Habari mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA na karibu tena katika makala yetu ya leo.
Wiki iliyopita nilifanikiwa kusoma makala ya rafiki na kocha wangu Makirita Amani hakika nilifurahishwa na makala hiyo ambayo ilikuwa inasema USIOMBE RUHUSA OMBA MSAMAHA, aliandika hivi kama wewe ni kijana una miaka zaidi ya 21 na bado unakaa nyumbani yaani akimaanisha bado hujaanza kujitegemea ondoka haraka nyumbani na nenda kaanze maisha ya kujitegemea. Ndio katika maisha kujitegemea siyo kujitosheleza ni bora uanze kujitegemea mapema pale ambapo hujitoshelezi ndio uombe msaada lakini tayari umeanza kujitegemea na uko kwako kuliko kuomba msaada wakati bado hujaanza kuchukua hatua. Kama hukusoma makala hiyo isome hapa; Usiombe Ruhusa, Omba Msamaha.

 
Katika hali ya kawaida watu wengi hususani jamii yetu ya Kitanzania vijana wengi wanashindwa kuchukua hatua mapema katika maisha yao kwa sababu tu ya mfumo tuliouzoea na kisingizio kikubwa bado wanajipanga na kujipanga siku zote hakutimii ni bora uingie katika mapambano kuliko kujifunza nje ya mapambano.
Hivi karibuni nimekuwa nafanya kazi na jamii ya watu wa marekani ni mambo mengi niliyojifunza kwanza ni jamii ya watu wanaojali muda, pili nilishangazwa na mmoja wa rafiki yangu kutoka marekani kwa kuniambia kwamba jamii ya kwao huwa wanafurahia na kufanya sherehe kwa kufikisha umri wa miaka 18. Nikamuuliza kwa nini? Akanijibu ili awe na uhuru na kuanza kujitegemea, nikamuuliza swali unawezaje kuanza maisha ya kujitegemea na huna pesa?
Akanijibu kutoka katika akiba yake aliyojiwekea kipindi anasoma. Nikajifunza kumbe wenzetu wanapenda kujitegemea bado wakiwa wadogo na wanafurahia kuondoka nyumbani je jamii yetu tunafanya hivi au ndio tunakimbia majukumu ya kujitegemea? Ni wangapi hapa Tanzania wana zaidi ya miaka 21 bado hawajaanza kujitegemea?
Ndugu mpenzi msomaji, karibu tujifunze kwa nini usiombe ruhusa na uombe msamaha. Na zifuatazo ni sababu 11 kwa nini usiombe ruhusa na uombe msamaha;
1. Ili Usikatishwe Tamaa; katika hali ya kawaida ukijaribu kufanya jambo ambalo linaweza kukuletea mafanikio na ukiomba ruhusa lazima utakatishwa tamaa, utaambiwa vikwazo vingi badala ya kupewa msaada katika jambo hilo. Lakini kama umejiunga na kundi la waasi wa mema ndio njia pekee ya kufikia kile tunachotaka katika maisha yetu.
SOMA; Hivi ndivyo unavyoua ndoto zako kubwa za mafanikio.
2. Ujifunze ; siku zote mtu anayejaribu anajifunza sana kuliko yule mtu ambaye hajaribu. sasa ukiwa mtu wa kuomba ruhusa kwa kila kitu utajifunzaje? Ndio maana unashauriwa kuomba samahani kuliko ruhusa ili uweze kujifunza uingie kwenye mapambano ya dunia.
3. Uweke Historia; ukitaka mafanikio hapa duniani basi thubutu kufanya bila ya kupewa ruhusa kwa wazazi, walezi au ndugu. Ukifanya jambo zuri nao wakilikubali baadae watakuheshimu sana na utakuwa umejenga historia kubwa. Maisha ni muda na maisha ni marefu kama ukitumia vizuri muda wako. Sasa kama maisha ni muda kama mpaka sasa bado hujaanza mchakato au harakati za kujikomboa unasubiri nini? tumia vema rasilimali ya ujana ambayo ni nguvu na muda utaokoa maisha yako ya uzeeni.
