Katika mazingira yanayofanana na kwa nyakati zinazofanana, kuna watu wanafanikiwa sana huku wengine wakishindwa kabisa. Ni kitu gani kinawatofautisha hawa wanaofanikiwa na wale wanaoshindwa? Hili ni swali la dola bilioni moja, yaani ni swali lenye thamani kubwa, ambalo limekuwa linajibiwa na vitabu vingi ambavyo vimeandikwa kuhusu mafanikio.

Kitu kimoja ambacho kimejidhihirisha katika tafiti nyingi zilizofanywa, kuhusu wanaofanikiwa na wanaoshindwa, ni kwamba wale wanaofanikiwa, kuna vitu wanavifanya tofauti kabisa, ambavyo wanaoshindwa hawavijui, au wanavijua ila hawapo tayari kuvifanya, kwa sababu siyo vitu ambavyo wanapenda kufanya.

Mafanikio ni swala na kupandisha maji kwenye mlima, unahitaji kutumia nguvu ya ziada, tofauti na kuyateremsha kwenye mlima, unahitaji kufanya mambo ambayo hutaki kufanya, unahitaji kuonekana wa tofauti, au hata wakati mwingine uonekane umechanganyikiwa.

Leo tunakwenda kuchambua na kujifunza kutoka kwenye kitabu cha mwandishi Mudock, ambaye ameyapitia maisha ya mfalme Selemani, na kuja na siri 31 ambazo zilimfanya afanikiwe sana. Najua kwamba unaposikia jina mfalme Selemani, moja kwa moja picha inayokujia ni ya HEKIMA, kwa sababu huyu ni mmoja wa watu wenye hekima kubwa kuwahi kuwepo kwenye historia ya dunia hii. 

 

Karibu tujifunze kwa pamoja, siri 31 za mafanikio ya mfalme Selemani, tuzitumie ili kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.

1. Selemani aliamua kufanya kitu ambacho hakijawahi kufanywa kabla yake. Aliamua kuwa wa tofauti na wengine. Pale ambapo watu walikuwa wanahofia yeye ndiyo alipata ujasiri, wakati watu wanatembea yeye alikimbia. Selemani alipitia magumu kwenye maisha yake, lakini hakukubali kushindwa, alipambana na kufanikiwa.

SOMO; Usikubali kuwa wa kawaida, fanya kile ambacho wengine hawapo tayari kufanya. NENO; BE UNCOMMON.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Katika Kwenye Kitabu Cha The Art Of Living.

2. Selemani alikuwa na ndoto kubwa ambayo alikuwa na mapenzi nayo. Selemani alijua ni kitu gani hasa anataka kwenye maisha yake, na siku zote alifanyia kazi ili kupata kile anachotaka. Ni watu wachache sana wanaojua ni nini hasa wanataka kwenye maisha yao.

SOMO; Jua ni nini hasa unataka kwenye maisha yako, kuwa na ndoto kubwa unayoipigania.

3. Selemani alifanya HEKIMA kuwa nguzo yake kuu. Imeandikwa kwamba Mungu alipomuuliza Selemani achague chochote anachotaka, alichagua HEKIMA, na kwa kuwa na hekima alipata kila alichokitaka. Selemani alikuwa na hekima kiasi kwamba wafalme wa maeneo mengine walikuwa wakienda kwake kuomba ushauri, na walienda na dhahabu ambazo zilimfanya azidi kuwa tajiri.

SOMO; Kuwa na hekima, jifunze na fanyia kazi yale unayojifunza kila siku.

4. Selemani alikuwa akijiamini, na hili liliwafanya wale wanaomzunguka kumwamini zaidi. Wale wanaojiamini wanakuwa tayari kufanya makubwa, hata kama hakuna mwingine anayefanya, na kule kujiamini kwao kunawafanya wengine wavutiwe kuwa karibu nao.

