Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kila mtu ambaye ameweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yake, kuna namna huwa anaonekana kuwa na roho mbaya. Kuna namna watu hao wanakuwa na ukatili unaowafanya wapate matokeo makubwa ambayo wengine hawayapati.

Wakati mwingine wale wasiofanikiwa huwa wanawaangalia waliofanikiwa na kujiambia kama wangeweza kuwa na roho kama walizonazo waliofanikiwa, basi na wao wangefanikiwa. Kwa sababu wanaona wazi jinsi ambavyo namna walivyo kunapelekea matokeo makubwa yapatikane.

Na pia kuna ambao wanajifariji kwa roho nzuri kama sababu ya kutokufanikiwa. Hawa wanapowaangalia waliofanikiwa na namna wanavyofanya mambo yao, wanawaona kama ni wenye dhambi sana. Kwa kuwa wao hawana vurugu ambazo waliofanikiwa wanazo, wanajiona wakiwa wema sana. Na wanaona wema wao ndiyo unaowakwamisha kufanikiwa.

Ukweli ni kwamba, mafanikio makubwa hayawezi kwenda kwa mtu ambaye anaishi maisha ya kawaida. Ni lazima mtu awe na maisha ambayo wengine wanayaona ni ya ajabu na hata kuwaonea huruma ndiyo waweze kuzalisha matokeo makubwa.

Na roho mbaya na ukatili ambao watu wanaofanikiwa wanaonekana kuwa nao, huwa siyo kwa watu wengine, bali ni kwao wenyewe. Wote waliofanikiwa huwa wanakuwa ni wakali sana kwao wenyewe kiasi cha kuonewa huruma na wale wanaowazunguka. Kwa ukali wanaokuwa nao kwao wenyewe, kunawafanya wanaozunguka nao kujiingiza wenyewe kwenye ukali wao.

Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza ‘ukatili’ unaopaswa kuwa nao ili uweze kujijengea mafanikio makubwa. Neno ‘ukatili’ lipo kwenye mabano kwa sababu siyo aina ya ukatili ambayo huwa inafanyika. Siyo ukatili wa kuwaumiza watu, bali ni ukatili wa kuhakikisha unafanya kilicho sahihi bila kuruhusu sababu zozote kukukwamisha.

Karibu ujifunze ‘ukatili’ unaopaswa kujijengea ili safari yako ya mafanikio iweze kukamilika.

1. Ondoa Mambo Kikatili.

Kitu kimoja ambacho nimekuwa naona kinajirudia kwa kila aliyefanikiwa ni fokasi. Wote wanaofanikiwa huwa wanapeleka rasilimali zao zote kwenye kitu kimoja au vitu vichache sana. Kwa mkusanyiko huo wa rasilimali kwenye maeneo machache, kupata matokeo makubwa inakuwa kitu cha uhakika.

Sasa basi, ili mtu aweze kufokasi, ni lazima awe na ukatili kwenye kuondoa mambo mengi anayovutiwa kujihusisha nayo. Lazima aseme hapana kwenye fursa nzuri zinazokuja kwake, ambazo haziendani na mafanikio anayoyataka. Lazima achague kuacha kufanya baadhi ya mambo ambayo ameshayafanya kwa muda mrefu, lakini hayana mchango kwenye mafanikio anayoyataka.

Steve Jobs amewahi kusema watu huwa wanadhani fokasi maana yake ni kusema ndiyo kwenye mambo muhimu. Lakini maana halisi ya fokasi ni kusema hapana kwa mambo ambayo ni mazuri, lakini hayana mchango kwenye kile ambacho mtu unataka kufanya.

Watu wengi wanakwama kufanikiwa kwa sababu wanakosa fokasi. Wanahangaika na mambo mengi, ambayo yanaweza kuwa ni mazuri, lakini hayana mchango kwenye mafanikio makubwa wanayoyataka. Na hata kama yana mchango, siyo yote yana mchango uliofanana. Mambo yanatofautiana kwenye mchango na umuhimu, kuna machache sana yenye mchango mkubwa na mengi yenye mchango mdogo.

Unahitaji kuwa katili ili uweze kuwa na fokasi. Kwa sababu fokasi inakutaka ukatae na kuondoa fursa ambazo zinaonekana kuwa na manufaa. Inahitaji ukatili kwa sababu unahitajika kuacha vitu ambavyo vina matokeo kwako au kwa wengine. Kwa kifupi, kufokasi kutafanya uonekane unapoteza mwanzoni, kwa kuziacha fursa ambazo zina manufaa.