4. Uweke Heshima; utapata heshima kutoka kwa jamii, ndugu, wazazi, jamaa na marafiki kama ukifanya jambo ambalo litagusa maisha ya watu wengine. Ili upate heshima amka sasa na nenda kapambane wewe tayari ni mshindi bado kukabidhiwa kombe tu na huwezi kukabidhiwa kombe ukiwa umelala inabidi uamke na uende kwenye mapambano.
5.Ujenge Nidhamu Binafsi; Nidhamu ndio kila kitu katika maisha yako ili uweze kufikia mafanikio yoyote yale hapa duniani. Kama umepanga kuamka saa 11 ujisomee uongeze maarifa ulishe ubongo wako chakula cha asubuhi, huwezi kuamka kama huna nidhamu. Kwa hiyo nidhamu ndio kila kitu lenga kuwa na nidhamu itakukomboa katika kila idara hapa duniani na kumbuka nidhamu haiji kwa kuomba ruhusa jiongoze na jisimamie mwenyewe utapata matokeo chanya na siyo hasi.
6. Ukumbane na Changamoto; Hakuna maisha bila changamoto, kila mtu hapa duniani ana changamoto zake, kwa hiyo changamoto zitakufanya ukue na ukomae kama huna changamoto basi wewe hujaribu kufanya mambo makubwa unafanya kile ambacho kila mtu anafanya. Na wakati mwingine changamoto zinaweza kukufanya kuwa mjasiriamali bora kwa sababu utaziona fursa, kama hujaribu basi huwezi kuziona fursa kwa jicho la tatu jaribu leo na usikate tamaa.
SOMA; Je Haya Unayoishi Ndio Maisha Yako Halisi?
7. Utajijengea Uhusiano Mzuri na Jamii; kama unaweza kufanya mambo mema basi jamii iliyokuzunguka itakuwa imenufaika katika kile unachofanya jamii itaonja mchango wako na hivyo utakuwa umejijengea uhusiano mzuri na jamii. Ili ufanikiwe unatakiwa ujenge uhusiano mzuri na jamii na huwezi kufanikiwa bila watu.
8.Utajijengea Falsafa ya Maisha Yako; watu wengi wanaishi lakini wanaishi katika falsafa za maisha ambazo siyo zao. Kwa hiyo ni vizuri kujijengea falsafa ya maisha yako mwenyewe hapo utaishi maisha ya furaha. Usikubali kuishi maisha ya furaha ya kununua ishi maisha ya furaha ya asili. Mfano wa furaha ya kununua ambayo ni ya muda mfupi ni kama vile kuvuta sigara, kutumia vilevi ili upate furaha tu ya muda mfupi tafuta furaha ya kudumu na ya asili acha kuwa mtumwa wa kutafuta furaha ya kununua kila siku.
9.Utajijengea Uwezo wa Kufikiri; kuna tofauti kati ya kufikiri na kuwa na mawazo, kufikiri ni kutafuta jawabu chanya katika maisha yako na kuchukua hatua. Mfano hali uliyo nayo sasa huridhishwi nayo kwa hiyo utachukua hatua chanya ya kukabili tatizo. Kama wewe ni binadamu na uko hai basi usiache kufikiri na kujifunza kwani kile ambacho hukijui huwa kinakufanya uwe masikini.
10. Utajijengea Juhudi na Maarifa; ukifanya kazi kwa juhudi na maarifa utajijengea ufanisi na utakuwa shujaa na shujaa ni alama ya ushindi. Jaribu kuthubutu kila siku usisubiri mpaka uombe ruhusa wewe fanya uje uombe msamaha baadaye.
11.Utaziona Fursa; Bilionea Richard Branson anasema fursa ziko kama magari barabarani moja linakwenda na lingine linarudi. Kama wewe umekaa tu huwezi kuziona fursa na bahati hutokea pale fursa inapokutana na maandalizi. Acha kulalamika chukua hatua utaziona fursa nyingi sana katika jamii yako iliyokuzunguka.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com