SOMO; Kabla wengine hawajakuamini, jiamini wewe mwenyewe kwanza. Hakuna mafanikio kama hujiamini.

5. Selemani alitambua mapungufu na madhaifu yake. Hakuna mtu anayejua kila kitu, lakini wengi huwa wanajifanya wanajua kila kitu, hili linawazuia kujifunza na hivyo kushindwa kufanikiwa. Selemani alijua kuna vitu vingi hajui, na hivyo alikuwa tayari kujifunza kwa wale wanaojua. Hili lilimfanya apate hekima na maarifa mengi yaliyomletea mafanikio zaidi.

SOMO; Hujui kila kitu, kuwa tayari kujifunza kila mara na kila wakati, usidharau chochote au yeyote unayekutana naye, kuna mengi ya kujifunza.

6. Selemani alitangaza ndoto yake kubwa kwa kila mtu. Selemani alijua kwamba kuwa na ndoto kubwa na kisha kuifanya siri ni kujidanganya wewe mwenyewe, maana ukikutana na changamoto utakata tamaa, kwa sababu hakuna anayejua. Selemani alitangaza ndoto zake kubwa kwa watu, hii ilimfanya kuendelea kuweka juhudi hata pale anapokaribia kukata tamaa, kwa sababu kila mtu anaijua ndoto yake.

SOMO; Kama una ndoto kubwa kwenye maisha yako, waambie watu waijue wazi, wapo wengi watakupinga na wapo watakaokupa moyo, hao wote watakupa nguvu ya kuendelea kuifanyia kazi, ili kuwaonesha wale wanaokupinga wanakosea, na kutokuwaangusha wale wanaokuunga mkono. Ndoto zangu kubwa mbili ambazo nimekuwa nazisema wazi wazi ni kuwa bilionea (USD) na kuwa raisi wa nchi yangu Tanzania. Zako wewe ni zipi?

SOMA; Kama Unafikiri Huwezi Kuwa Bilionea Soma Hapa Na Uanze Kuelekea Kwenye Ubilionea.

7. Selemani aliomba ushauri wa watu wengine. Hakuomba na kuchukua ushauri kwa kila mtu, bali kwa watu ambao wamefanya kile ambacho anataka kufanya yeye. Au waliofanya makubwa.

SOMO; chochote unachofanya, kuna wengine ambao wameshakifanya, utaokoa muda na nguvu kwa kuomba ushauri kwa njia ya kukutana na hao waliofanya au kusoma vitabu vyao. Usianze mradi au jambo lolote kubwa kwenye maisha yako kabla hujapata ushauri wa ana kwa ana au wa kusoma kutoka kwa yule ambaye ameshafanya.

8. Selemani aliwapenda sana wale wanaomzunguka na aliwashirikisha kwenye ndoto yake kubwa. Selemani alijua ni vigumu kuweza kufikia ndoto zake kubwa bila ya ushirikiano wa watu wengine, na njia bora ya kupata ushirikiano wa wengine ni kuwapenda.

SOMO; Wapende watu, waamini na wao watakuamini kisha washirikishe ndoto yako kubwa, watafurahi kuwa sehemu ya ndoto hiyo, na mtafanikiwa kwa pamoja.

9. Selemani alieleza wazi matarajio yake kutoka kwa wengine. Mara zote alikaa chini na mtu na kuwekeana makubaliano kabla hawajaanza kushirikiana. Hili lilipunguza makosa na hali ya kutokuelewana baada ya kuanza ushirikiano.

SOMO; kitu chochote ambacho unafanya na mtu mwingine, hakikisha mmeelewana vizuri, kuweni na utaratibu ambao upo wazi na kila mtu ajue majukumu yake na matarajio ya mwenzake. Usifanye kitu kwa makubaliano ya juu juu, mtasumbuana baadaye.

