua hii nataka nikusaidie uongeze kitu kidogo sana kitakachokuwezesha kufanya makubwa licha ya magumu unayokabiliana nayo.

Huwezi Kupoteza Chenye Thamani.

Huwa kuna kichekesho cha mtu aliyekuwa anapanda juu ya mti kwa ajili ya kujinyonga, lakini wakati anapanda akakutana na nyoka, akashuka na kuanza kukimbia.

Kama kweli mtu anataka kufa, kwa nini akimbie nyoka au hatari yoyote? Unapoona unaenda hatua za ziada ili kulinda kitu, maana yake kina thamani kwako. Wakati mwingine unaweza kuwa bado hujaijua thamani hiyo, ila unajua ipo na haupo tayari kuipoteza.

Ni sawa na mtu mwenye ardhi pembeni ya barabara, anakuwa hana haraka ya kuiuza wakati ambapo eneo halijawa na thamani. Ila anajua huko mbele thamani itakuja kuwa kubwa.

Ndivyo wengi tunavyoendesha maisha bila hata ya kujua. Tunakuwa hatujaona thamani ya maisha yetu, lakini pia hatuyakatishi, kwa sababu tunajua huko mbele mambo yanaweza kubadilika.

Na nikupongeze sana kuwa hai mpaka sasa, ina maana kubwa sana, kwa sababu kuna mengi yaliyopo ndani yako ambayo dunia bado haijapata nafasi ya kuyaona.

Sababu Ya Kuishi Ndiyo Yenye Nguvu Ya Kukuweka Hai.

Viktor Frankl, alikuwa daktari wa magonjwa ya akili, aliyekamatwa na kufungwa kwenye makambi ya mateso wakati wa vita ya pili ya dunia. Aliingia kwenye kadhia hiyo akiwa na uelewa mkubwa wa saikolojia ya binadamu na magonjwa ya akili.

Nadharia nyingi alizokuwa amejifunza, alizona kwenye uhalisia wake wakati wa mateso aliyopitia. Kwenye kitabu chake cha Man’s Search For Meaning, alieleza mengi kwenye safari hiyo.

Lakini kitu kimoja kikubwa ambacho alisisitiza ni hiki; “Maisha hayafanywi kuwa magumu na yasiyovumilika kwa hali zinazotuzunguka, bali kwa ukosefu wa maana na kusudi.” Kwa hali ngumu sana aliyopitia na wengi aliowaona, aliona jinsi ambavyo wale waliokosa maana ya maisha walivyoyapoteza haraka.

Hili linatupa funzo kubwa sana, kwamba namna pekee ya kukabiliana na ugumu na changamoto za maisha siyo kuyakatisha, bali kujua maana na kusudi la maisha. Kwa kifupi unapaswa kujua uko hapa duniani kufanya nini na maisha yako yana maana gani ndiyo uweze kuvuka magumu unayokutana nayo.

Ili kuhakikisha huendelei tu kuishi kusogeza siku, na magumu unayokutana nayo hayakukwamishi, barua hii ina misingi muhimu kwetu kuelewa kuhusu maana na kusudi la maisha. Wajibu wetu ni kuhakikisha hatuendelei tu kuishi kusogeza siku, bali tunaishi kwa kutoa thamani, kwetu na kwa wengine.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha mambo matano ya kuelewa na kufanyia kazi ili uweze kujua maana na kusudi la maisha yako. Ni kupitia kujua hayo ndiyo unaweza kujenga mafanikio makubwa na yanayodumu.

Karibu usome barua hiyo hapa; #BZK047; Kwa Nini Mpaka Sasa Hujajiua Na Kumaliza Shida Zako Zote?

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.