Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Unakumbuka zile hesabu za shuleni ambazo zilikuwa zinauliza hivi; ‘Mtu mmoja analima heka moja kwa masaa manne. Je watu wanne watalima heka moja kwa masaa mangapi?’

Huenda kwako zilionekana ni hesabu tu za kusumbua kichwa na kujua ili ufaulu, lakini zina matumizi makubwa sana kwenye maisha, hasa pale unapotaka kupata matokeo.

Tukirudi kwenye hiyo hesabu hapo juu, unaweza kuona ni rahisi. Kama mtu mmoja analima heka 1 kwa masaa 4, ukiweka watu 4 kwenye heka, itaisha kwa saa 1. Kihisabati inaweza kuwa ni sahihi kabisa.

Lakini kwenye uhalisia, mambo ni tofauti kabisa. Unaweza kuweka watu wanne kwenye heka moja na kazi ikachukua hata zaidi ya masaa manne. Na hata kama haitafika huo muda wa mtu mmoja, bado matokeo hayatakuwa kama unavyogawanya namba.

Na hiyo ni kwa sababu ya dhana muhimu ya ‘uvivu wa kundi’, ambayo kwa wasiojua huwa haiwezi kuonekana haraka.

Na nikuambie tu, kama umekuwa unaweka watu wengi kwenye kutekeleza jukumu lakini bado hupati matokeo unayotaka, hujajua hiyo dhana ya uvivu wa kundi.

Chukua mfano rahisi kwenye biashara, una wauzaji wawili na unauza milioni 1 kwa siku. Hapo unajiambia ukiwa na wauzaji wanne, unaenda kuuza milioni 2 kwa siku. Ni mpaka unapoongeza wauzaji hao na matokeo usiyapate ndiyo unashindwa kuelewa unakwama wapi.

Unapokwama ni mahali pamoja tu, kushindwa kuielewa dhana ya uvivu wa kundi na kuizuia isiwe kikwazo kwako kupata matokeo unayotaka.

Hapa kwenye #BaruaYaKocha naenda kukuonyesha dhana hiyo ya uvivu wa kundi, kwa nini inatokea, jinsi inavyokuathiri na njia za kuizuia ili isiwe kikwazo kwako. Kama unafanya kazi na timu ya watu, hiki ni kitu muhimu sana kwako kujua ili upate matokeo makubwa.

1. Ringelmann Effect; Juhudi Za Mtu Binafsi Kupungua Anapokuwa Ndani Ya Kundi.

Mwaka 1913, Maximilien Ringelmann, aliyekuwa mchumi wa kilimo wa nchini Ufaransa, aligundua kitu kimoja kilichomshangaza sana. Alifanya jaribio rahisi ambalo lilionyesha wazi jinsi saikolojia ya binadamu inavyofanya kazi, hasa inapokuja kwenye majukumu ya kushirikiana.

Alianza kwa kumwambia mtu mmoja avute kamba, na hapo mtu alitumia nguvu kubwa kuvuta kamba hiyo. Kisha akawaweka watu wengi kwenye kundi na kuwataka wavute kamba. Na hapo ndipo kitu cha kushangaza kilipoonekana. Walipokuwa ndani ya kundi, watu walitumia juhudi kidogo zaidi kuvuta kamba kuliko walivyokuwa wanavuta wenyewe.

Pamoja na kwamba juhudi kwa kundi zima zilikuwa kubwa kuliko juhudi za mtu mmoja, juhudi ya mtu mmoja mmoja ndani ya kundi ilikuwa ndogo kuliko wakiwa peke yao. Hapo kuna funzo kubwa sana kuhusu utendaji wetu binafsi na utendaji wa timu tunazosimamia.

Unaweza kuweka watu wengi kwenye jukumu moja, kwa matarajio ya kupata matokeo makubwa na kwa haraka, lakini matokeo unayopata yakawa tofauti na matarajio. Kwa matokeo hayo unaweza kudhani watu hawatoshi, na hivyo ukawaongeza zaidi na matokeo yakazidi kuwa mabaya.

Kwa kutambua hii dhana ya uvivu wa kundi, ya juhudi za mtu mmoja mmoja kupungua anapokuwa kwenye kundi, utaweza kujua kwa nini hupati matokeo unapokuwa na watu wengi na jinsi ya kulikabili hilo.

2. Kinachosababisha Uvivu Wa Kundi.

 Ni jambo la kushangaza sana unapoweka watu wengi kwenye jukumu moja matokeo yanayopatikana kuwa madogo kuliko ambayo yangepatikana kama kila mtu angefanya peke yake.

Inaweza kuonekana kama ni hujuma, lakini hii ni hali ya kisaikolojia inayotokea pale watu wanapofanya kitu chochote ndani ya kundi. Kinachosababisha juhudi za mtu mmoja mmoja kupungua ndani ya kundi ni kama ifuatavyo;

i. Kukosekana kwa uwajibikaji wa moja kwa moja. Watu wanapofanya jambo peke yao, wanakuwa wanawajibika moja kwa moja, hivyo wanajituma sana. Lakini wanapokuwa ndani ya kundi, hawaoni wakiwajibika wao moja kwa moja, hivyo hata wasipoweka juhudi sana, haiwaathiri moja kwa moja.

ii. Kudhania wengine watafanya na kufidia sehemu yao. Mtu anapofanya kitu peke yake, anajua kabisa yeye ndiye anayetegemewa. Lakini mtu huyo huyo akifanya kitu na watu wengine, anajiambia hata asipofanya kuna wengine watafanya. Mbaya zaidi ni pale mtu anapotegea kwa kudhani wengine nao pia wanategea. Hapo ndipo juhudi za kundi zinapokudha dhaifu zaidi.

iii. Mawasiliano na usimamizi mbovu. Mtu anapokuwa mmoja au wachache, mawasiliano yanakuwa rahisi na kazi inaenda. Watu wakiwa wengi, mawasiliano yanakuwa magumu na kuwasimamia wote inakuwa vigumu. Hilo linapelekea matokeo kuwa hafifu zaidi kwa kundi kubwa.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK108; Kabla Hujaongeza Watu Ili Upate Matokeo, Kuwa Makini Na Dhana Hii Ya ‘Uvivu Wa Kundi’