Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Mara zote tunakazana sana na kile tunachotaka, ambayo ndiyo mafanikio tunayopambania. Na licha ya kupambana sana, bado hatupati matokeo tunayokuwa tunatarajia kupata. Hapo ndipo wengi wanaposhindwa kuelewa, kwa sababu wanajiona wakiwa wamefanya yale wanayopaswa kufanya, ila matokeo siyo waliyotarajia kupata.

Kabla ya kuendelea kuhangaika na yale unayofanya, ni lazima kwanza uangalie wapi ambapo unajikwamisha. Kwa sababu, kama unafanya kila unachopaswa kufanya, lakini matokeo hayaji kama ulivyotarajia, kuna mahali unakuwa unajikwamisha wewe mwenyewe.

Kwenye barua hii tunaenda kuangalia maeneo matano ambayo ndiyo yamekuwa yanawakwamisha watu wengi wasipate mafanikio makubwa wanayoyataka. Yasome kwa kina na kisha jitafakari wewe mwenyewe ili uweze kuona ni wapi ambapo umekwama. Ukishajua ulipokwama, unajikwamua na matokeo yanabadilika.

1. Kutokuanza Kabisa.

Ukiwasikiliza wengi wanaokuambia wamepambana sana kupata mafanikio la hawajayapata, unaweza kuwaamini. Ni mpaka pale utakapowaangalia yale wanayofanya na yale yanayopaswa kufanyika ili wafanikiwe, ndiyo unaona wazi kwa nini hawapati mafanikio.

Watu wanafanya vitu vingi sana, siku zinaanza na kuisha wakiwa wamechoka kweli kweli. Lakini unapoanza kukagua kitu kimoja kimoja walichofanya, na kuhoji kina mchango gani kwenye mafanikio wanayoyataka, unakuta hakuna kabisa.

Kwa sababu wamesikia mafanikio yanataka mtu afanye kazi kwa juhudi kubwa na kwa muda mrefu, wengi wanawahi kuamka asubuhi na mapema na wanachelewa kulala. Masaa zaidi ya 16 kwenye siku zao yanakuwa yametawaliwa na kufanya mambo mbalimbali.

Lakini kwa bahati mbaya sana, karibu mambo yote wanayofanya hayana mchango wa moja kwa moja kwao kupata mafanikio makubwa wanayoyataka. Wanafurahia tu kusema wapo ‘bize’, ila hakuna tija yoyote kwa huo ubize wanaokuwa nao.

Wengi wanadhani uvivu kwenye mafanikio ni kutokufanya kabisa. Lakini ni zaidi ya hapo, kuhangaika na vitu ambavyo havina mchango kwenye matokeo unayotaka nao ni uvivu. Na hilo linasababishwa na kuepuka ugumu wa mambo ya msingi kufanya.

Iko hivi rafiki, yale unayopaswa kufanya ili upate mafanikio unayoyataka huwa ni magumu. Na sisi binadamu hatupendi mambo magumu, hivyo tunakimbilia kwenye mambo mepesi kufanya. Tunakuwa bize na kuchoka kweli kweli, lakini hakuna chochote tunachokuwa tumezalisha.

Kuondoa kikwazo hiki, kagua kila unachofanya, kabla hata hujaanz akukifanya na jiulize kina mchango gani kwenye mafanikio unayoyataka. Kama kina mchango fanya, kama hakina achana nacho mara moja. Ukifanya zoezi hili kwa kila unachofanya, utaona jinsi umekuwa unapoteza muda wako kwenye mambo mengi yasiyo na tija.

Okoa muda unaopoteza kwenye mambo yasiyo na mchango kwenye mafanikio yako ili upeleke kwenye mambo yenye tija na uache kujikwamisha kufanikiwa.

2. Kukata Tamaa Mapema.

Ukiacha kufanya mambo ambayo hayana tija na kufanya yale tu yenye mchango kwa mafanikio yako, utaona jinsi una muda mwingi. Utafurahi kuona sasa una muda wa kuhangaika na mambo yaliyo muhimu pekee.

Mwanzo utafurahia sana, kwa kuona kumbe inawezekana kabisa kufanya yale yote muhimu kwako kufanya. Lakini sasa, furaha yako haitadumu sana, kwani itakutana na uhalisia ambao hukuutegemea.

Pamoja na kufanya yale yaliyo sahihi kwa mafanikio yako, bado matokeo utakayoyapata, hasa awali, hayatakuwa mazuri kama unavyotegemea. Mambo yatakuwa magumu, changamoto na vikwazo vitakuwa vingi.

Hapo unaweka kazi, unaweka muda, unaweka juhudi na unachoka sana. Lakini matokeo unayokuja kupata, ni madogo sana ukilinganisha na matarajio unayokuwa nayo.

Na hapo ndipo wengi hukwama, kwa kukata tamaa na kuona hicho wanachohangaika nacho siyo sahihi. Ghafla wanaona fursa nyingine nzuri na rahisi kwao, ambazo wanaona wakiingia tu watapata matokeo kwa haraka kuliko pale walipo.

Wengi wanashawishika kuacha kile wanachofanya na kwenda kwenye hicho kingine kipya kinachowavutia. Na huko pia, mchezo unaenda kurudia hivyo hivyo. Wanaanza kwa matumaini makubwa, wanafanya yote wanayopaswa kufanya, lakini matokeo yanakuwa tofauti kabisa.

Watu wengi sana wamekuwa kwenye huo mzunguko kwa maisha yao yote. Kila wakati wanakimbizana na fursa mpya, fursa ambazo ni rahisi na za uhakika, kabla ya kuingia. Ni pale mtu anapoingia kwenye fursa husika ndiyo anagundua ina ugumu na changamoto zake.

Kuondokana na kikwazo hiki, acha kukimbia pale mambo yanapokuwa magumu. Unapoweka malengo na mipango yako ya mafanikio, jipe kipindi cha utekelezaji ambacho hutaacha hata matokeo yaweje. Mara nyingi sana watu wamekuwa wanakata tamaa wanapokuwa wamekaribia matokeo mazuri.

Kwa kujipa muda ambao utaendelea kufanya, utaweza kuzivuka nyakati ngumu ambazo ndiyo zinashawishi sana kukata tamaa. Ukishavuka nyakati hizo, unagundua kwamba mambo siyo magumu kama ulivyokuwa unaona wakati unayapitia.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK070; Kujenga Utajiri Mkubwa Kupitia Biashara, Unahitaji Wateja Wa Aina Hii