Habari mpendwa rafiki na msomaji wa Amka Mtanzania? Natumaini unaendelea vema kiroho, kimwili na kiakili pamoja na kuifanya dunia kuwa sehemu salama kabisa kila mmoja wetu kuishi. Mimi na wewe tunatakiwa kuwa sehemu ya mabadiliko ambayo tunataka kuyaona katika dunia hii. Kama unataka maisha yako yabadilike kuwa sehemu ya mabadiliko na siyo kulalamika. Kama unataka watu wabadilike anza kubadilika kwanza wewe mwenyewe. Kama unataka kupata mtu/watu sahihi katika maisha yako kuwa mtu sahihi kwanza wewe mwenyewe utawapata watu/mtu sahihi katika maisha yako.
Hii ni sheria ya asili kabisa kwamba usitegemee kupata kile ambacho hukitoi. Utapata kile ambacho unatoa na kama unatoa haba utapokea haba wala usitegemee miujiza ya kupata vinginevyo.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza kwenye kitabu cha The DNA of Relationships(Vinasaba Vya Mahusiano).

Karibu ndugu msomaji, katika somo letu la leo ili tuweze kuongeza maarifa katika ubongo wetu kwani maarifa ni hazina ya kuishi maisha sahihi hapa duniani. Na zifuatazo ni tabia nane zinazodhoofisha mahusiano yako ya ndoa, uchumba kutokua na furaha na mengine;

1. Kukosoa; Tabia ya kukosoa ni mbaya sana katika mahusiano yoyote yale. Kwa mfano, unaweza kua katika mahusiano mazuri na rafiki yako halafu huyo rafiki yako yeye ni mtu wa kukosoa tu yaani hathamini kile ambacho unafanya ukifanya kitu kizuri hapongezi bali yeye anatafuta mabaya tu ili aweze kukukatisha tamaa usisonge mbele. Kila mtu anahitaji pongezi pale anapokua amefanya kitu kizuri kutoka kwa watu wake wa karibu na sasa kama wewe una tabia ya kukosoa acha mara moja.
Hatua ya kuchukua; Kabla hujaanza kumkosoa mwenzako kwa kitu alichofanya jiulize je wewe ulishawahi kufanya nini ukakosolewa? Kwa sababu kuna watu wengine wao hawajawahi kufanya chochote katika hii dunia na kuifanya kuwa sehemu salama ya kuishi tokea Mungu aiumbe dunia. Bali kuna watu wako kwa ajili ya kuharibu tu na kukosoa. Hivyo kama una watu kama hawa katika maisha yako wakimbie na usiwashirikishe mipango yako kwani watakuwekea ukungu wa kutokuona mbele.

SOMA; Vikwazo Vitano(5) Vinavyoharibu Mahusiano Yetu Na Ndoa Zetu Na Jinsi Ya Kuviepuka.

2. Kulalamika; Kulalamika imekua desturi sana katika maisha ya leo kila mahali wamejaa walalamikaji. Mfano, labda katika ofisi Fulani kiongozi mlalamikaji, wafanyakazi wake wote walalamikaji yaani ukianzia getini unaanza kupokewa na walalamikaji. Sasa tabia kama hii inadhoofisha mahusiano yetu kabisa. Utamaduni wa kulalamika hovyo bila kuchukua hatua huwa unazaa wavivu wengi sana. Kama wewe uko katika mahusiano ya ndoa, uchumba, urafiki na mengine acha tabia ya ulalamikaji kabisa.
Hatua ya kuchukua; Kama kuna kitu unaweza kukibadilisha ambacho kipo ndani ya uwezo wako basi ukibadilishe na kama kipo nje ya uwezo wako nyamaza usilalamike. Muda unaotumia kulalamika chukua hata kitabu soma ukurasa mmoja utapata tumaini la maisha.

 

3. Kulaumu; Maisha ya kulaumu ni maisha ambayo hayana furaha. Sasa kama wewe muda mwingi unautumia katika kulaumu utapata wapi furaha? Kuna watu wanajilaumu kila siku kulingana na mambo waliyofanya hapo awali, kuwalaumu wengine kwa nini kitu Fulani hakipo hivi au kimeenda vile. Usilaumu, maisha ya kulaumu ni maisha hasi hayo ambayo yanaziba fursa na baraka nyingi katika maisha yako.
Hatua ya kuchukua; usiwe mtu wa kulaumu katika maisha yako kama jambo limetokea limeshatokea huwezi kulibadili tena bali chukua hatua kwa wakati wa sasa na acha kulaumu vitu vya wakati uliopita. Mwingine analalamika hata jinsi alivyoumbwa na huwezi kujibadilisha jinsi ulivyoumbwa kama umejikuta umeumbwa jinsi ulivyo basi jipokee jinsi ulivyo ili uishi maisha ya furaha.

