Rafiki yangu Mpendwa,

Hakuna kipindi bora kuwa hai kama hiki tulichopo sasa. Ukiangalia jinsi ambavyo teknolojia imerahisisha mambo mengi, unaona kabisa watu waliotutangulia walikosa fursa nzuri ambazo tunazo sasa.

Lakini sasa, cha kushangaza sana, pamoja na nyakati hizo kuwa bora sana kwa yeyote anayetaka kufanikiwa, bado ni wachache sana ambao wanayapata mafanikio makubwa wanayoyataka.

Imebaki kuwa kitendawili kigumu, iweje pamoja na fursa kuwa nyingi na sawa kwa wote, wachache pekee ndiyo wanaofanikiwa? Na majibu yanaendelea kuwa wazi kwamba wanaofanikiwa wanakuwa wanayataka mafanikio kuliko wasiofanikiwa.

Unaweza kuona kama hilo jibu ni jepesi sana na haliwezi kuelezea kwa uhalisia kile kinachoendelea kwenye michakato ya watu ya kimafanikio. Lakini nitakuonyesha kwa ushahidi kwamba hilo ndiyo jibu sahihi, pamoja na huo urahisi wake unaoonekana.

Inapokuja kwenye safari ya mafanikio, kuna hali tatu ambazo lazima mtu utumie moja wapo au hata zaidi ya moja. Hali hizo ni Werevu, Ujinga na Upumbavu.

Ujinga, ambao wengi wanaweza kuwa kwenye hali hiyo hata kama kuna vingi wanakosa, unatosha kabisa kumpa mtu mafanikio makubwa. Lakini ni kama utaweza kutumika vizuri. Werevu ni mzuri, lakini kuukosa hakuwezi kukunyima mafanikio. Ila sasa, upumbavu ni mzigo na kikwazo kwa mtu kupata mafanikio.

Kabla hujajipa upande, soma hii #BaruaYaKocha kwa kina na uone jinsi unavyoweza kutumia kila hali kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

1. Werevu, Ujinga Na Upumbavu Kwenye Safari Ya Mafanikio.

Inapokuja kwenye mafanikio na hata maisha kwa ujumla, huwa tunatumia hali hizo tatu.

Werevu ni pale tunapojifunza kutokana na makosa ya wengine. Kwa njia hiyo tunaepuka kabisa kuyafanya makosa hayo na hivyo kutokupoteza muda na gharama. Werevu ndiyo njia ya mkato ya kufanikiwa, ambayo inaokosa upotevu unaojitokeza kwa kufanya makosa bila kujua.

Ujinga ni pale tunapojifunza kutokana na makosa yetu wenyewe. Kwa kutokujua, tunafanya makosa, ambayo yanatugharimu muda na fedha. Lakini tunajifunza kwa makosa hayo na kutokuyarudia wakati mwingine. Japo ujinga unakuwa umetuingiza kwenye gharama, tunakuwa tumelipa kama funzo la nini hatupaswi kufanya tena.

Upumbavu ni kutokujifunza kabisa, hata kwa makosa ambayo mtu amefanya mwenyewe. Kwenye upumbavu, mtu anarudia kufanya makosa yale yale ambayo yamekuwa yanamgharimu na kumkwamisha. Licha ya gharama ambayo mtu anaingia, bado hajifunzi, anaendelea kurudia vile vile. Anaishia kupoteza rasilimali nyingi na hakuna hatua anazopiga.

Unaweza kudhani wewe unatumia werevu, kwa kujifunza kwa wengine. Ila nitakutahdharisha, usifikirie ni rahisi kihivyo. Historia inaonyesha binadamu huwa hatujifunzi mpaka tupate maumivu. Lakini ukiweza kujifunza kwa makosa ya wengine, utajiepusha na mengi.

Huwa hatupendi kuonekana ni wajinga, hivyo hatuulizi ambayo hatujui na tunakwepa kukosea. Kitu ambacho kinatufanya tuendelee kubaki kwenye ujinga. Hapo ndipo ambapo tuna mamlaka napo na tukiweza kupatumia vizuri, tutafanya makubwa.

Kwenye upumbavu, kila mtu huwa anakataa siyo mpumbavu, hata ambao ni wapumbavu kabisa. Hivyo nako usijipendelee sana, angalia vitu gani vimekuwa vinakukwamisha na ukiona kitu kinajirudia rudia, jua umekuwa mpumbavu kwenye hicho.

Hivo ndiyo hali tatu za mafanikio, sasa tuangalie jinsi ya kutumia kila moja.

2. Kuwa Mwerevu Kwa Kuiba.

Chukua mfano wa mtu ambaye amefanya biashara kwa miaka 30 na kupata mafanikio makubwa kwenye biashara hiyo. Na wewe unafanya biashara kama anayofanya mtu huyo, ila umepambana sana na hupati matokeo. Mtu huyo akakuambia yupo tayari kukuambia siri zake zote, je utakuwa tayari kulipa gharama kiasi gani uzipate hizo siri zake? Nina uhakika utakuwa tayari kulipa gharama kubwa sana.

Kwa bahati nzuri, mtu huyo akawa ameandika kitabu ambacho kimeeleza safari yake, makosa aliyofanya na kilichomwezesha kupata mafanikio hayo. Halafu kitabu hicho akawa anakiuza kwa gharama ndogo tu, je huoni hapo ni kama unaiba kabisa werevu wake?

Hiyo ndiyo maana nakuambia hapa njia ya kupata werevu ni kuiba. Simaanishi kuiba kwa kufanya hila yoyote, bali kwa kuangalia wale ambao wamefanikiwa kwenye kile unachofanya na kujifunza kwa kina kutoka kwao.

Jifunze makosa ambayo walifanya na wanayajutia ili na wewe usirudie kuyafanya. Jifunze vitu vilivyowatofautisha na wengine na wewe angalia nini kitakutofautisha. Jifunze kutoka kwao kwa umakini mkubwa na ondoka na vitu vya kwenda kufanyia kazi.

Hapa nakuambia uibe na siyo kuiga, kwa sababu hakuna safari za mafanikio zinazofanana. Hata yule aliyefanikiwa akirudia kila alichofanya hataweza kupata mafanikio aliyoyapata. Hivyo usijaribu kuiga, bali toka na thamani ambayo unaenda kuifanyia kazi.

Kwa zama tulizopo sasa, zama za Akili Unde (AI) huhitaji hata kuingia gharama kubwa na muda kujifunza kutoka kwa wale waliofanikiwa kwenye eneo unalofanyia kazi. Unaweza kuiambia AI eneo ualotaka kufanikiwa, ukaiambia ikuchagulie watu sahihi wa kujifunza kutoka kwao na ikakupa mpango mzima wa kujifunza.

Huko nyuma ilibidi utafute vitabu vya wahusika na kusoma, lakini kwa zama hizi, hata bila vitabu bado unaweza kujifunza kutoka kwa watu sahihi na kuiba yale ambayo yatakuwa na manufaa kwako.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK096; Ujinga Unakutosha Kufanikiwa. Werevu Unapunguza Gharama. Upumbavu Ni Mzigo.