Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kitu kimoja ambacho nimekuwa nakiamini na kuendelea kukushawishi wewe rafiki yangu ukiamini ni mafanikio yetu yanaamuliwa na sisi wenyewe. Pale tulipo sasa ni sisi tumechagua kuwa hapo. Na kama hapaturidhishi, hatuna yeyote tunayeweza kumlaumu isipokuwa sisi wenyewe.

Najua msimamo huo ni mgumu na unaoweza kupingwa na wengi, tena wakiwa na ushahidi wa jinsi mazingira na hali walizopitia zilivyowakwamisha. Lakini kwa kila unachodhani kimekukwamisha, kuna wengine wamepitia katika hali ngumu kuliko wewe na wameweza kupiga hatua kubwa kuliko ulizopiga.

Hatuwezi kukataa uwepo wa vikwazo na changamoto kwenye safari ya mafanikio. Lakini hivyo siyo vinavyoamua kama utapata mafanikio au la. Maamuzi ya mafanikio yapo kwako na jinsi unavyopambana mpaka kupata kile hasa unachotaka.

Moja ya visingizio ambavyo wengi wanaoshindwa wanakuwa navyo ni kukosa rasilimali muhimu walizohitaji ili wafanikiwe. Mtaji ni namba moja, kila ambaye hana biashara au biashara yake siyo kubwa atakuambia amekosa mtaji. Licha ya sababu hiyo kuwepo kwa muda mrefu, bado mtu anashindwa kuitatua.

Kukosa muda, elimu, uzoefu na hata watu ni sababu nyingine ambazo watu wamekuwa wanazitumia. Na kwa haraka haraka, ukiwasikiliza watu wanavyoeleza rasilimali walizokosa na jinsi hilo lilivyowakwamisha, unaweza kuwaamini.

Ni mpaka pale unapopata nafasi ya kuyachunguza maisha yao kwa kina ndiyo unagundua wanachotoa ni kisingizio tu na hakina ukweli wowote. Wanasema wamekosa rasilimali, lakini kiuhalisia rasilimali hizo wanakuwa nazo za kutosha, na mbaya zaidi wanakuwa wameamua kuzipoteza.

Vipi kama nikikuambia kwa miaka yako yote umekuwa unapoteza muda, fedha, nguvu, umakini na hata fedha? Unaweza kudhani nakutania, lakini kwenye barua hii utaenda kujionea wewe mwenyewe jinsi ‘unavyozingua’ kwenye matumizi ya rasilimali ulizonazo.

Lengo la barua hii, kama ilivyo kwa nyingine ninazokuandikia ni kukuonyesha ukweli ambao kwa muda mrefu umekuwa huuangalii. Unafanya nini na ukweli huo itabaki kuwa wajibu wako. Lakini hapa utatoka na kila unachopaswa kufanya ili kutumia vizuri rasilimali zote ulizonazo kufanikiwa.

1. Una Muda Mwingi Mpaka Umeamua Kuupoteza.

Huwa tunadhani tatizo la muda ni la zama hizi, hasa kwa teknolojia mpya tulizonazo na zinachukua muda wetu mwingi. Lakini ni tatizo ambalo limekuwepo tangu kuwepo kwa binadamu hapa duniani.

Miaka zaidi ya elfu 2 iliyopita, mwanafalsafa wa Ustoa alikuwa na mambo mazito sana ya kuandika kuhusu muda. Alisema; “Siyo kwamba tuna muda mfupi wa kuishi, bali tunapoteza muda mwingi. Maisha yana urefu wa kutosha na tumepewa muda mwingi kwa ajili ya kufanya makubwa kama tukiweza kuutumia vizuri. Ni pale tunapotumia muda kwenye mambo ya tija ndiyo tunakuja kushtuka tunakufa kabla hata hatujaishi.”

Kwa msisitizo zaidi akasema; “Kwa hiyo: hatujapewa maisha mafupi, bali tunayafupisha, na hatujapunjwa muda, bali tunaupoteza ….. Maisha ni marefu kama unajua jinsi ya kuyatumia.”

Halafu kuna wewe sasa, ambaye unasema sababu ya wewe kushindwa kufanya makubwa ni kwa sababu huna muda. Hebu rudia hilo kwa herufi kubwa; ‘SINA MUDA.’ Naamini hata kutamka tu hilo imekusuta, kwa sababu umeshaanza kugundua namna ambavyo umekuwa unapoteza muda wewe mwenyewe.