10. Selemani alitengeneza mpango wa kufikia ndoto yake kubwa. Hakuishia tu kuwa na ndoto kubwa, badala yake aliweka mpango wa namna gani atafikia ndoto hiyo, kisha akachukua hatua kufikia ndoto zake kubwa.

SOMO; Usiishie tu kuwa na ndoto, bali kaa chini na andika mpango wa utekelezaji wa ndoto yako. usiishie tu kupanga na kuandika mpango, badala yake fanyia kazi kila siku.

11. Selemani alikuwa na ratiba ya matumizi ya muda wake. Alijua ya kwamba zawadi pekee yenye thamani kubwa ni muda, muda ndiyo sarafu ya maisha yetu. Tunapimwa siyo kwa kile tulichopata kwenye maisha, bali kwa jinsi tulivyotumia muda wetu. Kwa maisha yako yote utakuwa unauza muda wako, swali ni je unamuuzia nani na kwa gharama gani?

SOMO; Linda sana muda wako, usiache ukuponyoke, pangilia siku yako kabla hujaianza, usipoteze muda kwa mambo ambayo siyo muhimu kwako. Kupoteza muda ni kupoteza maisha.

12. Selemani alijadiliana kwenye kila kitu alichotaka kwenye maisha yake, hakukubaliana na hali ilivyo, badala yake alijadiliana ili kupata kile ambacho anataka yeye, na siyo kile anachopewa. Katika kuhakikisha anapata kile anachotaka, alihakikisha anajua wengine wanataka nini na kuwapatia. Alitaka kila mtu ashinde, hivyo kupata ushindi mkubwa.

SOMO; Ili upate kile unachotaka, unahitaji kujadiliana na wale ambao wanapaswa kukupa unachotaka. Na katika majadiliano yako, angalia ni namna gani kila mtu anaweza kushinda (WIN – WIN)

SOMA; Falsafa Tatu(3) Za Maisha Yako Na Jinsi Zinavyoweza Kukuletea Mafanikio Makubwa.

13. Selemani mara zote alisikiliza pande zote mbili kabla hajafanya maamuzi. Hili lipo wazi kwenye mfano wa wanawake wawili waliokuwa wanagombea mtoto mchanga. Wanawake hawa wote walikuwa na watoto wachanga, mtoto mmoja akafa, mama wa yule mtoto aliyekufa akamchukua mtoto wa mwenzake na kusema ndiyo mtoto wake. Kesi ilifikishwa kwa mfalme Selemani ambaye aliwasikiliza wote, kisha akasema kwa kuwa kila mtu anamng’ang’ania mtoto huyu, basi nitamkata na kisu katikati kila mtu achukue kipande, mwanamke mmoja alisema sawa, bora kila mtu akose, lakini mwingine akasema usimuue mtoto, bali mpe huyo mwenzangu, mtoto aishi. Hapo Selemani alimpa mtoto yule mwanamke aliyekataa mtoto asiuawe.

SOMO; Kabla hujafanya maamuzi, kabla hujahukumu, hebu jaribu kusikiliza pande zote mbili, utajifunza mengi ya kukusaidia kufanya maamuzi sahihi.

14. Selemani mara zote alisisitiza mikataba kabla ya kufanya kitu. Mara zote alihakikisha amejua kitu vizuri kabla ya kuingia, hii ilimwepusha kufanya maamuzi ambayo siyo bora kwake.

SOMO; usiamini vitu juu juu, badala yake jua kwa undani. Kabla hujaingia makubaliano ya kikazi au kibiashara na mtu, ni vyema mkawa na makubaliano yaliyoandikwa, vinginevyo mtakuja kuumbuana.

15. Selemani mara zote aliajiri watu wenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi aliyotaka ifanywe. Hakuchukua tu mtu ni mtu, bali alihakikisha anachukua aliye bora, ambaye atatoa matokeo bora.

SOMO; Unapoajiri, usiangalie mtu anayetaka tu kazi, au ambaye yupo tayari kulipwa fedha kidogo, bali ajiri mtu aliye bora, anayeweza kuleta matokeo bora.

