Kuwa na mtazamo chanya katika maisha yako ni kitu ambacho unalazimika kuwa nacho ili kukabiliana na changamoto nyingi za maisha zinazojitokeza karibu kila siku. Bila kuwa na mtazamo chanya itakusababisha wewe kukata tamaa mapema katika mambo mengi yanayojitokeza kwako hususani yale ya kukatisha tamaa.
Kwa bahati mbaya wengi wetu pengine kutokana na malezi, mazingira au tabia ni watu wa mitazamo hasi sana ambayo inatupelekea  kukwama katika mambo mengi. Siri  kubwa ya kushindwa au kufanikiwa kwako ipo kwenye mitazamo uliyojiwekea. Kwa mfano, inapotokea umeshindwa katika jambo fulani, huwa unachukulia vipi kushindwa huko kunakojitokeza kwako?
Kama una tabia ya kuchukulia kushindwa huko ni kitu kibaya sana na kushindwa kuangalia kwa jicho lingine basi ni rahisi sana kwako kuweza kukata tamaa. Kwa sababu kila kitu utakuwa unakiona kibaya kwako na hata lile jambo ambalo unakuwa unaliweza, inakuwa ni ngumu kufanikiwa kwa sababu ya mtazamo hasi ulionao.
Je, unaweza vipi kujijengea mitazamo mingi chanya ili iweze kukusaidia kuishi maisha ya mafanikio?
1. Kaa karibu  na watu chanya.
Hawa ni watu ambao watakusaidia kukupa mtazamo chanya katika mambo yako mengi kimaisha. Itakuwa siyo rahisi wao kuweza kukukatisha tamaa, zaidi watakutia moyo hata pale mipango na malengo yao inapokuwa haiendi vizuri. Hii ni njia mojawapo sahihi ya kuweza kukujengea mitazamo chanya katika maisha yako.
2. Jifunze kila siku.
Ni muhimu kujifunza kila siku ili kujijengea mawazo bora yatakayokusaidia uweze kujiamini na kujenga mtazamo chanya. Mambo au vitu unavyotakiwa kujifunza  ni yale mambo chanya kwako na siyo zile habari ambazo zitakuwa zinakupa hofu nyingi za kimaisha. Kwa kadri unavyozidi kuilisha akili yako mambo mengi chanya ndivyo ambavyo itazidi kuwa chanya na kukupa mtazamo wa tofauti.
3. Anza siku yako vizuri.
Ili kujijengea tabia hii kwa urahisi, ni vyema ukaianza siku yako kila siku kwa kujilisha mambo chanya kwanza. Kila unapoamka asubuhi anza kwa kujisomea ili kuijengea akili yako misuli itakayokusaidia kujenga mitazamo mingi  chanya kuliko ambavyo ungeamka na kuanza kusoma gazeti au kusikiliza habari ambazo mara nyingi huwa ni hasi.
4. Badili mitazamo yako.
Kama katika maisha yako mambo yako mengi unakuwa unayaangalia kihasihasi ni muhimu kulijua hili na kubadili mitazamo hiyo  mara moja. Mara nyingi wengi wetu huwa ni watu wa kutazama mambo mengi katika mitazamo hasi sana hali ambayo huweza kupelekea sisi kuweza kukwama katika mambo yetu mengi. Lakini ukija kuangalia kinachotukwamisha siyo kitu kingine zaidi ya mitazamo yetu hiyo.
5. Jenga tabia ya kufanya mambo yako sasa.
Acha kujitengenezea tabia ya kuahirisha mambo yako mara kwa mara. Jijengee tabia ya kufanya mambo yako sasa. Kama kuna kitu ulitakiwa kukikamilisha kikamilishe sasa kuliko ambavyo unataka kukifanya kwa baadae. Kwa hali hiyo itakusaidia kujijengea mitazamo chanya sasa kwa yale mambo ambayo uliyachukulia kuwa huyawezi kumbe unayaweza kabisa.
6. Kuwa mtu wa shukrani.
Kama kitu umekifanisha hata kama ni kidogo vipi shukuru kwa hicho kwanza. Acha kusubiri mpaka ukamilishe mambo makubwa ndiyo uwe na shukrani. Hata ikitokea umefanyiwa kitu fulani kizuri na mwenzio ni vizuri pia kushukuru. Hiyo itakusaidia sana katika suala zima la kukujengea mtazamo chanya katika maisha yako.
Ili tuweze kujihakikishia mafanikio makubwa na ya kudumu suala la kuwa a mtazamo chanya katika maisha yetu ni jambo ambalo halikwepeki. Ni lazima kwetu kujijengea mitazamo hii kila siku ili kufanya mipango yetu kwa uhakika na ufanisi zaidi bila hofu ya kushindwa.
Tunakutakia ushindi katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kujifunza kila siku.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika zaidi.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,