Rafiki yangu Mpendwa,
Marafiki ni lazima waaminiane, kwa sababu hakuna mahusiano yanayoweza kujengwa kwa muda mrefu kama hakuna kuaminiana.
Nimekuwa nakuandikia #BaruaZaKocha kila siku, kwa sababu nakuamini sana. Naamini kuna kitu kikubwa unachotaka kwenye maisha yako. Na ninaamini, bila ya shaka yoyote, unao uwezo wa kupata kitu hicho kikubwa unachotaka.
Naamini hilo kuliko hata wewe mwenyewe unavyoamini. Na ndiyo maana kwenye kila #BaruaYaKocha siachi kukukumbusha upambanie kile kikubwa unachotaka.
Na hata kama hujui kipi kikubwa upiganie, tayari nimeshakusaidia hilo. Tayari nimekupa mwongozo ambao unagusa maeneo matatu; Mafanikio – kujenga tabia na nidhamu sahihi. Fedha – kujenga utajiri na uhuru wa kifedha. Na Biashara – kujenga biashara inayojiendesha bila kukutegemea moja kwa moja.
Kama utayatoa maisha yako kikamilifu kujijenga maeneo hayo matatu, ambayo yote yapo ndani ya uwezo wako, hutabaki kwenye maisha ya kawaida ambayo wengi wamenasa.
Nakuamini sana kwenye kuweza hilo rafiki, na sitaacha kukusisitiza upambanie bila kuacha, hata ukutane na nini.
Lakini pia, lazima niwe mkweli kwako. Marafiki ni lazima tuambiane ukweli, kama njia ya kuhakikisha tunakaa kwenye njia iliyo sahihi.
Kuna eneo moja ambalo nimekuwa sikuamini. Hata unaponieleza na nikaonekana kukusikiliza na kukuelewa, ndani yangu nakuwa sikuamini kabisa.
Sasa sielewi tatizo ni roho yangu mbaya na kutokujali au ni wewe unayezingua, sijui. Ila kwenye hii #BaruaYaKocha nimetaka niliweke hilo wazi, halafu wewe mwenyewe uone nani anazingua, mimi au wewe.

1. Haijashindikana, Umeacha Mapema.
Ukiniambia kitu kikubwa ulichokuwa unapambania ili kukipata kimeshindikana, halafu nakuona uko hai, huku ukicheka cheka kabisa, siwezi kukuamini. Hata unipe maelezo mazuri kiasi gani, hata utoe orodha na ushahidi wa jinsi mambo yameshindikana, nakuambia tu wazi, siwezi kukuamini.
Huwezi kusema kitu kimeshindikana wakati bado uko hai. Unachotakiwa kusema ili nikuamini ni kwamba umeamua kuacha. Ukiniambia hivyo nitakubaliana na wewe, kwa sababu huo ndiyo ukweli.
Haijashindikana, ni wewe umechagua kuacha mapema. Umeamua kuacha, huenda ukiwa umeshasogea karibu mno na kupata ulichotaka. Umeamua kupoteza nguvu zote ambazo umeshaweka kwenye kitu hicho.
Na ndiyo maana sikuamini, kwa sababu utaenda kwenye kitu kingine na kurudia mchezo huo huo. Unafanya, ukiona matokeo hayaji haraka kama unavyotaka, unaacha. Halafu unasema umefanya sana na imeshindikana. Endelea kuamini kama unataka, lakini mimi nimekataa kuamini hilo.
Sikatai tu kuamini kwa sababu sikuamini, nakataa kuamini kwa sababu sitaki kudanganyika na uongo wako ulioununua mwenyewe. Wewe mwenyewe, ndani yako, unajua kabisa kuna vitu vingi hujafanya kwenye hicho ambacho unasema kimeshindikana. Halafu unataka na mimi nikubaliane na uongo wako?
2. Afadhali Nijiue Kuliko Kukubali Kushindwa.
Elon Musk amewahi kunukuliwa akisema; “Akili yangu ni kama ya samurai. Ni afadhali nijiue kuliko kukubali kushindwa.” Hii ni nukuu inayoonyesha kitu kinachokuwa nyuma ya ushindi mkubwa. Kutokukubali kushindwa kwa namna yoyote ile. Yaani maisha kukosa maana pale mtu unapokubali kushindwa.
Ninapotafakari kauli hiyo, nazidi kukosa imani na wewe, hasa unaponiambia imeshindikana. Wanajeshi wa Sparta walikuwa wanapewa ngao wakati wa kwenda kwenye vita na maelezo yalikuwa machache; ‘Rudi ukiwa umeshika ngao hii au mwili wako urudishwe ukiwa umebebwa kwenye ngao hii.’
Hayo maelezo hayana kuchanganya, ni labda upate ushindi, au ufe ukiwa unapambania ushindi. Kuishia njiani na kukubali kushindwa, huku ukiwa bado uko hai ni aibu kubwa.
Je wewe huoni aibu unaposema imeshindikana, wakati huna hata makovu ya kutosha ya kuonyesha kwamba umepambana? Je kama maisha yako yangekuwa yanategemea wewe kupata ushindi kwenye eneo hilo unalojiambia imeshindikana, usingepambania ushindi huo?
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK093; Hili Ndilo Eneo Pekee Ambalo Kamwe Siwezi Kukuamini.