16. Selemani alikataa kuharakisha mambo. Mara zote Selemani alijipa muda wa kutafakari na kujifunza kabla hajafanya mazoezi. Alijua kabisa kuharakisha lazima ukosee. Kudhibitisha hili muulize mtu yeyote ambaye amewahi kuibiwa, kutapeliwa au kufanya makosa, mara nyingi aliharakisha au aliharakishwa. Ukishaona watu wanakusisitiza uharakishe kwa sababu ukichelewa utaikosa fursa, nusa harufu ya kuibiwa au kutapeliwa.

SOMO; Usiharakishe kufanya maamuzi, jipe muda w akutafakari na kujifunza kabla hujaamua ni hatua zipi unazochukua.

17. Selemani alitumia muda wake vizuri kwenye maeneo ambayo yanamletea matokeo bora. Hakuishia tu kupangilia muda wake, bali alihakikisha ameweka vipaumbele kwenye yale maeneo na mambo ambayo ni muhimu kwake.

SOMO; Kuwa na vipaumbele vya maisha yako, na ugawe muda wako kulingana na vipaumbele vyako. Popote unapowekeza muda wako mwingi, ndiyo matokeo utakayopata kwenye maisha yako.

18. Selemani alikuwa tayari kukabiliana na wapinzani wake. Selemani alijua migogoro haikosekani, na njia sahihi ya kutatua migogoro ni kukabiliana na wale ambao una mgogoro nao. Selemani hakuacha mgogoro ukue bila ya kutatuliwa, badala yake alihakikisha kila mtu ambaye ana mgogoro naye, unamalizwa kwa kutatuliwa au kwa mtu huyo kuondolewa kabisa.

SOMO; Usiache mgogoro wowote ukue, kitu ambacho kilikuwa kidogo kinaweza kukua na kuleta madhara makubwa baadaye. Kabiliana na wale ambao una matatizo nao kwa sasa, na tatueni matatizo hayo.

SOMA; Una Nini Cha Tofauti Mpaka Watu Wakufuate Na Kukusikiliza? Jua Hapa.

19. Selemani alikuwa na hamasa kubwa ya kufikia ndoto yake kila siku. ni kawaida kwa watu kuwa na hamsa pale wanapoanza ndoto zao, lakini baadaye hamasa hii hupotea kabisa na mwishowe kukata tamaa. Selemani alijua moto wowote ambao hauchochewi huwa unazima, hivyo alichochea ndoto yake kubwa kila siku, kwa kukutana na watu wanaohusika na ndoto yake.

SOMO; usikubaki ule moto wa mafanikio unaowaka ndani yako uzime, na kama hutaki uzime unahitaji kuuchoche kila siku. jihamasishe kila siku kwa kujifunza na kufanyia kazi ndoto yako hata kama ni kwa hatua ndogo. Pia zungukwa na wale watakaokuhamasisha kuliko kuzungukwa na wanaokukatisha tamaa.

20. Selemani alikataa kabisa kuvumilia ukosefu wa uaminifu. Kukosa uaminifu ni kasa mbaya ambayo inaweza kubomoa maisha ya mtu yeyote. Selemani alipoona mtu aliyemwamini amekosa uaminifu, hakumvumilia hata kidogo, alimchukulia hatua mara moja. Unapofanikiwa unakaribisha watu wengi, ukiwaruhusu watu ambao siyo waaminifu kuwa karibu na wewe, watakuangusha.

SOMO; kuwa mwaminifu, halafu usijihusishe kabisa na mtu ambaye siyo mwaminifu. Ataharibu mafanikio yako.

21. Selemani alikuwa mtu wa shukrani. Selemani alishukuru kwa kila kitu kilichokuwa kinatokea kwenye maisha yake, kwa njia hii alizidi kupata zaidi na zaidi. Je wewe ni vingapi unavyo mpaka sasa lakini umekuwa hushukuru, badala yake ni kunung’unika kwa yale uliyokosa?

