Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio kwenye maisha huwa hayatokani sana na nini unachofanya, bali jinsi unavyofanya kile unachofanya.
Tunaona kwenye kila eneo la maisha, kuna waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa. Kwenye kila aina ya kazi na biashara, kuna ambao wamefanikiwa na ambao hawajafanikiwa.
Kwenye kila eneo, tasnia na watu, kuna ambao wana utajiri na wenye umasikini. Hivyo basi, kama kuna watu wawili, wanaofanya kitu cha aina moja, ila mmoja ana mafanikio kuliko mwingine, tofauti yao haitakuwa inatokana na kile wanachofanya, bali namna wanavyofanya.

Yule ambaye amefanikiwa anakuwa anafanya kitu kwa utofauti kabisa na wale ambao hawajafanikiwa. Na kwa sehemu kubwa sana, wale wanaofanikiwa huwa wanafurahia kile wanachofanya na hivyo kukifanya kwa muda mrefu kuliko ambao hawajafanikiwa.
Je ni kitu gani ambacho mtu atapenda kukifanya na akakifanya vizuri kiasi cha kufanikiwa zaidi kuliko wengine? Jibu ni moja, kipaji ambacho mtu anacho.
Rafiki, kipaji kinalipa sana pale mtu anapoweza kukitumia vizuri. Pale unapofanya kazi au biashara inayotokana na kipaji chako, unakuwa kwenye nafasi kubwa ya kufanikiwa kuliko ambao hawana kipaji.
Hiyo ni kwa sababu wakati wengine wanaona ugumu kufanya, wewe unakuwa kama mchezo kwako. Wakati wengine wanatumia muda mwingi kukwepa kufanya na kupumzika, wewe unafanya muda mwingi zaidi.
Kwa mtu kupenda unachofanya, kukifanya vizuri na kwa muda mrefu kuliko wengine, hakuna namna utashindwa kufanikiwa kuliko wengine wanaofanya. Utapata fedha na mafanikio makubwa kuliko wengine.
Rafiki, je wewe kazi au biashara unayofanya sasa inatokana na kipaji chako au ni tofauti? Kama inatokana na kipaji, hongera, weka juhudi kubwa na haitachukua muda mrefu kwako kufanikiwa.
Lakini kama unachofanya hakitokani kabisa na kipaji chako, basi unapaswa kuangalia kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini maana kina ujumbe muhimu sana kwako. Jifunze na chukua hatua ili uweze kugeuza kipaji chako kuwa njia ya kukuingizia kipato na kukupa mafanikio makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.