Unahitaji ukatili kukataa na kuondoa vitu ambavyo vina matokeo, ili upeleke rasilimali zako kwenye vitu vichache ambavyo vitakupa matokeo makubwa baadaye. Watu wanaweza kukuona kama umechanganyikiwa, pale wanapokuletea fursa nzuri za kupata matokeo, lakini wewe unasema hapana ili uweze kufokasi kwenye kile ulichochagua.

Mafanikio makubwa yanakutaka uwe na kipaumbele kimoja kikuu unachokifanyia kazi. Kipaumbele hicho kinakuwa na jambo moja kubwa unalofanyia kazi au machache ambayo yanaendana sana. Baada ya kuchagua hivyo, mengine yote unaachana nayo kama tayari unayafanya au unasema hapana kama bado hujaanza kuyafanya. Hilo linahitaji ‘ukatili’ kwako binafsi ili kulitekeleza, lakini lina matokeo makubwa ukiweza kulikamilisha.

2. Chukua Hatua Kwa Vurugu.

Kuweka malengo na mipango ya mafanikio ni kitu rahisi, ambacho wengi huwa wanakifanya. Watu wamekuwa wanaweka mipango mizuri sana, ambayo ukiiangalia, unaona kabisa mafanikio makubwa haya hapa.

Na kwa zama hizi za teknolojia kama ya Akili Mnemba (AI), kuweka mipango mizuri siyo shida kabisa. AI inaweza kukusaidia kuweka mipango bora kabisa ya mafanikio, ikikupa kila aina ya taarifa unayohitaji kwenye kuweka mipango hiyo.

Shida kubwa huwa inakuja kwenye utekelezaji wa mipango hiyo, yaani kwenye kuchukua hatua. Inapofika wakati wa kuchukua hatua, watu wanagundua kuna vitu bado hawajawa navyo. Na hivyo wanajikuta wakiahirisha kuchukua hatua na kusubiri mpaka wawe tayari.

Hapo ndipo safari ya mafanikio kwa wengi huwa inaishia, kwa sababu hakuna wakati ambao mtu atakuwa na kila anachohitaji ili afanikiwe. Kila wakati kuna kitu ambacho mtu anakuwa hana au hajakamilisha. Na kila wakati kuna sababu ya kuendelea kusubiri badala ya kuchukua hatua.

Mafanikio makubwa yanataka mtu uwe katili kwenye kutekeleza mipango unayoweka. Yanataka uchukue hatua kwa vurugu kubwa ili mambo yaweze kutokea. Ni kuanza kufanya hata kama bado hujawa tayari au kuna vitu havijakamilika. Ukishapanga, unaanza kufanya, kwa kutumia vile ambavyo tayari unavyo.

Kuchukua hatua kwa vurugu siyo kuleta uharibifu, bali ni kutokuruhusu kitu chochote kikukwamishe. Ukishapanga, unafanya, hata kama una sababu nzuri kiasi gani za kutokufanya.

Unaweza kudhani kuchukua hatua ni rahisi na halihitaji ukatili tunaozungumzia hapa, lakini jaribu kujichunguza wewe mwenyewe, ni mambo mangapi umepanga na mangapi umetekeleza. Na kama ungetekeleza kila ulilopanga, kwa jinsi ulivyopanga, unadhani ungekuwa wapi sasa?

Ni rahisi sana kujishawishi kutokuchukua hatua, hasa pale unapokuwa na vitu ambavyo havijawa tayari. Ni rahisi zaidi kushawishika kuacha kuchukua hatua pale unapokutana na magumu na changamoto.

Ukatili unaohitaji ni wa kupanga na kutekeleza kama ulivyopanga bila kuruhusu sababu zozote. Hata kama kuna kitu hakikuwa sawa kwenye mipango, huachi kutekeleza, badala yake unatekeleza huku ukiendelea kuboresha.

Kilicho muhimu ni kuhakikisha unakuwa mtu wa kuchukua hatua mara moja na kuendelea kuchukua hatua kama ulivyopanga. Ni kuacha kuwa mtu wa kuruhusu sababu na visingizio kukukwamisha kuchukua hatua kwenye mambo uliyopanga.

Umepanga mambo kwa akili zako timamu, yatimize kama ulivyoyapanga bila kuruhusu chochote kukukwamisha.

Soma #BaruaYaKocha hapa; #BZK156; Bila Kuwa Na Huu ‘Ukatili’ Kamwe Hutaweza Kufanikiwa