4. Kukosa uvumilivu; Maisha ya mafanikio yanahitaji uvumilivu. Kama uko kwenye uhusiano wa ndoa mnatakiwa kuvumiliana kama mlivyoweka agano lenu siku ya kwanza. Mkiwa mnaishi maisha ya kujifananisha na watu wengine hakika mtakata tamaa ya maisha na hatimaye kila mmoja wenu kuingia na hali ya kukosa uaminifu katika maisha ya ndoa. Uvumilivu wenu katika maisha ya ndoa utazaa matunda mazuri sana kama kila mmoja katika nafasi yake akiwajibika ipasavyo. Kama kila mmoja akikwepa majukumu katika nafasi yake basi hakika hawezi kukwepa matokeo atakayopata katika nafasi yake.

SOMA; Umuhimu Wa Mawasiliano Katika Kujenga Mahusiano Bora Ya Kijamii.

5. Kutosamehe; Kwanza muasisi wa msamaha ni Mungu mwenyewe. Sasa wewe binadamu uliyeumbwa na huyo Mwasisi Huyo kwa nini hutaki kusamehe? Hujui kusamehe ni kuponya majeraha ya nafsi? Maisha ya ndoa nyingine yamejaa kutosameheana kila mtu kashika hamsini zake maisha ya ndoa kati ya wawili hao hatimaye yanakua hayana furaha. Mtunga zaburi anasema, kama Bwana angehesabu makosa yetu nani angesimama? Hakuna hata mtu angeweza kusimama. Lakini Mungu mwenye huruma anatusamehe kwa nini wewe hutaki kumsamehe mwenzako? Kutokusamehe kunadhoofisha mahusiano yoyote yale katika maisha yetu ya kila siku. Na kama tukisameheana tunarudisha uhusiano wetu uliovunjika awali. Unarudisha upendo wa awali uliopotea.
Hatua ya kuchukua; kila siku ni zawadi kutoka kwa Mungu. Unatakiwa kusamehe kila siku ya Mungu katika maisha yako. Kusamehe ni kumfutia mtu deni, je una madeni mangapi mpaka sasa ya kutosamehe? Inuka nenda kasamehe leo usisubiri kesho kwani hujui kama kesho utakua hai au la hivyo usikubali kufa huku ukiwa na deni la kutosamehe. Ndugu, kama una madeni ya hela unadaiwa, je hata madeni ya kutokusamehe unashindwa kulipa?

6. Mabishano; mabishano yanaleta fedheha katika mahusiano yetu. Wanaobishana kila mmoja anataka akubalike kama yeye ndio bora kuliko mwenzake. Sasa hali hii inawafanya hata watu kuingia katika hali ya magomvi na hatimaye kusababisha mauti. Watu wakiwa katika mabishano husababisha ugomvi, hasira, huleta visasi na hatimaye chuki ambayo chuki huzaa mauti.
Hatua ya kuchukua; epuka mabishano katika mahusiano yoyote uliyonayo sasa hivi kama ni ndoa, urafiki, uchumba nakadhalika.

7. Kumdhibiti au kumtawala mwenza wako; kila binadamu ana tabia yake hapa duniani. Ni ngumu sana kumdhibiti mwenzako ambaye ulishamkuta na tabia ambazo tayari anazo. Kila mtu anapenda uhuru katika maisha yoyote yale. Usimtawale mwenzako kama mtoto mdogo vile yaani afanye vile unavyotaka wewe. Matatizo mengi huwa yanaanzia hapa ambapo kila mmoja anataka kumtawala mwenzake. Wanaume wengi hupenda kuwatawala wenza wao na kutowapa uhuru katika maisha yao ndio maana matatizo hayaishi. Muelewe mwenzako na anataka nini na siyo kumkataza kila kitu kama mtoto kwani kila mtu anatakiwa kuwa na uhuru lakini pia haijalishi uko kwenye ndoa au la kila mtu ana thamani yake ambayo anatakiwa kuitoa katika hii dunia kabla hajafa. Sasa kwa nini unataka mwenzako afe na hazina aliyokua nayo ambayo bado hajaitoa duniani?

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha Law Of Attraction

8. Vitisho; maisha ya vitisho siyo maisha ya kuishi. Mke anatoa vitisho kwa mume wake vivyo hivyo kwa watoto. Mahusiano hayawezi kuimarika kwa kupeana vitisho kila siku. Maisha ya vitisho ni maisha ambayo yamejaa hofu. Kwanini tusiponye mahusiano yetu na tuondoe hofu iliyotawala katika mahusiano yetu? Mahusiano yamejaa hofu baba anawajaza watoto hofu, viongozi wanawajaza watu wanaowaongoza hofu hivyo maisha yamegeuka kuwa hofu badala ya furaha. Maisha ya vitisho yanafanya dunia kuwa si sehemu salama ya kuishi. Maisha ya vitisho yanaharibu thamani au hazina walizo nazo watu katika kuifanya dunia kuwa bora zaidi.
Mwisho, maisha ni furaha, upendo, amani, muda, uhuru. Kila mmoja wetu atumie nafasi yake kuifanya dunia kuwa bora na salama kwa kila mmoja wetu kuishi. Wawezeshe wenzako kupata kile wanachokitaka kwanza, na wewe utapata usiwe na ubinafsi kabisa kama ingekua watu wengine ni wabinafsi sidhani kama dunia ingekua hivi ilivyo leo. Mabadiliko ni mimi na wewe.