Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Fikiria umeingia kwenye mchezo, ambao umeahidiwa zawadi pale unapokamilisha hatua za mchezo huo. Unacheza kwa kujituma sana, kwa sababu unajua zawadi iko mbele yako. Unakamilisha hatua zilizopo na unapewa zawadi ambayo uliahidiwa.
Lakini, baada ya muda mfupi unanyang’anywa zawadi hiyo na unaambiwa kama unataka uipate, tena ikiwa kubwa zaidi, unatakiwa urudi tena kwenye mchezo, ambao kwa awamu hiyo unakuwa mgumu zaidi.
Unaitaka sana zawadi na hivyo unarudi kwenye mchezo, mchezo unakuwa mgumu, lakini wewe unaangalia zawadi, unajisukuma na kukamilisha hatua zilizopo. Unapewa zawadi, ambayo kweli ni kubwa kuliko ya awali. Wakati unaifurahia, inachukuliwa tena, na unaambiwa kuipata unatakiwa kurudia tena mchezo.
Kufika hatua hiyo, wengi huwa wanaamua kuachana na mchezo moja kwa moja, na hapo ndipo wanapokwama kujenga na kudumu kwenye mafanikio makubwa.
Wengi wanachukulia mafanikio kama mchezo wa kucheza na kumaliza pale unapokuwa umepata ushindi. Hivyo wanakuwa tayari kujitesa wakiamini ni kwa muda mfupi tu.
Ni mpaka pale wanapopata ushindi ndiyo wanagundua kwamba mafanikio ni mchezo ambao hauna mwisho. Kwa kila ushindi unaopata, unakuwa ni mwanzo wa mchezo mwingine, ambao ni mgumu zaidi.
Kushindwa kutofautisha aina hizi mbili za mchezo kumewazuia wengi kufanikiwa. Na pia kumewafanya wengi kushindwa kufurahia maisha yao na hata hatua ambazo wanapiga.
Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia njia mbili za kucheza mchezo wa mafanikio. Achana na hizo aina mbili, za mchezo wenye ukomo na endelevu, zipo njia mbili za kuucheza mchezo wenyewe.

1. Kucheza Kwa Urahisi Au Kwa Ugumu.
Kuna njia mbili za kuishi maisha na kucheza mchezo wa mafanikio.
Njia ya kwanza ni kucheza kwa urahisi (easy mode). Hii ni njia ambayo watu wanaitumia pale wanapotaka kupata matokeo kwa haraka na bila ya kulazimika kuweka kazi kubwa. Hii ndiyo njia inayokimbiliwa na wengi wanaotaka mafanikio makubwa na ya haraka.
Njia ya pili ni kucheza kwa ugumu (hard mode). Hii ni njia ambayo watu wanaitumia pale wanapotaka kupata matokeo ambayo yatadumu kwa muda mrefu. Kwa njia hii, kazi inakuwa kubwa na inayochukua muda mrefu mpaka matokeo yaweze kupatikana.
Kucheza mchezo wa mafanikio kwa urahisi ni kutaka matokeo ya haraka na kumaliza mchezo. Ni kufikiri kwamba ukishapata matokeo umemaliza kila kitu. Kwa njia hii, mtu anatafuta njia za mkato na wakati mwingine zisizokuwa sahihi ili tu kupata matokeo. Kwa sehemu kubwa matokeo yamekuwa hayapatikana, na hata yakipatikana hayadumu kwa muda mrefu, kwa sababu ya njia inayokuwa imetumika.
Kucheza mchezo wa mafanikio kwa ugumu ni kutaka kuwa imara ili uendelee kucheza kwa muda mrefu bila kuacha. Ni kujua kwamba mchezo wa mafanikio hauna mwisho, na kufanikiwa siyo tu kupata matokeo, bali kudumisha matokeo hayo kwa muda mrefu. Kwa kuwa imara na kuendelea kucheza, unakuwa na uhakika wa kutokushindwa, kwa sababu hata usipopata matokeo unayotaka, unakuwa kwenye njia ambayo itakufikisha.
Dunia imewahadaa wengi kucheza mchezo wa mafanikio kwa urahisi, kutafuta vitu rahisi na vya haraka. Na hivyo ndivyo wamekuwa wanapotea pia. Wewe kaa kwenye mchezo sahihi, mchezo wa ugumu. Usikimbie magumu, jua kwamba yanakufanya imara ili uweze kuendelea na mchezo huo kwa muda mrefu.
2. Kuwa Tayari Kushindwa
Sisi binadamu huwa tunatabirika kirahisi sana. Kukiwa na njia mbili mbele yetu, moja rahisi na nyingine ngumu, huwa tunachagua njia rahisi. Na sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kuepuka kushindwa. Tunajua ugumu huwa unaambatana na kushindwa na huwa hatupendi kushindwa.
Moja ya kosa kubwa ambalo mfumo wa elimu umetufanyia ni kutufanya tukimbie kushindwa. Kwa kuwa kufeli mitihani shuleni kulionekana ni kitu kibaya, tumeenda na hilo kwa maisha yetu yote. Mambo mengi tunayofanya kwenye maisha, tunaepuka sana kufeli.
Hilo ndiyo limekuwa linawasukuma watu kuchagua kucheza mchezo wa mafanikio kwa urahisi. Kuchagua kile ambacho wanajua hawawezi kushindwa. Na ndiyo maana unaenda mahali na kukuta watu wote wanafanya kazi au biashara ya aina moja, kwa namna inayofanana. Kwa sababu ndiyo njia rahisi na ambayo mtu hawezi kushindwa. Japo wanaishia kwenye ushindani mkali na kutokupata matokeo.
Wanaofanikiwa wanakuwa tofauti, wanakuwa tayari kukabiliana na ugumu kwa sababu hawaogopi kushindwa au kufeli. Wanajua kutokupata matokeo siyo mwisho wa safari, bali ni sehemu ya safari yenyewe. Wao wanaendea kile wanachotaka, bila ya kujali kama ni rahisi au ngumu, kwa sababu wanajiamini kupata wanachotaka.
Wanaofanikiwa hawachukulii kushindwa au kufeli kama kitu cha aibu. Badala yake wanachukulia kama sehemu ya kujifunza na kuwa bora zaidi. Na wanajua wakiweza kuvuka kile kinachowakwamisha, watapata wanachotaka na hayo ndiyo mafanikio.
Wengi wanaokimbilia njia rahisi, hata wakipata kinachopatikana bado hawaridhiki, kwa sababu siyo mafanikio waliyokuwa wanayataka.
Epuka sana kubebwa na urahisi kwa sababu ya kuogopa kushindwa au kufeli. Mafanikio kwenye maisha siyo kutokushindwa, ni kupata kile hasa unachokuwa unataka. Na kupata unachotaka, lazima uvuke magumu yanayokuwa kwenye njia hiyo.
Soma #BaruaYaKocha hapa; #BZK155; Njia Mbili Za Kucheza Mchezo Wa Mafanikio Na Itakayokupa Mafanikio Ya Kudumu