Mpendwa rafiki yangu,

Watoto wengi zama hizi wanapitia changamoto nyingi na wakati mwingine hakuna mtu anayewasikiliza matatizo yao wanayopitia. Huenda wazazi wako bize sana na kazi kiasi cha kusahau watoto wao.

Watoto hawapati muda wa kukaa na wazazi wao, wazazi wanatakiwa kutenda muda wa kukaa na watoto wao kuwauliza nini kinaendelea katika maisha yao,wanapitia nini, kwa sababu watoto wanafanyiwa udhalilishaji wa kijisia kama vile watoto kulazimishwa mapenzi na watu wao wa karibu na hata watoto wa kiume kulawitiwa.

Watoto wengi hawapo salama zama hizi kwa sababu ya wazazi hawajawajengea watoto wao falsafa bora ya kuwawezesha kukabiliana na haya yote haya. Tunawalea watoto kama vile tutaishi nao milele na inapotokea sisi hatupo watoto wanapata shida.

Unatakiwa kuwajengea watoto falsafa bora ya kujitegemea tokea wakiwa wadogo. Wafundishe watoto misingi ya kazi na misingi ya dunia. Tusipowafundisha watoto wetu ukweli dunia itakuja kuwafundisha ukweli wa maisha kwa adhabu kubwa sana.

gift to my childern

Walee watoto kama hutoishi nao milele, wafundishe misingi ya kujitegemea wao wenyewe na kukabiliana na magumu yanayojitokeza mbele yao. Kama mtoto wako kwa sasa humfundishi kazi, unamwachia tu akae baadaye dunia itakuja kumtesa. Mfundishe mtoto misingi yote, jinsi fedha inavyopatikana na namna ya kufanya kazi.

Unapowapa watoto misingi ni rahisi kusimama wao wenyewe kwa miguu yao. Misingi bora utakayowapa itakuja kuwasaidia huko mbeleni na watakuja kukushukuru sana. wazazi wengi hawawaelezi watoto wao ukweli halisi wa maisha ndiyo maana watoto wanakuja kupata shida huko mbeleni.

SOMA; Hizi Ndiyo Nguzo Nne Za Malezi Bora

Anza kuwajengea watoto falsafa bora tokea wakiwa wadogo, wafundishe tabia bora, wafundishe namna ya kujilinda na pale watu wanapotaka kuwafanyia ndivyo sivyo wafanye nini. Tuwapatie watoto malezi elekezi ambayo yatawajengea msingi wa kujitegemea kuliko kuwalea kama vile tutaishi nao milele.

Hakuna mwenye uhakika kwamba mtoto au watoto alionao ataishi nao milele hivyo ni vema kumwandaa kama vile hutaishi naye milele kwa kumfundisha kile atachopaswa kufanya nini.

Hatua ya kuchukua leo; wafundishe watoto falsafa ya kujitegemea, wape misingi bora ambayo itawawezesha kusimama wao wenyewe na kujua ukweli wa dunia kuliko kuwaficha. Usiwafundisha watoto maisha, dunia itakuja kuwafundisha kwa riba bila huruma.

Hivyo basi, maisha hayana huruma na mtu, kama unamwonea mtoto wako huruma basi anza kumfundisha mapema misingi bora ya kuishi. Mfundishe falsafa bora ya kujitegemea ambayo ataweza kuiishi hata wewe usipokuwepo.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana