Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Unajua jinsi ninavyokupenda, na ndiyo maana siachi kukuandikia hizi barua. Kwa sababu najua ni mwongozo muhimu sana kwako na kwangu kuhakikisha tunajenga maisha tunayoyataka, kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wetu kabisa.
Kitu kimoja ambacho kimekuwa kinanishangaza sana kuhusu watu wengi kwenye hii safari ya mafanikio ni jinsi wanavyohangaika na mambo mengi, wakati swali la msingi kabisa hawajaweza kulijibu.
Unakuta mtu anahama kutoka kazi moja kwenda nyingine kila baada ya muda mfupi. Anaanzisha biashara mpya kila anaposikia ni fursa, lakini baada ya muda anaiacha na kwenda kuanzisha nyingine. Anahamia eneo fulani, lakini hakai muda anahama na kwenda eneo jingine.
Watu wanahangaika na mambo hayo mengi, kwa kuona wana uhuru wa kufanya hivyo au wanatafuta fursa nzuri zaidi. Lakini sasa, mwisho wa hayo yote ni lini? Na wapi? Kwa bahati mbaya sana, mtu akishakuwa kwenye mwendo huo, huwa hakuna mwisho. Kwa sababu tatizo siyo fursa, tatizo ni wao wenyewe hawajajua nini hasa wanachotaka.
Mtu ambaye hajajua nini hasa anachotaka kwenye maisha yake, atahangaika na mambo mengi na kamwe hatapata utulivu. Hiyo ni kwa sababu kila atakachofanya, hata kama kinampa matokeo, kama siyo hasa alichotaka, hawezi kuridhika. Bado ataona kuna fursa nzuri zaidi ambazo hazipaswi kumpita.
Ndiyo maana kwenye barua ya leo tunarudi kwenye msingi muhimu, wa kujua nini hasa tunachotaka kwenye maisha yetu, ili tupate utulivu na mafanikio. Hata kama tayari tumeshajua, ni muhimu tujikumbushe, kwa sababu sisi binadamu tuna tabia ya kujisahau sana.
Tusipojikumbusha mara kwa mara kile tunachotaka na njia ambayo tumeichagua, ni rahisi kubebwa na mkumbo wa wengine kwa kuona kuna fursa nzuri kuliko zile ambazo tayari tunazo.

1. Jukumu Kubwa La Utu Uzima.
Wakati nakua, kulikuwa na utani kwamba polisi wanapomkamata mtu kwa ajili ya upelelezi wa jambo lolote wanatumia kauli; ‘Utaenda kuisaidia polisi.’ Sasa utani ulikuwa kwamba mtu akisikia anaambiwa anaenda kuisaidia polisi, anadhani anaenda kuwasaidia polisi kupiga watu. Kumbe huenda yeye ni sehemu ya tatizo, kwa hiyo anachofurahia, ni tatizo kwake.
Ukitafakari, hivyo ndivyo utu uzima ulivyo. Ukiwa mtoto, unaona kama watu wazima wanafaidi sana. Unaona wanajiamulia nini wafanye, hakuna wa kuwatuma tuma wala kuwakataza wasifanye vitu.
Tukiwa watoto tulitamani sana kuwa watu wazima, tukiona tutakuwa huru na kujiamulia mambo yetu wenyewe. Lakini sasa tumekuwa watu wazima, na ukiwa mkweli kwako, ni mara ngapi umewaangalia watoto na kutamani kuwa kama wao?
Ukiwaangalia watoto wadogo, huwezi kuacha kutamani kuwa kama wao. Kwa sababu wanaamka asubuhi, hawana majukumu yoyote ya kuwasumbua, wanajua watakula, watapata mahitaji yao, watalala na kadhalika. Hawana ratiba yoyote ya kukamilisha, hawana ahadi yoyote ya kutimiza na hawana yeyote wanayetaka kumfurahisha. Wanaishi maisha yao, kwa uhalisia wake.
Wakati tunakimbilia utu uzima hatukupewa taarifa kwamba jukumu kubwa la utu uzima ni kujua nini hasa unachotaka kwenye maisha yako. Na hatukujulisha jinsi jukumu hilo litakuwa gumu kuliko majukumu mengine yote kwenye maisha.
Kipindi chote cha utoto tulikuwa tunapangiwa nini cha kufanya, kuanzia nyumbani mpaka shuleni. Hebu fikiria shuleni, hata ulipotaka kujisaidia, hukuweza tu kuamka na kwenda chooni, ilikuwa mpaka usubiri kengele ya mapumziko au uombe ruhusa kwa mwalimu.
Hebu tafakari hilo kwa kina rafiki, kwa miaka takribani 20 umekuwa unapangiwa kila kitu cha kufanya, jinsi ya kukifanya na wakati wa kukifanya. Halafu ghafla unaachiliwa ukajiamulie mambo yako mwenyewe. Haliwezi kuwa jukumu rahisi hata kidogo.
Ulitamani sana uweze kujiamulia mambo yako mwenyewe, lakini unapofika wakati wa kuwa huru kujiamulia, unagundua ni kitu kigumu sana. Matokeo yake unarudi kwenye mazoea, ya kuangalia yale ambayo wengine wanafanya na kuyaiga.
Hiyo ndiyo sababu ya watu wengi kwenye jamii kuigana, badala ya kusikiliza kile kilicho ndani yao na kukifanya. Kwa sababu tumezoeshwa kwa kipindi kirefu kufanya yale ambayo wengine wanafanya, tunaona hayo ndiyo salama.
Hatua ya kwanza na ambayo ni muhimu zaidi kujua nini hasa unachotaka kwenye maisha yako ni kujua hilo ndiyo jukumu kuu la utu uzima. Unapaswa kujua ni jukumu gumu pia, kwa sababu hujaandaliwa kulitekeleza. Una wajibu wa kujiandaa mwenyewe ili uweze kulitekeleza kwa usahihi.
Kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha mambo mengine manne ya muhimu kwako kufanyia kazi ili uweze kujua kile unachotaka na kukifanyia kazi na mafanikio yawe yenye maana kwako.
Soma barua hiyo hapa; #BZK064; Kwani Ni Nini Hasa Unachotaka Kwenye Maisha Yako?