Rafiki yangu Mpendwa,

Kwenye mafunzo ya mauzo ambayo huwa natoa, nimekuwa natumia dhana ya ‘kumi ni moja’. Kwenye dhana hiyo nimekuwa namaanisha chochote unachotaka kupata, zidisha mara kumi. Kwa maana kwamba, kama unataka kumuuzia mteja mmoja, basi ongea na wateja 10.

Katika kufafanua zaidi dhana hiyo, nimekuwa nasema chini ya 10 ni sifuri. Mtu akiniambia ana ahadi za wateja, namuuliza ni ahadi ngapi. Akiniambia ahadi ni 5 namwambia hapo huna ahadi. Ukiwa na ahadi 10 za wateja, hapo ndiyo una ahadi 1.

Ni dhana inayosaidia sana, kuhakikisha watu wanaweka juhudi sahihi. Kwa sababu watu wamekuwa na matumaini makubwa kwenye juhdi zisizo sahihi na hawapati matokeo.

Unakuta mtu wa mauzo analalamika wateja wengi wamenipa ahadi ila hawajatimiza. Mimi huwa naanza tu na namba; ‘wangapi walikupa ahadi?’ Mara nyingi unakuta ni chini ya kumi. Na hapo nawaambia wazi, hukuwa na ahadi yoyote.

Msisitizo ni mmoja, chochote unachotaka kitokee, hakikisha umeweka juhudi mara 10 yake. Kama unataka wateja watatu wanaoweka ahadi wanunue, hakikisha una ahadi 30. Tofauti na hapo unajifurahisha tu.

Hivi karibuni nimekutana na upande wa pili wa dhana hiyo ya ‘kumi ni moja’ ambao umeniongezea kitu. Na kwa sababu wewe rafiki yangu huwa sipendi ubaki nyuma, kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukushirikisha upande huo pia.

1. Moja Ni Kumi Kwenye Ushindi.

Kitu kipya nilichojifunza na kuboresha dhana ya kumi ni moja ni hiki; Fikiria kila wateja 10 unaoongea nao kama kipande kimoja cha mauzo. Kama umefanikiwa hata kwa mteja mmoja tu, kipande kizima kimefanikiwa.

Unajua, pamoja na ung’ang’anizi tunaokuwa nao, bado kushindwa na kukataliwa kunauma. Kama unaongea na mtu wa kwanza akakataa, ukaongea na wa pili naye akakataa. Wa tatu na wa nne hivyo hivyo, ni rahisi sana kukata tamaa na kuona zoezi limeshindikana.

Lakini ukichukulia kuongea na watu kumi kama kipande kimoja cha kazi, unachohitaji ni mmoja tu aeleweke ili kipande hicho kiwe kimefanikiwa. Sasa kweli utashindwa kupata mtu mmoja wa kueleweka kwenye watu 10? Unahitaji hapana 9 na ndiyo 1 tu kuwa umefanikiwa.

Unaona jinsi kubadili huo mtazamo kunavyokupa nguvu ya kuendelea? Kwa sababu hufikirii kila hatua kama vita ya kushinda au kushindwa, unajua ni hatua tu. Ni mpaka ukamilishe hatua 10 ndiyo utapima kama kipande kimefanikiwa au la.

Ni nadra sana upige hatua 10 na zote utoke kapa kabisa.

2. Shinda Kwa Mafungu.

Watu wanaouza vitu kwa mafungu huwa hawakubali uchague mwenyewe fungu lako liweje. Wanakupangia fungu, na ndani ya fungu kutakuwa na vitu vizuri na visivyokuwa vizuri. Ukitaka uchague fungu mwenyewe, bei inabadilika.

Ni sawa na uende buchani kununua nyama, halafu unamwambia muuzaji usiniwekee mfupa kabisa. Atakupa bei tofauti ya kupata nyama tu bila mifupa. Lakini ukitaka kwa bei ya kawaida, lazima nyama itakuwa na mfupa.

Sasa wewe unataka matokeo, lakini siyo kila hatua unayochukua itakupa matokeo. Kuna hatua ambazo hazitaleta matokeo na zipo hatua zitakazokupa matokeo.

Kwa bahati mbaya sana, hatua zisizoleta matokeo huwa zinaumiza na kukatisha tamaa. Ni sawa na uende buchani na uuziwe mifupa tu, tena kwa bei ya kawaida.

Ili kuzuia hatua zisizokupa matokeo kukukatisha tamaa, ziweke kwenye mafungu hatua zote unazochukua. Unakuwa na fungu la hatua unazochukua, ambapo huhitaji hatua zote zilete matokeo. Unachotaka ni hatua chache kati ya hizo kuleta matokeo. Na hapo fungu zima linakuwa la mafanikio.

Kwa kila unachofanya, weka kwenye mafungu. Yanaweza kuwa ya namba, muda, gharama n.k. Muhimu ni kuhakikisha kitu kimoja hakiamui mafanikio yako.

Uzuri wa dhana hii ya kushinda kwa mafungu ni inafukia zile hatua ambazo hazikuleta matunda. Na inafanya usikatishwe tamaa na hatua za aina hiyo.

Ni kama kubadili mchezo, kutoka kuwa wa kutoana na kwend akuwa wa ligi. Kwenye mchezo wa kutoana una nafasi chache tu unakuwa umetolewa. Lakini kwenye ligi, una nafasi nyingi za kucheza, hivyo kushindwa mchezo mmoja siyo mwisho wa mashindano.

Geuza mchezo wako wa mafanikio uwe wa ligi, ambapo una michezo mingi ya kucheza na huhitaji kushinda yote ndiyo uwe umefanikiwa. Ukienda kwa mtazamo huo hakuna kitakachoweza kukukatisha tamaa.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK099; Kumi Ni Moja, Mtazamo Sahihi Wa Kutokukatishwa Tamaa Na Kushindwa.