SOMA; Shukuru kwa kila jambo kwenye maisha yako, unapokuwa mtu wa kushukuru, unapata mazuri zaidi kwenye maisha yako.

22. Selemani alikuwa na washauri (MENTORS) na aliwaamini washauri wake. Washauri, MENTORS ni daraja kati yako na mafanikio yako, hakuna mtu ambaye ameweza kufanikiwa yeye mwenyewe, unahitaji kuwa na washauri, iwe ni wa moja kwa moja au wasio wa moja kwa moja. Lazima kuwe na watu ambao unawaangalia na wanakusukuma zaidi kuelekea kwenye mafanikio yako.

SOMO; Kama upo makini na mafanikio unayoyataka, unahitaji kuwa na MENTORS katika safari yako ya mafanikio, tofauti na hapo unapoteza muda wako, maana utakuwa unafanya makosa na kurudia makosa yale yale kila mara.

23. Selemani alijifunza kutokana na majanga yake. Hakuna wakati mzuri wa kujifunza kwenye maisha kama wakati wa majanga. Selemani alijua majanga yanamfika kila mtu na njia bora ni kujifunza kupitia majanga hayo ili kuwa bora zaidi. Tofauti ya matajiri na masikini ni matajiri wanayapokea majanga na kujifunza, wanafanikiwa kutokana na majanga waliyopitia. Lakini masikini wanayakimbia majanga, na kuyatumia kama sababu ya kutokufanikiwa.

SOMO; Jifunze kupitia majanga na magumu unayopitia, usiyatumie kama sababu ya kushindwa, bali yatumie kama sababu ya kufanikiwa.

24. Selemani alichunga sana maneno ya kinywa chake. Alijua sumu ya maneno ya hovyo na namna yanaweza kuvuruga amani na mahusiano mazuri. Selemani alichagua maneno yake vizuri ili kuhakikisha haleti maana mbaya kwa wale anaozungumza nao. Ni mara ngapi umewahi kusema neno kwa nia njema lakini watu wakachukulia ulikuwa na nia mbaya? Hapo jua hukuchagua maneno yako vizuri.

SOMO; linda sana ulimi wako, chagua kwa makini maneno unayotumia katika mawasiliano yako na wengine. Neno dogo linaweza kuleta matatizo makubwa.

25. Selemani hakuwahi kupoteza muda wake kubishana na mpumbavu. Selemani alikuwa mkali sana juu ya wapumbavu, na alisema wazi kwamba kwa namna yoyote ile usijihusishe na mpumbavu, usimsahihishe, wala usimkosoe kwa sababu atakuona wewe ndiye unayekosea na kukupotezea nguvu zako. Hakuna kipindi ambacho ushauri huu ni mzuri kama sasa, maana wapumbavu wanazidi kuwa wengi kadiri siku zinavyokwenda, kaa nao mbali, watakuhamisha kwenye safari yako ya mafanikio.

SOMO; Wajue wapumbavu, na waepuke haraka sana, usijaribu kubishana au kumwelewesha mpumbavu, hata kuelewa na atakupotezea muda wako. Mpumbavu ni mtu asiyejua, na hajui kama hajui, hivyo mara zote hujiona yupo sahihi kuliko wengine.

26. Selemani aliwazawadia wale ambao walimsaidia kufikia ndoto yake. Alijua ili kuwahamasisha watu kuweka juhudi zaidi, unahitaji kutambua mchango wao na kuwapa zawadi kulingana na juhudi wanazoweka. Kile ambacho watu wanazawadiwa, ndicho wanachoendelea kufanya.

Somo; wape watu zawadi kutokana na juhudi wanazoweka kukusaidia kukamilisha ndoto yako. iwe ni wafanyakazi au washirika, kile unachowazawadia watu kwa kufanya, wataendelea kukifanya.

