Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kila binadamu aliye hai ana ndoto kubwa kuliko maisha anayoishi. Hata wale ambao tayari wanaonekana wamefanikiwa, bado wanakuwa na ndoto wanazopambana kuzifikia.

Kwa bahati mbaya sana, maisha yamekuwa hayatupi kwa urahisi chochote tunachokuwa tunakitaka. Kuna vikwazo na changamoto nyingi ambazo kila mtu huwa anakutana nazo wakati anapambania ndoto zake.

Kila mtu huwa anaanza na ndoto kubwa anazokuwa nazo. Lakini wanaopambana mpaka kuzifikia huwa ni wachache. Wengi huishia kukata tamaa na kukubali maisha ya kawaida kutokana na magumu wanayokutana nayo.

Imekuwa inaonekana kama wachache sana wanaofanikiwa wana bahati ya kipekee na wengi wasiofanikiwa wanaikosa. Lakini hiyo siyo kweli, ndiyo, kuna tofauti ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa, ila haitokani na bahati.

Tofauti ya wanaofikia ndoto zao na kupata mafanikio na wale wasiofanikiwa ni kwenye matumizi ya nguvu kubwa zilizo ndani ya kila mtu. Wanaofanikiwa ni wale wanaotambua nguvu kubwa waliyonayo na kuitumia. Wanaoshindwa hawajui kama wana nguvu kubwa ndani yao, hivyo wanakubali kukwamishwa na chochote kinachoingilia njia zao.

Wewe rafiki yangu umekuwa na bahati ya kupata mwongozo sahihi juu ya mambo yote yanayohusu mafanikio yako makubwa. Kupitia #BaruaZaKocha umekuwa unapata uelewa wa yale ya kufanya na ya kuepuka ili uweze kujenga maisha unayoyataka.

Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujua na kutumia nguvu kubwa iliyopo ndani yako ili ufikie ndoto kubwa ulizonazo. Ndiyo, wewe hapo una nguvu kubwa sana iliyo ndani yako na ambayo hujaanza kuitumia. Ni wakati sasa wa kufungulia nguvu hiyo ili usikwamishwe na kitu chochote.

1. Sauti Mbili Zilizo Ndani Yako.

Sisi binadamu huwa tunafanya maamuzi yetu kwa kusukumwa na hisia mbili kuu; hofu ya kupoteza na tamaa ya kupata. Tunapenda kujiona kwamba tunafanya maamuzi kwa mantiki, kwa kufikiri, lakini hatuna uwezo huo. Maamuzi yetu yanaanza na hisia kwanza, kisha tunayahalalisha kwa mantiki. Tunasukumwa kuamua pale tunapokuwa na kitu cha kupoteza au cha kupata.

Hisia hizo mbili ni matokeo ya nje, ambayo mzizi wake upo kwenye sauti kubwa mbili ambazo zimekuwa zinaendesha maisha yetu.

Ya kwanza ni sauti ya kuishi au kusalimika. Hii ni sauti inayohakikisha sisi binadamu tunaepuka mambo yote ambayo yanaweza kukatisha uhai wetu. Sauti hii hufanya kazi kubwa ya kututahadharisha na hatari mbalimbali zinazoweza kuathiri maisha yetu. Sauti hii ndiyo huwa inachochea hisia za hofu ya kupoteza.

Ya pili ni sauti ya kukua au kufikia ndoto tulizonazo. Hii ni sauti inayotusukuma kufanya mambo makubwa kwenye maisha yetu. Sauti hii inatuonyesha makubwa tunayoweza kufanya au kufikia na kutusukuma tuyaendee.

Kwa kujua sauti hizo mbili, unaweza kuona wazi kwamba sauti ya kukua ndiyo tunayopaswa kuisikiliza zaidi. Lakini kwenye uhalisia, sauti ya kuishi huwa ina kelele kubwa kuliko ya kukua. Matokeo yake ni tunaishia kusikiliza sauti ya kuishi zaidi huku tukikandamiza sauti ya kukua.

Sauti ya kuishi ilikuwa muhimu kwa binadamu wa kale, ambao waliishi kwenye mazingira hatari. Lakini kwa sasa tunaishi mazingira yenye usalama mkubwa, na bado sauti hiyo inatufanya tuone kama tuna hatari kubwa.

Nguvu kubwa uliyonayo ya kukufikisha kwenye ndoto zako kubwa ni kuacha kusikiliza sauti ya kuishi na kuanza kusikiliza sauti ya kukua. Haitakuwa rahisi, kwa sababu siyo mazoea yetu, lakini ni kitu kinachowezekana.

2. Ondoa Msumari Ulio Kichwani Kwako.

Ili uweze kuendea ndoto zako na kufanikiwa, kitu cha kwanza kushughulika nacho ni hofu. Hofu ni kitu ambacho hakipo, ni fikra tunazokuwa tumetengeneza sisi wenyewe, kutokana na sauti ya kuishi ambayo tumeipa nguvu kubwa.

Huwa wanasema hofu kwa kiingereza ni kifupisho cha ushahidi wa uongo unaoonekana kuwa wa kweli (FEAR; False Evidence Appearing Real). Hii ina maana kubwa sana, kwamba hofu haipo popote isipokuwa kwenye fikra zetu pekee.

Na huo ndiyo msumari ambao umekuwa unakukwamisha wewe kufikia ndoto kubwa ulizonazo. Kila unapofikiria kuanza ndoto zako, hofu inakuonyesha vitu ambavyo hata havipo kabisa. Na kwa sababu sauti ya hofu ni kali na inayojirudia rudia, huwa ni rahisi kuaminika.

Kila unapopanga kufanya kitu chochote kikubwa, utaona njia za kushindwa. Utajiona hujawa tayari. Utaziona hatari mbalimbali ambazo zitakukwamisha. Lakini hapo unakuwa hujaanza, hivyo chochote unachofikiria hakipo.

Kuondoa msumari ulio kichwani kwako ni kuainisha mambo yote ambayo unayahofia kama utaziendea ndoto zako. Badala ya kuacha tu fikra hizo zikae kwenye kichwa chako na kukukwamisha, ziweke wazi.

Andika chini mambo yote ambayo unayahofia yatatokea kama utaziendea ndoto zako, kama utapambana kufanikiwa. Na kwa kila jambo utakaloandika, jiulize kama kweli litatokea, ndiyo utakuwa kabisa mwisho wa maisha yako?

Kitu kimoja utakachoona ni kwamba hata kama hayo unayohofia yatatokea, maisha hayatakuwa yameisha. Maisha yataendelea na utapata nafasi ya kufanya tena. Na hapo ni kama yatatokea, maana kwa sehemu kubwa mengi unayohifia hayatatokea.

Soma #BaruaYaKocha hapa; #BZK152; Tumia Hii Nguvu Kubwa Uliyonayo Kufikia Ndoto Kubwa Ulizonazo