Kama unabisha, twende kwenye ushahidi, maana hapa hatuna maneno mengi leo, ni mambo kwa ushahidi. Chukua karatasi na igawe pande mbili, upande wa kulia andika malengo makubwa unayotaka kuyafikia. Upande wa kutosha andika mambo yote uliyofanya kwa wiki moja iliyopita. Kila ulichofanya kwa muda ambao hukuwa umelala, kiorodheshe. Namaanisha kila kitu, hata kama ulibishana na mtu, uliingia mtandaoni, ulifuatilia michezo, yote yaandike. Baada ya hapo, chora mshale kutoka kwenye kile ulichofanya kwenye huo upande wa kushoto na lengo ambalo kinatimiza kwenye upande wa kulia.

Sitaeleza zaidi hapo, fanya hilo zoezi na kile utakachokiona, kama hakitakupa hasira kwenye usimamizi mzuri wa muda wako, basi umepotea kiasi kwamba hakuna kinachoweza kukuokoa.

Nimalize tu kwa kusema, muda unao mwingi sana, mpaka umeamua kuupoteza kwa mambo yasiyokuwa na tija. Ukiamua sasa kusimamia na kutumia vizuri kila muda wako, utaweza kufanya makubwa sana unayotamani kufanya. Ni maamuzi yako tu kwenye matumizi ya muda wako.

2. Huhitaji Jitihada Za Ziada Kwenye Kufanya.

Nakumbuka nilipochaguliwa kidato cha tano, nilienda shule na kukuta wanafunzi karibu wote huwa wanakesha wakisoma. Mimi nilikuwa nimezoea kulala saa nne, lakini kila niliporudi bwenini kulala, nilijikuta peke yangu. Nikasema wacha na mimi nikeshe kama wengine. Kweli nikakesha siku moja, lakini nilijikuta nalala siku tatu bila kuweza kabisa kusoma. Na hapo ndipo nikarudi kwenye ratiba yangu ya kulala saa 4 na kuamka saa 10 alfajiri. Niligundua nikisoma muda wa saa 10 alfajiri mpaka saa 1 asubuhi nilikuwa napiga hatua kubwa kuliko nikikesha.

Najua unapowaangalia wengine jinsi wanavyoweka kazi kwa juhudi kubwa, unaweza kujiona wewe kama unacheza hivi. Na hilo litakusukuma uwaige kwenye utendaji wao, kitu ambacho kinakupoteza zaidi kuliko kinavyokusaidia.

Kuna makala moja nimeisoma karibuni, ambayo inaeleza vizuri dhana hiyo. Mwandishi Michael Ashcroft ameandika; “Ufanisi wa kweli unamaanisha kuondoa juhudi zisizohitajika; unapoacha kulazimisha, kiwango sahihi cha juhudi kinachohotajika ni sifuri.”

Unaposikia kiwango cha juhudi kinachohitajika ni sifuri unaweza kudhani hupaswi kufanya kazi kabisa. Lakini hicho siyo anachomaanisha, bali anamaanisha usiweke juhudi zozote za kulazimisha. Ukishaona unaweka tu juhudi kwa kulazimisha, jua hizo juhudi zinapotea na hakuna matokeo utakayoyapata.

Hapo ulipo, kuna vitu ambavyo wewe kuvifanya ni kama mchezo tu, huhitaji hata kujilazimisha, wakati kwa wengine ni kazi ngumu na ya kuchosha. Hivyo vinavyokuja kirahisi kwako ndiyo vyenye mafanikio yako makubwa. Siyo kwamba vinakuwa rahisi kufanya au havihitaji kazi, bali huhitaji kujilazimisha kuvifanya.

Inapokuja kwenye juhudi, umekuwa unazipoteza bure kwa mambo unayolazimisha kufanya, ambayo hayatakupa matokeo yoyote. Peleka juhudi sahihi kwa mambo yaliyo sahihi kwako na hiyo itakuwa na tija kwa kile unachotaka kupata au kufikia.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekueleza rasilimali nyingine tatu za msingi ulizonazo sasa na ambazo ukizitumia vizuri utafanikiwa sana. Na moja ya rasilimali hizo ni pesa. Najua unalalamikia sana kukosa fedha au mtaji, lakini ukweli ni fedha ulizonazo sasa zinakutosha kabisa kujenga mafanikio unayoyataka.

Kwenye barua nimekuonyesha jinsi ya kuanza na fedha ulizonazo sasa, hata kama ni ndogo sana, kuwa mbegu ya kujenga utajiri mkubwa. Ukijua hilo, kamwe hutalalamikia tena kukosa fedha au mtaji kama kikwazo.

Karibu usome barua hiyo hapa; #BZK046; Rasilimali Za Msingi Unazo Za Kutosha, Unashindwa Kuzitumia Vizuri Kufanikiwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.