27. Selemani alijijengea sifa ya HEKIMA na UADILIFU. Kinachokufikisha kwenye mafanikio, ni ile sifa yako, jinsi ambavyo watu wanakuchukulia. Na hii inatokana na namna unavyofanya mambo yako, wala siyo kwa jinsi unavyosema unafanya, bali jinsi unavyofanya. Selemani alihakikisha maneno yake na matendo yanaendana.

SOMO; Kwa mwadilifu, timiza lile unaloahidi, fanya kile unachosema utafanya, na mara zote hutakosa cha kufanya, utaaminika na wengi.

28. Selemani alielewa nguvu ya muziki katika kutuliza akili na kupumzika. Selemani alikuwa na nyimbo nyingi ambazo zilimburudisha. Na yeye mwenyewe aliweza kuandika nyimbo zake, zaidi ya elfu moja.

SOMO; Chagua miziki ambayo inaendana na wewe, ambayo ukiisikiliza moyo wako unasuuzika, na mwisho wa siku unapokuwa umechoka, sikiliza miziki hiyo, utapata nguvu na hamasa ya kuendelea na mapambano. Unajua ni kwa nini majeshi yana bendi za muziki?

29. Selemani alihakikisha wale wanaomjua ni watu ambao ni wa muhimu kwake. Hakuruhusu kila mtu ajue maisha yake binafsi, kwa sababu alijua kwa kufanya hivyo anawapa watu nafasi ya kutumia taarifa hizi kumwangamiza. Pamoja na mengi kuandikwa kuhusu Selemani, ni machache sana yanayojulikana kuhusu maisha yake binafsi.

SOMO; Usiyaanike maisha yako hadharani, usitake kila mtu ajue kila kitu kuhusu maisha yako, taarifa nyingine zinapaswa kuwa kwako na kwa wale unaowajua tu. Huwezi kujua ni mtu gani atachukua taarifa zako na kuzitumia vibaya kujifaidisha. Na hili ni gumu sana hasa enzi hizi za mitandao ya kijamii, ambapo watu wanasukumwa kutangaza kila kitu cha maisha yao.

30. Selemani aliajiri watu ambao wana furaha, hakuajiri mtu asiye na furaha. Hii ni kwa sababu watu wenye furaha wana ufanisi mkubwa, wana hamasa na siyo watu wa kulalamika kila wakati. Ni watu ambao wanawahamasisha wale wanaowazunguka.

SOMO; ajiri na fanya kazi na watu wenye furaha. Kama utafanya kazi na watu ambao hawana furaha, watu ambao kila wakati wanalalamika na kunung’unika, kila siku yako itakuwa hovyo na utaona kukata tamaa. Zungukwa na watu wenye furaha.

31. Selemani alikuwa mwaminifu kuhusu ukomo wa utajiri wake. Licha ya kuwa mtu tajiri kuliko wote, lakini alijua kuna mambo ambao utajiri hauwezi kutatua. Licha ya kuwa na dhahabu, ardhi na kila aina ya mali, kuna nyakati ambazo Selemani alikuwa mpweke na alikiri kwamba wote tumetoka mavumbini na mavumbini tutarudi, bila ya kujali una utajiri kiasi gani.

SOMO; Hata uwe tajiri mkubwa kiasi gani, kuwa mnyenyekevu, jua kuna vitu ambavyo fedha haiwezi kutatua. Kuwa na maisha ya kawaida, ambayo yanakuridhisha wewe na yana mchango kwa wale wanaokuzunguka.

Kuna mengi sana ya kujifunza kutoka kwa mfalme Selemani, aliandika vitabu vingi vya misemo na nyimbo, aliweza kuwaongoza watu wake kwa haki na kupata utajiri mkubwa. Tunaweza kujifunza haya na sisi pia tukawa na maisha bora kama aliyokuwa nayo yeye.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita