Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa The Psychology of Money: Timeless Lessons on Wealth, Greed, and Happiness kilichoandikwa na Morgan Housel

Fedha ndio kitu pekee kinachotuleta pamoja binadamu wote duniani, kama fedha ingekuwa dini, basi ndiyo dini pekee ambayo kila mtu duniani anaiamini. Watu watatofautiana kwenye mambo mengine yote, lakini kwenye fedha watakubaliana.

Lakini watu wamekuwa wanakabiliana na changamoto nyingi mno inapokuja kwenye swala la fedha. Changamoto nyingi ambazo watu wanapotia kwenye maisha, mzizi wake mkuu ni fedha. Iwe ni kwenye afya, kazi, biashara na hata mahusiano, fedha ina mchango mkubwa.

Pamoja na umuhimu mkubwa ambao fedha inao na pamoja na kugusa kila eneo la maisha yetu, bado watu wengi hawana uelewa sahihi wa fedha na hilo limekuwa chanzo cha matatizo zaidi ya kifedha.

Morgan Housel kupitia kitabu hiki cha The Psychology of Money anatuambia kwamba tatizo la fedha siyo kile tunachojua kuhusu fedha, bali tabia zetu binafsi inapokuja kwenye fedha. Hivyo matatizo makubwa ya kifedha ambayo watu wanapitia kwenye fedha, siyo kwa sababu hawajui bali kwa sababu tabia zao zinawaangusha.

Chukua mfano wa kuweka akiba na kuwekeza, hakuna mtu mzima anayeweza kutafuta kipato asiyejua umuhimu wa kuweka akiba kwa ajili ya baadaye. Lakini ni wachache sana wanaoweza kufanya hivyo. Hiyo ni kwa sababu tabia ambazo watu wanazo inapokuja kwenye fedha, ndiyo zinawakwamisha.

Kufundisha maarifa ya kawaida ni rahisi, lakini kufundisha watu tabia mpya ni kitu kigumu, hata kwa wale ambao wana uwezo mkubwa wa kujifunza na kuelewa, kujifunza tabia siyo kitu rahisi.

Kupitia kitabu hiki cha The Psychology of Money tunakwenda kujifunza chimbuko la tabia tulizonazo inapokuja kwenye fedha na namna sahihi ya kuzibadili ili tuweze kuondokana na changamoto mbalimbali za kifedha tunazopitia.

Kwenye kitabu hiki, Morgan ametushirikisha hadithi 19 kuhusu tabia za watu mbalimbali kwenye fedha na matokeo waliyopata. Kupitia hadithi hizo, unaweza kujifunza hatua sahihi kwako kuchukua inapokuja kwenye fedha.

UTANGULIZI; ONYESHO KUBWA ZAIDI DUNIANI.

Nguzo kuu ya kitabu hiki cha The Psychology of Money ni kwamba kufanya vizuri kifedha haihusiani na una akili kiasi gani, bali inategemea na tabia ulizonazo. Na tabia ni kitu kigumu kufundisha, hata kwa wale wenye akili sana.

Ndiyo maana watu wengi wenye akili sana, wanaoweza kung’amua mambo magumu, inapokuja kwenye fedha, huwa wanafanya mambo ya kijinga kabisa ambayo watu wanaweza kushangaa.

Hata wale ambao wamesomea mambo ya fedha na wanajua kila kitu kuhusu misingi ya kifedha, bado kwenye fedha zao binafsi huwa hawafanyi vizuri. Hivyo hilo linaonesha ni kwa namna gani tabia zilivyo na mchango.

Kwa upande wa pili, ukiwaangalia wengi ambao wanafanya vizuri kifedha, huwa ni watu ambao hawana elimu kubwa au akili sana. Ni watu wa kawaida ambao wana tabia nzuri inapokuja kwenye fedha.

Kuna watu ambao huwa wanaonekana wana maisha ya kawaida kabisa lakini siku wakifariki ndiyo inakuja kugundulika kwamba walikuwa na utajiri mkubwa. Watu hao siyo wanakuwa wanaigiza maisha, bali tabia zao ndiyo zinakuwa zimewajengea utajiri mkubwa na kuwaepusha na mambo ambayo yangekuwa kikwazo kwao.

Mafanikio ya kifedha siyo sayansi ngumu ambayo inahitaji akili na uwezo mkubwa kuielewa. Ni sayansi na sanaa ya kawaida kabisa, ambayo inategemea zaidi tabia zako kuliko unachojua.

Kwa kifupi, fedha zinaathiriwa zaidi na saikolojia ya mtu kuliko akili yake. Ndiyo maana kitabu hiki kinagusa kwenye saikolojia, maana hapo ndipo tabia zetu zilipo.

Lengo la kitabu hiki ni kutumia hadithi fupi kutushawishi kubadili tabia zetu na kujenga tabia ambazo zitatusaidia kufanikiwa kifedha.

Mada mbili zinazomgusa kila mtu.

Kuna mada kuu mbili ambazo huwa zinamgusa kila mtu bila kuacha yeyote. Mada hizi ni fedha na afya. Kila mtu huwa ana maoni yake na tabia zake inapokuja kwenye mada hizo.

Sekta ya afya imeweza kukua sana kwa miaka 100 iliyopita. Ugunduzi wa dawa na teknolojia mbalimbali umeweza kuongeza umri wa watu kuishi duniani. Hivyo tunaweza kusema, ongezeko la maarifa kwenye sekta ya afya, limekuwa na matokeo chanya kwa watu.

Lakini sekta ya fedha, licha ya kuongezeka kwa maarifa mengi kuhusu uchumi, fedha na uwekezaji, bado hakuna mabadiliko makubwa kwenye maisha ya watu inapokuja kwenye fedha. Bado masoko ya hisa yanakua na kuanguka, bado watu wanapata fedha na kuzipoteza.

Kinachopelekea maarifa ya kifedha yasiweze kuwabadili watu ni kwa sababu tunaweka mkazo kwenye kanuni na sheria badala ya tabia na hisia ambazo ndiyo zinazowasukuma watu kufanya maamuzi yao ya kifedha.

Kwa nini watu wanatofautiana kwenye fedha.

Kwenye sayansi, kanuni ikishathibitishwa, huwa inakuwa kweli kwa watu wote. Hakuna anayeweza kuipinga kanuni ambayo imethibitishwa kufanya kazi.

Lakini inapokuja kwenye fedha, kila mtu huwa ana maoni yake na hakuna kanuni moja ambayo watu wote wanakubaliana nayo.

Kwa kuwa fedha zinagusa maisha ya kila mtu na kwa kuwa kila mtu ana mtazamo wake inapokuja kwenye fedha, mwandishi anaita hali hiyo ni onesho kubwa zaidi duniani.

Katika onesho hili, kila mtu anafanya kile ambacho kwake ni sahihi, hata kama kwa wengine kitaonekana ni cha ajabu kabisa.

Inapokuja kwenye fedha, kila mtu anafanya maamuzi ambayo kwa uelewa wake ni sahihi kabisa kwake. Wewe kwa nje unaweza kushangaa na kuona mtu huyo anakosea, lakini ndani yake anajua anachofanya ni sahihi.

Hiyo ni kwa sababu huwezi kuona saikolojia ya mtu, huwezi kujua tabia na hisia alizonazo wakati anafanya maamuzi hayo. Hivyo japo kwako yataonekana ni ya hovyo, kwake na kwa wakati huo, yatakuwa ni sahihi kabisa.

Kujua kinachowasukuma watu kufanya maamuzi.

Kama unataka kujua kinachowasukuma watu kuchukua mkopo wenye riba kubwa na unaowaumiza huhitaji kujua kiwango cha riba na madhara yake, bali unapaswa kujua historia ya tamaa, hofu na matumaini. Kila mtu anajua riba inaumiza, lakini pale mtu anapokuwa na tamaa ya kupata kitu, haangalii riba wakati wa kufanya maamuzi, anachotaka ni kutimiza haja yake.

Kama unataka kujua nini kinawasukuma watu kununua uwekezaji wakati bei yake iko juu na kuuza wakati bei yake chini (na hivyo kupata hasara) huhitaji kujifunza kuhusu makadirio ya faida zijazo, bali unapaswa kujua uchungu wa mtu kuiangalia familia yake na kuona inapoteza kila kitu. Kila mwekezaji anajua kununua kwa bei juu na kuuza kwa bei chini ni hasara, lakini pale mtu anapoona hatari ya kupoteza kila kitu, anaona ni bora apate hasara kidogo kuliko kupoteza kabisa.

Makosa 20 tunayofanya kwenye fedha.

Kwenye kitabu hiki, tunakwenda kujifunza makosa 20 ambayo watu wamekuwa wanayafanya kwenye maamuzi yao ya kifedha na kuona jinsi ambayo makosa hayo yanavyochochewa na tabia na hisia za watu na siyo maarifa au ujuzi walionao kuhusu fedha.

Kitabu kina sura 20 na kila sura inaelezea kosa kupitia hadithi fupi ambayo inatuonesha jinsi tabia na hisia zinavyokuwa chanzo cha changamoto za kifedha.

Karibu usome uchambuzi

Karibu sana usome uchambuzi kamili wa kitabu hiki, ujue makosa ambayo umekuwa unayafanya kifedha na yanakugharimu.

Uchambuzi kamiliwa wa kitabu hiki unapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA. Kuupata karibu ujiunge na channel hiyo kwa kufungua kiungo hiki na kubonyeza JOIN CHANNEL. Kiungo; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.